MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibr (TAMWA ZNZ) katika kutetea na kupambania haki za wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi nchini.
Mkuu huyo wa mkoa
ametoa Pongezi hizo ofisini kwake wakati wa kikao tendaji na wanaume mawakala
wa mabadiliko ambao wamewezeshwa na TAMWA ZNZ chenye lengo la kujadili na
kuwakumbusha viongozi wa mikoa juu ya umuhimu wa kuzingatia usawa wa kijinsia
katika uteuzi wa nafasi mbalimbali hasa kuanzia ngazi ya Shehia na Wilaya.
Amesema Serikali
inatambua na kuthamini kwa kiasi kikubwa juhudi zinazochukuliwa na TAMWA
Zanzibar katika kujenga jamii yenye kuzingatia haki na usawa katika ngazi za
maamuzi na kuahidi kuendelea kutoa mashirikiano ili kuhakikisha malengo ya
usawa wa kijinsia yanafanikiwa katika kila sekta.
“Serikali inatambua
sana harakati na juhudi za TAMWA katika kutetea haki za wanawake, lakini bado
tunayo kazi kubwa ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya dhana ya wanawake
na uongozi kwani suala hili ni suala la kihistoria hivyo linahitaji muda zaidi
wa kuweza kufanikiwa,” alisema.
Aidha mkuu huyo wa
Mkoa amesema kuwa licha ya juhudi hizo lakini pia bado kuna haja ya kujikita
zaidi katika kuwaandaa wanawake kuwa viongozi ili kuwawezesha kutekeleza kwa
ufanisi zaidi majukumu yao pale wanapopata fursa ya kuwa viongozi katika nafasi
mbalimbali.
“Ni lazima tutambue
kuwa bado kunahitajika nguvu zaidi kwanza za kuwaandaa wanawake kuwa viongozi
ili waweze kuwa na ubora katika utendaji kwani mara nyingi nafasi za uongozi
haziangalii tu suala la kijinsia bali uwezo, maadili na uwajibikaji wa mtu
mwenyewe katika utendaji kwa lengo la kuleta ufanisi wa kazi,” alisema mkuu
huyo wa Mkoa.
Hata hivyo amekishauri
chama hicho kuendelea kuwatumia zaidi viongozi wa dini ili kusaidia kubadili
mitazamo ya jamii juu ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.
Alisema, “nawapongeza
pia kwa mbinu mnazotumia kwa kuwashirikisha viongozi wa dini katika masuala
haya, nikuombeni tuendelee kuwatumia sana viongozi hawa ili watusaidie kubadili
mitazamo ya jamii yetu kwani inaonekana kwamba dini ni kikwazo kwa wanawake
kugombea nafasi za uongozi.”
Katika hatua nyingine
Mattar ameahidi kuweka kipaumbele kwa wanawake katika nafasi mbalimbali za
uogozi kwenye Shehia kwa kuzingatia uwezo wa atakayeweza kusaidia katika
utendaji.
“Tukipata fursa
tutazingatia ushiriki wao kwa namba kwa kuangalia zaidi uwezo na nani ataweza
kutusaidia kwa ufanisi,” alisema.
Mratibu wa TAMWA
Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said akizungumza mbele ya mkuu huyo wa
Mkoa alisema Chama hicho kinatekeleza mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki
katika nafasi za uongozi wenye lengo la kujenga uwezo wa wanawake Zanzibar
kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi na siasa.
“Taasisi yetu
inatekeleza mradi huu kwa lengo la kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi
mbalimbali za uongozi na siasa kupitia kuhamasisha jamii kukubali kuwa mwanamke
nae anaweza kuwa kiongozi,” alisema.
Nae mjumbe wa wanaume
mawakala wa mabadiliko Dr. Amour Rashid Ali alisema mawakala hao wanafanya
mikutano na makundi mbalimbali katika jamii kwa lengo kushawishi na kutetea
haki za wanawake kwenye uongozi.
Alisema, “Wanaume
mawakala wa mabadiliko tumejitolea kufanya mikutano na makundi mbalimbali
kwenye jamii kwa lengo la kutoa elimu ili jamii itambue kuwa wanawake nao wanao
uwezo wa kuwa viongozi.”
Kikao hicho cha Mkuu
wa Mkoa na wanaume mawakala wa mabadiliko ambao wamewezeshwa na TAMWA Zanzibar
ni mwendelezo wa juhudi za Chama hicho kutetea na kuhamasisha ushiriki wa
wanawake katika nafasi za uongozi na Siasa.
0 Comments