📌JOYCE KASIKI.
MKURUGENZI wa Shirika linaloangazia malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (CiC) Creig Ferla amesema,anajivunia mafanikio ambayo yameanza kupatikana katika madarasa ya elimu ya awali katika shule za msingi wilaya za Kongwa na Chamwino mkoani Dodoma kupitia mradi wake wa Watoto Wetu Tunu Yetu unaotekelezwa katika wilaya hizo mkoani Dodoma.
Akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu Mkurugenzi huyo amesema,katika mradi huo ambao umelenga kuboresha madarasa ya elimu ya awali na mazingira yake kwa ujumla,zaidi ya shule 178 zimeanza kuboresha mazingira ya elimu ya awali katika wilaya hizo mapema kuliko ilivyokuwa imepangwa.
Amesema,mwaka jana Shirika hilo lililotoa mafunzo kwa shule 58 tu kwa awamu ya kwanza lakini cha kushangaza shule ambazo hazijapata mafunzo nazo zimeanza kuboresha mazingira ya kufundishia na ujifunzaji wa wanafunzi wa darasa la awali.
"Maboresho ya elimu ya awali kwa wilaya za Kongwa na Chamwino yalifanyika kwa shule 58 kwa awamu ya kwanza na baada ya hapo tulitarajia awamu ya pili sasa kuhawilisha yale mafunzo kwenye shule zote zilizobaki yangefika kuanzia mwaka huu,
" Sasa tukashangaa kuona kwamba pamoja na kwamba wale walimu ambao tulikuwa tumewapa haya mafunzo walikuwa wameboresha mazingira ya awali kwenye shule zao na tukakuta hata shule ambazo hazikushiriki mafunzo zilikuwa zimeanza kuboresha mazingira ya elimu ya awali kwenye shule zao kutokana na elimu waliyoipata kutoka kwa waratibu elimu kata,walimu wakuu wa shule,maafisa Elimu Kata na walimu wa madarasa ya awali waliopata mafunzo kwenye awamu ya kwanza."amesema Ferla
Amesema hiyo ni ishara kwamba mwitikio kwa upande wa Halmashauri ,Kata ,shule ,walimu na wazazi ,umekuwa mzuri kuliko matarajio yao ya awali.
"Maana kabla ya kuanza mradi tuliambiwa Dodoma kunaweza kukawa na changamoto kwa upande wa elimu na mapokeo ya elimu ya awali tofauti na maeneo mengine ,lakini kiukweli tumekuta mapokeo yamekuwa makubwa ,mwitikio mkubwa pia."amesema
Amesema matarajio yao uboreshaji huo wa elimu ya awali katika mkoa wa Dodoma unaweza kuwa chachu ya kuboresha elimu ya awali katika mikoa mingine na Taifa kwa ujumla kwa sababu macho yote ya Serikali yapo Dodoma .
"Kufuatia hali hiyo,tutaendelea kusisitiza ziara nyingi za viongozi wa Serikali akiwemo Kamishna wa Elimu ya Awali ,Katibu Mkuu wa Elimu kwenda kuona hayo madarasa ili waendelee kusimamia maendeleo lakini pia waone kuna kitu gani wanachoweza kujifunza ili kusaidia uhawilishaji kwenye mikoa mingine ,na ndio kitu ambacho mimi najivunia kwamba ile 'project' inaelekea kuzaa matunda ." amesisitiza Mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa
"Maana ushirikiano ni mkubwa kwa ngazi zote na tunaamini kwamba ile Dora ya kuchangia kwenye uboreshaji limu ya awali inawezekana kwa yale ambayo tumeyaona mapema huku Dodoma."
Mwezi Juni mwaka jana,CiC kupitia mradi wake wa Watoto Wetu Tunu Yetu,ilitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wakuu,waratibu elimu kata,maafisa Elimu Kata na walimu wa madarasa ya awali kwa wilaya za Kongwa na Chamwino ,mradi ambao kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika hilo umeanza kuonyesha matunda.
Pia mradi huo umetekelezwa katika mikoa ya Morogoro na Mwanza ambapo madarasa ya awali yameboreshwa na kuwekewekwa zana mbalimbali za kujifunzia lakini pia walimu wamepata ujuzi ukiwemo wa kulimudu darasa hata watoto wakiwa wengi darasani.
xxxx
0 Comments