MCHANGO WA MAJI KATIKA KUPAMBANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO



 ðŸ“ŒSALOME MLAY

UPATIKANAJI na uboreshwaji wa huduma ya maji safi na salama ya kunywa na usafi wa mazingira imebainikwa kuwa ndio msingi mkuu wa kulinda afya ya jamii.

Upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na usafi wa mazingira ni muhimu katika kulinda afya za wananchi. Utumiaji wa maji ambayo sio salama na uhaba wa maji huchangia katika kusababisha milipuko na kuenea kwa magonjwa kama kuhara na kipindupindu.

Zaidi ya watu milioni 579  ulimwenguni kote wanakunywa maji ambayo si salama kutoka kwenye visima vya kuchimba kwa  mikono, mabwawa, mabwawa, mito, na chemchemi. Maji machafu husababisha magonjwa milipuko na hata kifo,hususani kwa watoto chini ya miaka mitano.

Idadi hii ni kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani katika ripoti yake ya mwaka 2015,ambapo  (81%) ya watu  wanaokunywa maji ambayo si salama na kuishi katika maeneo ya vijijini pamoja na kwenye makazi holela (slums &informal settlement) ambayo bado hayajafikiwa na huduma za uhakika za maji safi.

Kwa mujibu wa Shirika la afya Ulimwengu (WHO), watu milioni 262 wanakunywa kile kilichoainishwa kama maji salama, na wanasafiri/tembea zaidi ya dakika 30 kwenda kuyapata maji hayo. WHO inasema ufikiaji huu  mdogo (limited access)mara nyingi huzuia maendeleo ya jamii nyingi dunia.

WHO inasema kunywa maji yasiyo salama kunawafanya watu waugue magonjwa ambayo huwagharimu pesa nyingi kwa ajili ya matibabu,na pia wanatumia muda mwingi kujiuguza badala ya kufanya kazi za kuwaingizia kipato.

Lengo namba 7 katika malengo 8 ya Milenia inataka mataifa ya dunia kukusanya nguvu kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama sio tu kwa vile maji ni uhai bali uwepo wa maji safi na salama uhepusha jamii na magonjwa ya milipuko.

HAKI YA KUPATA MAJI

Haki ya binadamu ya maji inampa kila mtu maji ya kutosha, salama, yanayokubalika, kupatikana kwa ukaribu na kwa bei nafuu kwa matumizi ya  mtu binafsi ya nyumbani 

Maoni ya Jumla: Namba 15 (2002): Haki ya Kupata Maji.

Katika mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliotokea mwaka 2015 katika jiji la Dar es Salaam, maeneo mengi yanayopata huduma kidogo au kutofikiwa kabisa na maji ya Shirika la Usambazaji Maji Dar es Salaam, (Dawasco) ndiyo yaliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kipindupindu.

Maeneo ya Buguruni, Kigogo na Yombo ambayo hutegemea zaidi maji ya visima virefu kama mbadala wa huduma za DAWASCO, lakini visima hivyo havina maji salama.

Hili linathibitishwa na kauli ya aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagilia, Mhandisi Gerson Lwenge wakati wa bunge la bajeti 2016/2017 alipoelezea kuhusu uchunguzi wa visima 108 ambapo visima 66 vilikuwa sio salama na maji yake yalikuwa na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu.

Imebainika kuwa hali ya uhaba wa maji safi na Salama na ukosefu wa miundombinu ya kutosha ya maji taka kwa baadhi ya maeneo mengi nchini  kunaweza kusababisha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa watu kutumia maji yasiyo safi na Salama.

Ukosefu au huduma hafifu za maji safi na salama huwalazimisha wakazi wa meneo ya husika kutumia kutumia maji machafu yanayotokana na mvua au vyanzo vingine visvyo  salama kwa kunywa, kuandaa vyakula au vinywaji, kusafisha meno, kuosha uso,kunawa mikono,kuosha vyombo na kuosha matunda.

Takwimu za Wizara ya Maji nchini zinaonyesha kuwa wastani wa idadi ya watu wanaopata huduma ya maji ya safi na salama vijijini imeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.1 mwezi Machi mwaka 2020.

