KWANINI TUNASHEREKEA SIKU YA VALENTINE DAY?

 

📌DOTTO KWILASA.


JANA ilikuwa siku ya wapendanao  ambayo ni maarufu kwa  jina la “Valentines Day ”siku hii Pamoja na Mambo mengine hutumika  na wengi Katika kuelezea hisia za upendo kwa ndugu,jamaa na marafiki.

Hata hivyo,katika kusherehekea inatupasa kutafakari kwa kina na kufahamu malengo na maana ya siku hii  ambayo kwa kawaida hufanyika kila mwaka ifikapo  February 14.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ,Neno Valentine lilitokana na jina ‘Valentino’ huyu alikuwa Mtakatifu wa Kiroma aliyeitwa Valentino,sikuya Valentino hufahamika kama Siku ya wapendanao na wengi wanaiita‘Valentine Day’ ni maadhimisho ambayo hufanyika kila  mwaka sehemu
nyingi Duniani.

Watu wengi husherehekea siku hii kwa kuonyesha upendo,kuthaminiana pamoja na kujaliana kati ya watu wenye mahusiano mbalimbali ya karibu japo mara nyingi siku hii hutumiwa na walio kwenye mahusiano ya kimapenzi.


Hata hivyo baadhi ya watu huitumia siku hii kufanya ibada ikiwa ni ishara ya kumuenzi Mtakatifu Valentino ambaye kihistoria inamtaja kuwa ndiye chanzo cha siku hii.

Kwa kawaida kabisa asili ya  Siku hii ni baada ya wakristo wa zamani kuteswa hadi kufa
kwa ajili ya kuupenda Ukristo na Kihistoria ambapo Mtakatifu Valentino alitumika kama kiongozi wa dini kanisani katika utawala wa mfalme Claudia II.

Mfalme Claudia II alimkamata na kumfunga,Mtakatifu Valentino nakumtesa kwa ajili ya Imani yake ya Kikristo na Kufa  February 14 Kwaajili ya msimamo,imani yake na kufa kwa kutetea Ukristo .

Hivyo historia inaeleza kuwa Papa Gelasius aliitangaza February 14 kuwa siku
ya Mtakatifu Valentino mnamo mwaka 496 AD.

Kwa mujibu wa kumbukumbu nyingi za kihistoria kuihusu siku hii, inatupasha kuwa kipindi hicho ,vijana wengi hawakupenda vitakwa kuogopa kuziacha familia zao  na hivyo kupingana na kiongozi waoClaudis ambaye alitaka awe na jeshi kubwa akategemea vijana wangejitolea na kujiunga na jeshi lake.

Claudis akafikiria akaona hawa vijana kuwakomesha waingie jeshini ni kupiga marufuku watu kuoana ambapo Kuanzia hapo akapiga marufuku watu kuoana akitegemea vijana hawatajali sasa kujiunga na jeshi kwasababu ya familia zao.

Jambo hili halikuwa rahisi kwa baadhi ya viongozi wa dini hususani Askofu Valentine ambaye kwa usiri mkubwa akawa anawafungisha ndoa vijana hao kwa siri  na kusisimua hasira za Claudius ambapo aliposikia habari hizo aliamuru Valentine akamatwe na akahukumiwa adhabu ya kifo cha kunyongwa.

Wakati akiwa jela akisubiri siku yake ya kunyongwa Valentine alikuwa akitembelewa na vijana waliokuwa wakimpelekea maua kuonyesha wako pamoja nae ikiwa ni pamoja na kumpa moyo wa ushujaa na uvumilivu.

Mmoja wa vijana hao ni mtoto wa mkuu wa gereza ambaye aliruhusiwa kuingia mpaka kwenye selo la Valentine kuongea nae mambo mbalimbali .

 Hata hivyo siku hii bado inapewa heshima yake na wakristo kwa sababu,ndiyo maana kila ifikapo February 14 ya kila mwaka huwa kuna ibada maalumu ya kushikilia na kujikita imara katika ukristo .

