Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
akimuonya mhasibu wa mnada wa upili wa Mhunze uliopo Wilaya ya Kishapu Mkoani
Shinyanga Bw. Athanas Msiba kwa tuhuma za kutokuwa mwaminifu. (Picha na Edward Kondela )
📌EDWARD KONDELA ( Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
WAZIRI wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amepiga marufuku halmashauri zote nchini kutotumia
wafanyabiashara kuchanja mifugo na kutaka kuvunjwa kwa mikataba hiyo mara moja.
Waziri Ndaki
amebainisha hayo alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja
Mkoani Shinyanga ambapo alipokuwa katika josho la kuogeshea mifugo la Kijiji
cha Mipa kilichopo Wilaya ya Kishapu mkoani humo kwa ajili ya kushuhudia
uogeshaji mifugo na utoaji wa chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, wafugaji
wamemlalamikia kuwa baadhi ya ng’ombe kijijini hapo wamekuwa wakivimba na
wengine kufa baada ya kupatiwa chanjo.
Waziri Ndaki akiwa
ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amesema
kuanzia sasa chanjo zote nchini zitatolewa na wataalamu wa wizara ambao
wamethibitishwa na kugoma kushuhudia zoezi la uchanjaji lililokuwa limeandaliwa
baada ya kukasirishwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kutokuwa
na takwimu yoyote ya idadi ya ng’ombe waliovimba na wengine kufa baada ya
kuchanjwa.
Halmashauri zetu zote kuanzia sasa hivi ni marufuku kutumia wafanyabiashara kuchanja mifugo yetu, halmashauri zitumie wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa waweze kuchanja mifugo ya wananchi wetu.
Mashimba Ndaki
Mh.Ndaki
ameongeza kuwa kama halmashauri hizo zimeingia mikataba na wafanyabiashara hao
ivunjeni haraka iwezekanavyo ikiwa ngg’ombe wanazozichanja zinavimba na
nyingine zinakufa.
Aidha, Waziri Ndaki katika ziara yake ya siku
moja Mkoani Shinyanga amefika katika mnada wa upili wa Mhunze ambao ni moja ya
minada inayosimamiwa na wizara na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Kishapu kumuondoa mara moja kazini mhasibu wa halmashauri hiyo anayefanya
kazi katika mnada huo Bw. Athanas Msiba kwa tuhuma za kutokuwa mwaminifu katika
kuandika idadi ya mifugo inayoingia na kutoka katika mnada huo hali
inayosababisha wizara na halmashauri kukosa mapato stahiki.
Mkurugenzi huyu Athanas Msiba siyo mwaminifu hafai kukaa hapa tena aondoke sasa hivi ulete mtu mwingine, watu wakipita hapa na mbuzi watano anaandika watatu anaandika kidogo hafai aondoke hapa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
akiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul na baadhi ya viongozi kutoka wizarani
na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, alipokuwa akikagua
miundombinu ya mnada wa upili wa Mhunze
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bw. Emmanuel Johnson amesema
amepokea maelekezo hayo na atayafanyia kazi kwa kuihusisha pia Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ili ifanye ufuatiliaji kwa kuwa
serikali haiko tayari kuwa na watu wenye tabia ya namna hiyo.
Akiwa katika mnada huo
Waziri Ndaki amepata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa
wafanyabiashara na wafugaji ikiwemo ya kuzuiwa kuondoa mifugo mnadani kabla ya
saa 12 jioni hali inayohatarisha maisha yao kutokana na uwepo wa fisi wengi
kwenye maeneo ya mashamba wakati wa kurudi nyumbani majira ya jioni hali
iliyomlazimu Waziri Ndaki kuutaka uongozi wa mnada utafute utaratibu wa
kuwaruhusu wafanyabiashara kuondoka kabla ya muda huo wakiwa wamemaliza
shughuli zao.
Mtu amemaliza biashara yake mkagueni vizuri kwenye mlango wa kutokea aende zake akimaliza hapa akikaa saa mbili aondoke, akikaa dakika 15 aondoke ili mradi amemaliza shughuli zake siyo unawaleta unawafungia humu haka kamekuwa kajela kadogo? Hapana hiyo!.
Akiwa Mkoani Shinyanga
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri Mhe. Pauline
Gekul, ametembelea ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa yaliyopo katika
Manispaa ya Shinyanga unaogharimu Shilingi Bilioni 5.5 ambapo tayari zimelipwa
Shilingi Bilioni 5.1 na umefikia asilimia 97 hadi kukamilika kwake.
Ujenzi wa machinjio
hayo unatarajiwa kukamilika mwezi Februari Mwaka 2021, yatakuwa na uwezo wa
kuchinja ng’ombe 500 mbuzi na kondoo 1,000 kwa siku.
0 Comments