📌ATLEY KUNI-TAMISEMI
SERIKALI imelegeza
masharti ya kukopa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa halmashauri kwa vikundi vya
wanawake, vijana na walemavu ili kuviwezesha vikundi vingi zaidi kukopa.
Kauli hiyo imetolewa
leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo wakati akifunga mkutano mkuu wa nne wa maafisa
maendeleo jamii.
Waziri Jafo amesema
kuanzia leo tarehe 26 Februari, 2021, Serikali imerekebisha na kutoa kanuni
mpya ambazo zimechapishwa kwenye gazeti la Serikali ili zianze kutumika na kuwa
moja ya kigezo kilicholegezwa ni kupungua kwa idadi ya wanavikundi.
“Kigezo cha kuwa na
idadi ya watu kumi kwa vijana na wanawake na watu watano kwa walemavu, kwa muda
mrefu kimechangia kwa baadhi ya watu waliokubaliana na malengo yanayofanana
kushindwa kuungana.”
“Kanuni mpya zinasema
kwa vikundi ya vijana na kina mama wakipatikana watano kikundi hicho kinaweza
kukopesheka, lakini tumeenda mbali zaidi kubadilisha kanuni kumwezesha hata mtu
mmoja mwenye ulemavu aweza kupewa mkopo, haya ni mapinduzi makubwa,” amesema
Waziri Jafo
Amesema kuanza
kutumika kwa kanuni hizo mpya kutatoa fursa kwa vikundi vingi kuwa na sifa ya
kupata mikopo hiyo.
Waziri Jafo katika
eneo lingine ambalo limeimarishwa ni suala la urahisishwaji wa ufuatiliaji wa
mikopo kwa Serikali kwa kutenga fungu kulingana na ukopeshaji wa kila mamlaka.
Kuanzia sasa kanuni mpya zinaelekeza kwa kila halmashauri kutenga kiasi cha fedha ili kuwawezesha maafisa maendeleo jamii kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mikopo iliyotolewa
Akifafanua zaidi,
Waziri Jafo amesema kwa halmashauri ambazo mapato yake ya ndani hayazidi
shilingi bilioni moja katika kila marejesho idara ya Maendeleo ya Jamii
itatengewa shilingi laki tano wakati halmashauri ambazo mapato yake ni zaidi
shilingi bilioni moja zimeelekezwa kutenga kati ya Sh milioni moja na shilingi
milioni moja na nusu kwa mwezi kwa ajili ya ufuatiliaji.
Aidha kwa halmashauri
ambazo mapato yake yapo kati shilingi bilioni tano, na kuendelea amesema idara
ya maendeleo ya jamii ipatiwe shilingi milioni tano kwa ajili ya tathmini na ufuatiliaji.
Sambamba na maboresho
hayo, waziri Jafo amewataka, wataalamu wa kada hiyo, kwenda kusimamia ipasavyo
marejesho ya mikopo na atakayeshindwa kufanya hivyo, basi atakuwa ameshindwa
kazi.
Katika hatua nyingine
Waziri Jafo, ameziagiza Mamalaka za Serikali za Mitaa, kuhakikisha
wanawahusisha wataalamu wa Maendeleo ya Jamii, kwenye Miradi yote
inayotekelezwa katika eneo husika kuanzia hatua za awali.
Amesema kutokana na
umuhimu wa Maafisa Maendeleo Jamii kama wahamasishaji wa Jamii kwenye shughuli
za Maendeleo, ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwashikisha wataalam wa
kada hii katika miradi yote inayotekelezwa.
Kufuatia kauli hiyo ya
Waziri Jafo, akizungumza kwa niaba ya Maafisa Maendeleo Jamii wenzake, rais
mpya wa chama hicho Angela Kiama, amesema wamepokea kwa furaha mabadiliko
ambayo serikali imeyafanya katika kanuni.
Tatizo lilikuwepo mathalani kwa walemavu, unaweza kukuta mlemavu mmoja katika eneo anashindwa kupewa mkopo kwa kigezo cha kuwataka wawe kikundi, kwa kweli tunaishukuru sana serikali kwa kuliona hili na kufanya maboresho kwenye kanuni hizo.
Kiama.
Maafisa Maendeleo
Jamii hao waliokutana kwa siku tatu kutathmini hali ya utendaji wao wa kazi
sambamba na kuwachagua viongozi wa chama chao.
Mkutano mkuu wa
Maafisa Maendeleo ya Jamii, ni wa nne tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka
2017, na ulikuwa na kauli mbiu, “Maafisa Maendeleo ya Jamii Nguzo Muhimu
kufikia Uchumi wa Viwanda” huku ukiwa umewashirikisha maafisa wa kada hiyo
kutoka serikalini na taasisi binafsi.
0 Comments