📌MWANDISHI WETU.
SERIKALI imebaini uwepo
wa mkakati wa kukwamisha kuanza kwa ujenzi wa viwanda vingi vya kuchakata miwa
ya wakulima ili nchi isijitosheleze kwa uzalishaji wa sukari nchini.
Kauli hiyo ya serikali
imetolewa leo (17.02.2021) na Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda wakati
akiongea na wakulima wa miwa wa bonde la Mbigiri wilayani Kilosa mkoa wa
Morogoro ambapo ameeleza kuwa bado wamiliki wa viwanda vya kuzalisha sukari
vilivyopo nchini wameshindwa kununua miwa yote ya wakulima
Waziri huyo amesema kuwa
kuna taarifa za uhakika kuwa baadhi ya watu wasioitakia mema nchi wanakwamisha
jitihada za kuanzishwa kwa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mkulazi II hatua
ambayo inayoendelea kuwaumiza wakulima wa miwa kwa mazao yao kutupwa kwa kukosa
wanunuzi wa uhakika
“Nawahakikishia ninazo
taarifa kwamba sasa kiwanda kitakamilika na kuanza kazi haraka, kwa hiyo
wakulima msiwe na wasiwasi na soko la miwa. Anayezuia kiwanda hiki cha Mkulazi
II kisianze kazi serikali itachukua hatua kali. Tunawashukuru wakulima kwa
uvumilivu wenu, serikali haitawaangusha” alisema Prof. Mkenda
Kwa muda wa miaka
mitatu sasa tangu mwaka 2018 wakulima wa miwa wa Bonde la Mbigiri wilaya ya
Kilosa wamekuwa wakihangaika kuuza miwa yao kutokana na kiwanda cha Mkulazi
kushindwa kukamilika huku wakulima wakiendelea kudaiwa mikopo ya fedha
walizokopeshwa na Benki ya Azania
Katika hatua nyingine
Waziri Prof. Mkenda ametoa onyo kwa wawekezaji wa viwanda vya sukari Kilombero na
Mtibwa kuondoa zuio la wakulima kuuza miwa yao kwa watu wengine kwa kigezo cha
kulinda soko la ndani hatua inayosababisha wakulima miwa kukosa soko na nchi
kuendelea kuwa na upungufu mkubwa wa sukari.
Waziri Mkenda aliongeza
kuwa wizara itaangali upya marufuka hiyo ya kuzuia wakulima kuuza miwa
inayowapa nafuu kampuni za Kilombero na Mtibwa pekee kuwa wanunuzi wa miwa ya
wakulima hivyo wafanyabiashara wengine wenye nia ya kununua miwa kushindwa.
Amesema kunapokuwa na wanunuzi wengi wa miwa kunaleta nafuu kwa wakulima ambao
huchagua nani wamuuzie miwa na kuongeza ushindani wa bei katika soko
“Leo mkulima wa miwa
hana soko la uhakika alafu Mtibwa Sugar anataka serikali imlinde wakati tunahitaji maslahi mapana kwa wakulima wetu.
Kazi yangu kama Waziri wa Kilimo ni kumlinda mkulima, siwezi kulinda marufuku
ya kuzuia miwa popote iendelee, tutachukua hatua . Kwanini tumzuie mkulima auze
miwa yake popote” alisisitiza Waziri Mkenda.
Prof.Mkenda amehoji “
ni uchumi gani kumzuia mkulima auze miwa yake kwa mtu anayetaka kununua halafu
mwekezaji anataka serikali imlinde wakati yeye hanunui na zaidi ya tani 350,000
za miwa huharibika mashambani “ kisha akawataka wakulima wa Kilosa na Mvomero
kuwa na subira wakati mkakati wa kuanzisha kiwanda cha Mkulazi ukikamilika.
Wakulima wa miwa wa kijiji
cha Mbigiri walimweleza waziri huyo kuwa kutokuanza kwa kiwanda cha sukari cha
Mkulazi kumesababisha washindwe kurejesha mikopo walipopewa na benki ya Azania
mwaka 2018 na kuwa sasa imefikia wanadaiwa riba ya asilimia 6 ikiwa ni adhabu
kwa Kuchelewa kurejesha asilimia 50 ya mikopo.
“Sasa imefika wakati
mkandarasi aliyetulimia mashamba anadai fedha za kulima ambapo ametuzuia
tusivune miwa yetu. Tunaomba wizara isaidie mkandarasi aliyepewa kazi na
kampuni ya Mkulazi alipwe fedha zake ili
na sisi turuhusiwe kuvuna mashamba yetu” alilalamika Godfery Philipo mkulima wa
miwa wa Mbigili.
Naye Mkulima Saidi Mazunde wa Mbigiri alisema
tatizo la kudaiwa kukatwa riba ya asilimia sita zaidi limetokana a mkataba kati
ya Kampuni ya Mkulazi , AMCOS na wakulima kuwa kitakapoanza kiwanda wakulima
wote watauza miwa yao huko .Sasa ni miaka mitatu kiwanda hakijaanza na mkulima anaonekana kupewa adhabu.
“ Hii asilimia 6 ya riba
ya adhabu tunaomba ibebwe na Mkulazi kwa kuwa ndio waliotushawishi tulime kwa
kuwa wataanzisha kiwanda hapa Mbigiri” alisema Mazunde.
Kwa upande wake
Mwenyekiyi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Dkt. Chritine
Ishengoma alisema wakulima wasikate tamaa na kuacha kulima miwa kutokana na
kiwanda Kuchelewa kuanza bali wawe watulimvu kwa kuwa seriklai ya awamu ya tano
imepokea kilio chao kwa Waziri wa Kilimo kuja kuwasilikiza .
“Wakulima wangu msife
moyo mkachukua hatua za kuchimbua miwa,Tunataka kilimo kimkomboe mkulima hivyo
kwero zenu zitapatiwa ufumbuzi haraka.” Dkt. Ishengoma
Prof. Mkenda
akihitmisha ziara yake mkoa wa Morogoro leo ameiagiza Bodi ya Sukari nchini
kukutana na viwanda vya sukari vyote nchini kuweka utaratibu wa kupima viwango
vya utamu wa sukari kutumika kuuzia miwa badala ya matumizi ya mizani hatua
inayolalamikiwa na wakulima .
Pili ametoa rai kwa
taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutoa mikopo kwa
wawekezaji wa ndani wenye nia ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata
miwa na kuzalisha sukari hatua itakaoondoa utegemezi wa viwanda vikubwa vya
sukari.
Na tatu,wizara
itafanyia kazi marufuku ya kuuza miwa nje ya eneo la mwekezaji iliyopo hatua
inayodidimiza jitihada za serikali kukuza uzalishaji wa miwa kwani imeonekana
ni njama ya kuwaumiza wakulima na kupeleleka miwa kuharibika shambani bila
soko.
Waziri Mkenda amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Morogoro leo amabpo alitembelea vowanda vuya sukari vya Kilombero, Mtibwa na skimu za umwagiliaji Msolwa Ujamaa pamoja na kukongea na wakulima wa miwa kwenye wilaya za Kilombero, Mvomero, Kilosa na Morogoro.
Imeandaliwa na;
Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Kilimo
Morogoro
17.02.2021
0 Comments