📌MWANDISHI WETU.
Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) imefanikiwa kuwadhibiti makundi ya nzige yaliyovamia wilaya za Longido na Simanjiro kwa kuwaua kwa kutumia ndege maalum iliyonyunyizia kiuatilifu kwenye maeneo ya mapori walipovamia.
Kauli hiyo ya serikali
imetolewa leo (23.02.2021) katika kijiji cha Kimokouwa wilaya ya Longido wakati
Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliopotembelea kukagua maeneo ambayo
yalikuwa makazi ya nzige wa jangwani mara baada ya kazi ya upulizaji sumu
uliofanywa na ndege maalum.
“Leo tumefanikiwa kuua
makundi makubwa ya nzige wa jangwani kwenye wilaya za Simanjiro na Longido
ambapo ndege maalum imefanya kazi hiyo asubuhi na hapa tunashuhudia tayari
nzige wameanza kufa na hakuna nzige aliyepo angani hadi muda huu (saa 6 mchana)
ninapozungumza nanyi waandishi wa habari hapa Longido” alisema Bashe.
Bashe alibainisha kuwa
serikali mara baada ya kupata taarifa toka kwa wananchi kuwa eneo la wilaya ya Mwanga
hapo mwezi Januari waliona nzige ilituma
wataalam wa udhibiti wa visumbufu vya mimea toka TPRI kufuatilia nyendo zao na
pia tarehe 16 Februari nzige wa jangwani waliingia Longido kupitia mpaka wa
Namanga wakitokea Kenya hatua za mapema zilichukuliwa ili wasilete madhara.
Aliongeza kusema hadi
nzige hawa wanaangamizwa leo hakuna eneo la kilimo ambalo mazao yake
yameathirika na wadudu hao kutokana na hatua ambazo serikali kupitia wataalam
wa wizara ya Kilimo imechukua.
“Hakuna eneo la kilimo
ambalo limeathiriwa na nzige wa jangwani tangu waliporipotiwa kuingia nchini
kwetu, hivyo wakulima na pia wafugaji wasiwe na hofu serikali ya awamu ya tano
ipo madhubuti kuwakabiri ili nchi yetu iendelee kuwa na uhakika wa chakula”
alisisitiza Naibu Waziri Bashe.
Katika hatua nyingine
Bashe alitembelea na kujionea eneo la kilometa 39 za kijiji cha Kimokouwa wilaya
ya Longido ambalo lilikuwa makazi ya nzige na kushuhudia makundi ya nzige
yakiwa wamekufa na hakuna nzige aliyepo angani
hatua inayoonesha ufanisi wa zoezi la kupulizia sumu.
Bashe aliagiza kuwa
wataalam wa wizara kwa ushirikiano na mikoa yenye uvamizi wa nzige wataendelea
kuwepo kwenye maeno yote ambayo nzige wamepuliziwa dawa kufanya ufuatiliaji wa karibu
ili kusitokee nzige wengine wakaendelea kusambaa.
“Waziri wa Kilimo Prof.
Adolf Mkenda ameagiza niendelee kubaki kwenye mikoa hii yenye uvamizi wa nzige
kufuatilia kwa karibu hivyo kwa wataalam wote wanaohusika nanyi pia mtaendelea
kubaki kwenye maeneo haya hadi serikali ijiridhishe na kutokuwepo kwa masalia
ya nzige.” Alisema Bashe.
Kwa upande wake Mkuu wa
Kitengo cha Teknolojia za Unyunyiziaji na Udhibiti wa Visumbufu TPRI Mhandisi
Julius Mkenda alisema ndege maalum imenyunyiza kiuatilifu(sumu) aina ya
Fenitrothion 96% ULV chenye uwezo mkubwa kuua nzige wa jangwani ambapo eneo la
hekta 412 za wilaya ya Longido ambako yalikuwa makazi ya nzige hao limefanikiwa
kunyunyiziwa sumu hiyo.
“Tathmini ya awali leo
asubuhi tumefanikiwa kunyunyiza sumu kwenye maeneo haya ya Kimokouwa na
Ildoinyo kata ya Sinya wilaya ya Longido ambapo makundi ya nzige yalikuwa
yamelala kisha ndege imefanikiwa pia kupuliza kiuatilifu maeneo ya Simanjiro na
kazi imefanyika salama.” Alisema Mhandisi Mkenda
Mkenda aliongeza kusema
kiuatilifu hicho kinafanya kazi kwa masaa kati ya 24 na 48 kuua nzige wote na
kwa kuwa nzige hawa walikuwa bado wachanga kazi ya kuwaua itakauwa rahisi hivyo
wataendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu kuona ufanisi wa zoezi hilo.
“Nzige hawa walikuwa bado
wachanga hali inayosaidia kusiwe na hofu ya uwepo wa masalia baada ya kazi ya
kuwapulizia leo. Tutaendelea kufuatilia maeneo yote walikopita kwenye vijiji
kujua ufanisi wa kazi ya kuwadhibiti nzige “ alisema Mhandisi Mkenda.
Kwa upande wake Mratibu
wa Masuala ya Visumbufu vya Mimea kutoka
Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) Tanzania aliyeshiriki zoezi hilo Mushobozi Baitani alisema shirika hilo
kazi yake ni kuhakikisha nchi wanachama zinakuwa na uhakika wa chakula kwa
kudhibiti visumbufu vya mimea na mazao ndio maana wameshirikiana na serikali
kutafuta ndege maalum
Mushobozi aliongeza
kusema baada ya uwepo wa taarifa za nzige kuingia Tanzania kutokea mpaka wa
Kenya walianza jitihada za kutafuta viuatilifu na ndege ili kufanya kazi ya kudhibiti
wasiongezeke na kufika mashambani .
“FAO muda wote
tunashirikiana na serikali ya Tanzania kudhibiti majanga yanayohusu chakula na
kilimo hivyo tatizo la nzige tumelikabili kwa pamoja ili uwepo uhakika wa
chakula kwa wananchi wote” alisema
Mushobozi
Mushobozi aliongeza
kusema makundi makubwa ya nzige yapo kwenye nchi za Somalia, Kenya na Ethiopia ambapo kazi kya kuwadhiti
inaendelea na kuwa ndege maalum iliyokuja Tanzania ikimaliza itarejea Kenya
kwenda kufanya kazi ya kudhibiti mazalia ya nzige yasiweze kuenea kwenye nchi
zingine inazopakana nazo.
Naye Mwenyekiti wa CCM
wilaya ya Longido Joseph Ole Sadira
akiongea kwa niaba ya wakulima alisema wanaishukuru serikali kwa kuchukua hatua
za haraka kuleta ndege kudhibiti nzige waliokuwa wameanza kuongezeka kwenye
maeneo ya wakulima na malisho ya wafugaji.
‘Tunaimani na serikali
yetu kwa hatua za haraka ilizochukua kuwaua nzige hawa ambao wangeachwa
wangeleta madhara kwa mazao ya kilimo na malisho ya mifugo yetu kwa kuwa
Longido eneo kubwa ni la wafugaji hivyo tungekiosa nyasi” alisema Ole Sadira.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Longido Jumaa Mhina alirejea agizo
lake la kufungwa kwa shule za msingi na sekondari kwa siku 5 kwenye maeneo yote
ambapo sumu imepuliziwa kuua nzige na kuwa watendaji wa vijiji na kata
waendelee kutoa matangazo ili wananchi wachukue tahadhali.
Mwisho
Imeandaliwa na K
Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Kilimo
LONGIDO
23.02.2021
0 Comments