 Hii ni katika kuuenzi uimara wa Valentino mwenyewe ambapo wakati mfalme alipotaka kumsamehe kwa sharti aache ukristo na kuabudu miungu ya Kirumi ili awe msiri wake na awe mkwe wake lakini bado alishikilia imani yake kwamba watu Wana haki ya kuoa na kuolewa. inasemekana kwamba Valentine aliangukia katika mapenzi na binti huyo

wa mkuu wa gereza wakati anasubiria kunyongwa na  kwamba muda mchache kabla hajanyongwa Valentine aliomba kalamu na karatasi na kuandika meseji yake ya kuaga akiweka sahihi ikisomeka hivi"From Your Valentine" ( kutoka kwa Valentine wako ) akanyongwa tarehe 14 februari
mwaka 269 AD.

Kwa mujibu wa mtandao mmoja wa habari wa kimataifa  mtakatifu Valentine alikataa ahadi hiyo na akapendelea ukristo, kwa hiyo akauliwa siku ya tarehe 14 Februari 270 CE ndo ikaitwa siku hii kwa
jina la huyo mtakatifu (Valentine). 

Papa (Pope) naye akaifanya siku hiyo ya kufa Saint Valentine tarehe 14 Februari 270 CE kuwa ni sikukuu ya mapendo papa huyo alikuwa ni Askofumkuu wa kanisa la 'Universal Church', ambaye ni mrithi wa mtakatifu Peter.


Baada ya kunyongwa kwa Valentine, vijana wa Roma walianza kumuiga Valentine na kuwaandikia na kuwatumia wanawake waliowapenda salamu za mapenzi.

Tangu siku hiyo tarehe hiyo ikaanza kuhusishwa na dini, urafiki, upendo na mahaba duniani huku ikihusishwa zaidi na mambo ya mapenzi.

Siku hiyo imezidi kuwa maarufu kila miaka inavyoenda huku  makampuni na wafanyabiashara mbali mbali wakiigeuza siku hiyo kuwa ya biashara zaidi kwa kufanya kila kitu maalumu kwa siku ya wapendanao kionekane kiwe chekundu kuanzia kadi za salamu, maua, mpaka nguo wavaazo wapendanao kuonyesha ishara ya upendo.

Rangi nyekundu hutafsiriwa na wengi kama ishara ya upendo japo kuwa kwa wakati mwingine rangi hiyo huashiria hatari.

Kuna watu wengi pia ambao hawasherehekei siku hii kwa kuhoji umuhimu wa kuonyesha kumjali umpendaye katika siku moja tu ya mwaka badala ya
siku zote 365.

Mbali na hayo siku hii katika misingi ya dini hususani katika kanisa katoliki inalenga kuwafundisha watu kuwa na moyo wa mapendo na kutokukata tama.

Padre mmoja wa kanisa katoliki ,Deus Mulokozi anaizungumzia siku hii
kama ni maalumu kwa wakristo kujifunza kuwa na moyo wa kutokata tamaa
ikiwa ni pamoja na kuwahurumia waliokatishwa tamaa na mambo ya kidunia.

Padre Mulokozi anasisitiza na kuwakumbusha wakristo  kuitumia siku hii
kwa kujumuika na watu wenye kukosa mahitaji muhimu au faraja kama
watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu,Wagonjwa hata wazee .

"Maana si lazima utoe pesa,lakini ushiriki wako kwa chakula au mavazi
unaweza kuwapatia furaha ,Siku ya wapendanao ni sikukuu ambayo huadhimishwa ifikapo Februari 14
kila mwaka historia yake imeanzia karne ya tatu nchini Italia, japo Kuna
watu wanaigeuza siku hii kwa kufanya ngono/uzinzi, wakifikiri kwamba
ndiyo maana ya siku hii ya Valentine Day, kitu ambacho si
kweli"anasisitiza.

 Mbali na hayo Padre huyo anasisitiza usahihi wa siku ya wapendanao kuwa ni kwamba,  imelenga kuhamasisha watu kupendana,

ndiyo kusema kwamba unaweza kuonyesha upendo kwa mtu yeyote, si lazima
awe mwenza wako”amesema Mulokozi.

Mwandishi wa makala haya ,alijariku kukusanya maoni ya watu tofauti
kuhusiana na siku hii ya wapendanao ambapo baadhi ya watu wanaoihusudu
siku hii huku wakiwa tayari wamejipanga katika kuiadhimisha waliweza
kuzungumzia siku hii.

