📌HAMIDA
RAMADHANI.
SERIKALI imesema kuwa
kwa sasa haina mpango wa kupokea chanjo ya ugonjwa wa Corona (COVID 19)
inayoripotiwa kuwepo na kutumika katika mataifa mengine.
Hayo yamebainishwa leo
na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Doroth
Gwajima, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Dk, Gwajima amesema
kuwa, kutokana na mlipuko wa pili wa ugonjwa wa corona katika mataifa jirani,
amekuwa akipokea maswali mengi kutoka vyombo vya habari kuhusu matumizi ya
chanjo hiyo, pamoja na njia za kujikinga.
“Naomba ifahamike kuwa
serikali kupitia wizara ya Afya inazo taratibu zake za kufuata pale inapotaka
kupokea bidhaa yoyote ya afya na hufanyika baada ya serikali kijiridhisha hivyo
sasa ni hadi tujiridhishe na siyo vinginevyo”ameeleza Dk, Gwajima
Amesema, kuhusu mbinu
za kujikinga na ugonjwa huo Wizara inaendelea kuwakumbusha wananchi kujielekeza
kwenye elimu ambayo imekuwa ikitolewa na wataalamu wa afya.
“Hii ni pamoja na
kuimarisha usafi, kujifukiza, kufanya mazoezi, kula lishe bora, kunywa maji
mengi bila kusahau matumizi ya tiba asili ambazo taifa hili limejaliwa”amesema
Dk. Gwajima
Amesema Wizara kwa
kushirikina na Mkemia Mkuu wa Serikali na Baraza la tiba asili na wananchi
watengenezaji wa tiba ya asili tayari wameshafanya usajili wa bidhaa za tiba
asili.
Dk, Gwajima alisema
kuwa upo ushahidi wa kutosha kuhusu watu wengi ambao wamepata nafuu na kupona
magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza mara baada ya kutumia
dawa za tiba ya asili hataka kama walikuwa kwenye matibabu ya hospitali
“Naomba wataalamu wote
na wajuzi wa tiba asili wasisite kujitokeza kufuata taratibu za kuwasilisha
dawa na bidhaa zao kwa mamlaka ya maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali ili
zifanyiwe uchunguzi “amesisitiza Waziri huyo wa Afya.
Amesema Wizara hiyo,
itawapa ushirikiano mkubwa wote watakajitokeza na kujiandikisha kupitia
madawati ya tiba asili yaliyoko katika halmashauri na mikoa.
“Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imedhamiria kuinua huduma za tiba ya
asili”amebainisha
Kadhalika, amesema kuwa
analielekeza Baraza la tiba asili kutoa orodha ya dawa zote ambazo zimepita
kwenye utaratibu wa kufanya uchunguzi wa kimaabara na maabara ya Mkemia Mkuu wa
serikali na kuonekana kuwa ni salama.
“Ifahamike kuwa dawa
nyingi zinazotumika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya zinatokana na miti
au mimea kwa mfano dawa ya kwinini inatengenezwa kutokana na mti wa
mkwinini ambao hapa Tanzania unastawi maeneo ya Lushoto, Korogwe na
Mufindi”amefafanua Dk, Gwajima
Pia, amesema kuwa
serikali itaendelea kuchukua tahadhari zote za ufuatiliaji wa mwenendo wa
magonjwa yote kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote na kuelimisha wananchi
juu ya hatua za kuchukua.
“Nawaelekeza Waganga
wakuu wa Mikoa, Wilaya na Waganga wafawidhi na Maafisa afya mazingira nchini
kote, kuendelea kuimarisha mifumo yote ya udhibiti na kinga ya magonjwa kwa
kushirikiana na wananchi ili kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza na yasiyo
ambukiza”alisema Dk. Gwajima
Hata hivyo,
amezikumbusha Taasisi zote za Umma, Binafsi, Kidini, Kijamii na Vyombo vya
habari kuepuka kutoa taarifa za afya ambazo hazifuati miongozo ya wizara
zinazoleta taharuki kwa wananchi.
“Ieleweke kuwa taasisi
zetu zote kama shule, vyuo, taasisi za kijamii na kidini zinawajibika kwa
Wizara zao husika katika kutoa taarifa zozote au kuchukua maamuzi yanayoweza
kugusa maisha ya wananchi wengine”ameeleza
Mwisho
0 Comments