WATAALAMU wa lugha ya Kiswahili nchini
wameiomba Serikali nguvu katika Taasisi zinazofundisha lugha hiyo kwa
wageni kama hatua ya kuendelea kukuza Kiswahili kimataifa pamoja na kuboresha
sera zitakafungua mwanya wa wageni kuja kwa wingi nchini.
Akizungumza na mtandao huu Mmiliki wa
Kituo cha kufundisha Kiswahili kwa wageni (LILINGA SWAHILI SCHOOL),Tunku Kyoba
alisema kiswahili ni bidhaa inayohitajika kwa kiasi kikubwa katika mataifa ya
nje hivyo ipo haja ya kuweka jitihada madhubuti kufanikisha hilo.
Alisema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa raia wa
kigeni kuja nchini kwa lengo la kusoma lugha ya Kiswahili ambapo mataifa
ya Marekani , Ujerumani na Uingereza yameonyesha uhitaji wa kufahamu lugha hiyo
kwani hulazimika kuitumia katika utekeleza ma majukumu yao ndani nan je ya
nchi.
“Wenzetu wametengeneza fursa kufanya kazi hapa
kwetu na sera za Mashirika yao zinawataka kufahamu kwa kiswahili na utamaduni
na wamekuwa wakija kwa wingi kujifunza tunaomba Serikali kuona namna inavyoweza
kuboresha mazingira ya ufundishaji wa Kiswahili kwa ufasaha katika vituo vya
Kiswahili na utamaduni tukidhi mahitaji yao kuongeza thamani ya lugha
yetu,”alisema Kyoba.
Kyoba alisema changamoto wanazokabiliwa nazo
kwa sasa ni uwepo wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi
vya Corona kwa baadhi ya mataifa ya nje hivyo kusababisha kupungua kwa
wanafunzi na mabadiliko ya sera ya Nchi kuhusu wageni katika nyanja ya
utolewaji wa vibali vya makazi na kikazi.
Kwa upande wake Profesa Mshiriki katika
taaluma za Kiswahili Aldin Mutembei aliwataka watanzania kubadilika kifikra kwa
kutodharau lugha yao wakiamini kuzungumza lugha za kigeni ndiyo kuelimika
huku akiwahimiza wazazi na walezi kuwajenga watoto wao kuthamni lugha na
utamaduni wa Taifa lao .
“Wengi wanaamini kuzungumza lugha ngeni ndiyo
kuwa na lakini ni zaidi ya lugha yenyewe na unajua shule zetu za siku
hizi mtoto yuko darasa la kwanza haongei Kiswahili na sisi hatupigi vita lugha
hizo tunasema ni lugha muhimu lakini tukumbuke sisi ni kisiwa hakuna nchi iliyounganisha
watu wake wakazungumza lugha moja tuwe watendaji katika hili,”alieleza
Prof.Mutembei.
Naye Mhadhiri wa Tafsiri na Taaluma za
Kiswahili kutoka Chuo Kikuu Huria, Dk.Hadija Jilala alieleza kwamba
endapo Serikali itapitisha lugha hiyo kutumika kama lugha ya kufundishia
kuanzia shule za masingi hadi vyuo vikuu itakuwa fursa ya kipekee katika
kukuza Kiswahili.
“Kutakuwa na mafanikio makubwa sana shida ni
kuhofia yajayo suala la ufundishaji na utafsiri vinaenda sambamba kwa sasa
tunatumia kiingereza kufundisha na unakuta mwalimu analazimika
kuchanganya na kiswwahili ili wanafunzi waelewe hii itakuwa fursa kwetu
watafsiri tuko tayari kutoa tafsiri ya vitabu vya kitaaluma zipo tafsiri nyingi
tumezifanya kwa marejeleo ya kiingereza hakuna kinachoshindikana,”alisema Dk.
Hadija.
Aidha akizungumzia ushirikishwaji wa
watu wenye ulemavu Oktavian Malaba ambaye ni mkalimani wa lugha ya alama
alisema Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) lina jukumu la kuendeleza na
kukuza lugha ya alama kama sehemu ya kutambua mchango wa watu wenye ulemavu
kueneza Kiswahili.
“Changamoto kuwa ni kukubalika na kutambuliwa
kwa ukalimani katika jamii tunasahau kuwa ni muihimu maana unaweza kukutana na
mtu huyu utawasiliana naye vipi ikiwa hujui lugha yake tuwajali maana ni watu
kama sisi wana uwezo wa kufanya makubwa kuliko hata wana viungo
kamili,”alieleza Mkalimani huyo.
0 Comments