KAMPUNI INAYOCHINJA PUNDA YAPEWA MAELEKEZO RASMI.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

        Mji wa Serikali Mtumba,

        Mtaa wa Ulinzi,

        S.L.P  2870,

        DODOMA.

 

 

 

Telegram: “MIFUGO”

Simu: 262322613

Nukushi: 0262322613

Barua pepe: ps@mifugo.go.tz

Tovuti: www.mifugouvuvi.go.tz

 

 

 

 

 

 

 

 

 


Unapojibu tafadhali taja:

 

TAARIFA KWA UMMA

 

UCHINJAJI WA PUNDA KIWANDA CHA SHINYANGA

 

Dodoma, Februari 3, 2021

 

1.   Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaujulisha Umma kuwa Kampuni ya Fang Hua Investment iliyopo Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, Mwezi Septemba 2020, ilifutiwa leseni yake na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZA) baada ya kukiuka masharti ya leseni kulingana na Sheria ya Export Processing Zones (EPZA); Sura ya 373 ya mwaka 2012.  

2.   Kwa kuwa Kampuni hii iliwekeza kwenye biashara ya Uchinjaji Punda kupitia uhalali wao wa kusimamiwa na sheria ya EPZA, baada ya kupoteza sifa za kuwa chini ya masharti ya EPZA, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilibidi nayo iondoe uhalali wa leseni zake kwa Kampuni ya Fang Hua Investment.

3.   Kampuni ya Fang Hua Investment inafahamu kuwa baada ya kukosa Uhalali wa EPZA ili waweze kupata leseni upya ya uchinjaji ni muhimu kwao kujisajili kwa mfumo mwingine wa Kituo cha Uwekezaji (TIC). Hata hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi baada ya kuona kuwa Kampuni hii haijafanya hivyo ilichukua jukumu la kuwaandikia na kuwakumbusha kuwa njia mbadala ni kujisajili Tanzania TIC ili maombi yao mapya ya leseni ya Uchinjaji wa Punda yaweze kushughulikiwa na Wizara.

4.   Hadi sasa, kampuni hii haijatekeleza ushauri huo wa kujisajili TIC na kuwasilisha maombi mapya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya leseni za uchinjaji wa Punda na uhifadhi wa Ngozi za Punda.

 

Kwa siku za hivi karibuni, yamejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau wakionyesha hisia zao kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi inakwamisha leseni za Kampuni hii kuhusu Uchinjaji. Ni vyema Umma ukafahamu kuwa hoja hii sio ya ukweli na kwamba Kampuni yenyewe ndiyo haijaona haja ya kutekeleza ushauri walipoewa.

 

Msimamo, Maamuzi na Maelekezo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi

 

(i)     Kampuni ya Fang Hua Investment, kama bado wanapenda kuendelea kufanya biashara ya Kuchinja Punda wapate Cheti cha Uwekezaji kutoka TIC kisha walete maombi ya leseni na yatashughulikiwa haraka.

(ii)  Kampuni ya Fang Hua, iwe inaeleza ukweli huu kwa wadau wake.

(iii) Wafanyabiashara wa Punda waelewe ukweli huu na watafakari namna ya kuendelea kujihusisha na biashara hiyo na Kampuni ya Fang Hua.

(iv)  Wizara haikupenda kueleza mambo ya Kampuni hadharani ila imelazimika kufanya hivi baada ya kuona kuna upotoshaji kuhusiana na jambo hili hivyo kusababisha taharuki kwa wafanyabiashara wa Punda.

 

Imetolewa na:-                          (SIGNED)

Rehema Mbulalina

MKUU WA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI


Post a Comment

0 Comments