Devotha Methuselah,anasema"Kwa bahati nzuri Mwaka huu siku hii imeangukia Jumapili,ambapo kwa sisi wakatoliki ni ibada kubwa,Siku hii huwa ni maalumu sana kwani

hutukumbusha kuwajali wengine bila kujali itikadi za siasa ama dini,lakini tunapaswa kuwamakini na watu wanaopotosha mioyo yetu kwa mwamvuli wa upendo,"anafafanua.

 Haikael Zubery  anasema kuwa maadhimisho ya siku hii yalipoanza, ilionekana kama ni ya kidini zaidi, lakini baadaye ilipochunguzwa mantiki ya uadhimishaji wenyewe, ikaonekana kuwa na maana kwa watu wa madhehebu yote.

“Kwa jinsi ninavyofahamu mtu aliyetangaza rasmi kuadhimisha siku hii ya wapendanao ni Papa Gelasius, ambapo alisema ikumbukwe kama ishara ya kumuenzi mtetezi wa ndoa, Mtakatifu Valentino”amesema.

Hata hivyo penye wengi misimamo lazima hutofautiana,Jesse Mangala  alithubutu kusema kuwa siku hii ni maalumu kwa wazinzi kwa kuwa inapofika siku hii watu wengi huacha shughuli zao na kuanza kutumiana zawadi na wapenzi wao badala ya kufanya ibada.

“Siku hii haina umuhimu wowote,kwanza ingepigwa marufuku hapa nchini kwa kuwa katika kipindi cha kuazimisha siku hii ndoa nyingi huvunjika na hata mahudhurio na ongezeko la watu katika nyumba za kulala wageni huwa mara dufu hii inamaanisha kwamba uzinzi huchua nafasi kubwa,” amesema.

Naye Salmin Ahmed anaizungumzia siku hii kwa kusema kuwa japo kuwa imekaa kiimani haina haja ya kuipuiza kwani mlengo wake umejengeka zaidi Katika mambo yanayofaa.

 "Wengi huibeza siku hii na kuhisi Kuwa haiwafai,niwakumbushe tu kuwa sisi wote tumekuwa na mashirikiano Katika jamii na hivyo ili kuendana na maagizo ya Mwenyezi Mungu Ya kutenda mema siku zote

tunapaswa kuienzi siku hii kwa nia moja ya mapendo na sio uzinzi,"anasema Ahmed .

Hata hivyo anasisitiza kuwa kupeana zawadi mbalimbali sio dhambi,lakini jamii inapaswa kufahamu zawadi
hizo zinatolewa kwa maana ipi.

"Kuna watu huthubutu kuibadili maana ya siku hii kwa Kubadilishana maneno ya mapenzi na matamanio katika kadi wanazopelekeana, yakiwa katika mfumo wa kimashairi, tenzi na sentensi fupi fupi,Wakati mwingine  sherehe hii huambatana na kuchanganyika wanaume na wanawake, kuimba, na kucheza dansi mpaka kupelekea kulewa na kushawishika kufanya mambo yasiyo faa katika jamii,"anasema na kuongeza,;

"Hivyo basi,tunapaswa tutambue kuwa tunatakiwa kuwa makini kwa kuangalia na kuyafanya yanayofaa ikiwa ni pamoja na kufuata  kauli zile zilizo njema,imefikia wakati lazima ufikirie kufanya jambo kubwa, maalumu ambalo si tu halitasahaulika bali litatengeneza kitu kikubwa katika historia ya
maisha yako kwa kutenda yaliyomema,"anasema.

Licha ya hayo inawezekana umeumiza kichwa  ukijaribu kufikiria kitu cha kufanya kwa ajili ya kuwapendeza rafiki na jamaa zako, lakini uwezo wako wa kufikiri umefika mwisho na hujapata cha kufanya.

Hebu jaribu kuwaonesha kuwajali wanapokua na matatizo mbalimbali Kama vile ugonjwa ,upweke na mengineyo na hapo utakua unewapa maana halisi ya upendo kwa vitendo.

 Nakutakia sikukuu njema ya wapendanao,ni mimi Valentine wako!!.

 Mwisho.

 

Post a Comment

0 Comments