Kwa upande wa mijini, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2020 kitu ambacho wasimamizi wa masuala ya afya wanasema kimepunguza kasi ya magonjwa ya milipuko.

Hali hii inaweza punguza uwezekano wa jamii kupata magonjwa ya mlipuko ya mara kwa mara kama ilivyo kwa mkoa wa Dodoma ambako upatikanaji wa maji umechangia kutokomezwa kwa magonjwa mbalimbali ya milipuko ikiwemo ugonjwa wa macho ‘trachoma’ pamoja na kipindupindu.

Tafiti zinaonesha upatikanaji wa maji safi katika maeneo ya Kongwa na wilaya nyingine za mkoa wa Dodoma kumechangia kupunguza visa vya magonjwa ya macho.

Ugonjwa wa macho kama trachoma unaweza kudhibitiwa kwa unawaji wa uso kwa maji safi,bakteria wanaosambaza ugonjwa huu wanapenda kukaa kwenye uchafu kama uso haujaoshwa utakuwa ni makazi ya bakteria wa ugonjwa huo

Dkt. Rajabu Kisonga daktari wa magonjwa ya macho hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba ukosefu wa maji katika wilaya za Chamwino,Kongwa na hata Dodoma mjini ulichangia baadhi ya watu hususani watoto kushindwa kunawa nyuso zao hivyo kuwa rahisi kwa Inzi wanaoambukiza ugonjwa huo kutua katika nyuso zao.

Upatikanaji wa  maji safi ya kunywa na matumizi mengine ya binadamu ni huyaweka jamii katika mazingira ya usafi na kukabiliana na magonjwa mbalimbali ambayo hutokei lakini chanzo kikuu ni usafi aidha wa mtu au mazingira yake kama vile vyoo.

MAJI NA MAGOJNWA YA KUHARA

Kwa mujibu wa WHO Watu milioni 1.8 hufa kila mwaka kutokana na magonjwa ya kuhara (ikiwemo  kipindupindu); na kati yao 90% ni watoto chini ya miaka 5.

Vifo hivyo hutokea zaidi katika nchi zinazoendelea ambako  88% ya ugonjwa wa kuhara huhusishwa na usambazaji wa maji salama, usafi wa mazingira


Uboreshaji wa maji hupunguza magonjwa ya kuhara kati ya 6% hadi 25%,
hivyo Maji salama ya kunywa pia  ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto mwenye afya. Inamaanisha watoto hawatapata magonjwa ya miipuko yanayosababishwa na maji kama vile typhoid na kipindupindu.

Kwa mujibu wa WHO ugonjwa wa kuhara ni moja ya sababu kuu tatu za vifo vya watoto na hii mara nyingi husababishwa kutokana na kunywa maji machafu,na tawkimu zinaonesha kwamba kila dakika 2 mtoto mmoja hufa kutokana na ugonjwa unaosababishwa maji yasiyo salama.

Ukosefu wa upatikanaji wa maji salama pia huathiri ustawi/afya ya mwili wa wanawake na watoto wadogo hususani wale wa kike ambao hawana njia mbadala isipokuwa  kwenda umbali mrefu nan doo zao kichwani kwenda kutafuta maji kwa ajili ya familia zao.

MAJI NA COVID-19

Katika wakati huu ambao dunia inakabiriwa na janga la COVID-19, upatikanaji wa maji unabaki kuwa jambo muhimu zaidi kuthibiti kuenea kwa ugonjwa huo,maji yanahitajika kwa wingi ili watu waweze kufuata ushauri wa wataalam wa afya wa kunawa mikono kila mara.

Kwa kiasi kikubwa maji tiririka huitajika ili kuweza kuzuiza maambukizi ya virusi vya korona kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Hivyo basi,mamlaka za maji za miji na mikoa zina jukumu kubwa kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama unawafikia wakazi wa maeneo husika ili kupunguza kasi ya magonjwa ya milipuko katika maeneo hayo.

 

Post a Comment

0 Comments