WANANCHI WATUPA JICHO KWA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE.

 


📌Faustine Gimu Galafoni.

Ikiwa Juma hili  kamati za kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeanza kukutana jijini Dodoma tangu  Januari 18 hadi 31 ,2021 kutekeleza majukumu ya kibunge kabla ya mkutano wa pili wa Bunge la 12 uliopangwa kuanza  tarehe 2,Februari,2021 baadhi ya  wananchi  jijini Dodoma wametoa maoni mbalimbali juu ya Umuhimu wa Kamati hizo kwa Mstakabali mzima wa Maendeleo ya Taifa .

 Wakizungumza na Mtandao huu  baadhi ya wananchi hao walisema kuwa matarajio makubwa kwao kwa kamati hizo ni kuhakikisha zinakuwa mstari wa mbele katika kusimamia na kufuatilia miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo maji,elimu,biashara,Miundombinu na sekta ya afya kwani kupitia kamati za kudumu za bunge zina nguvu kubwa ya kusimamia na kuwajibisha Serikali pamoja na taasisi zake pindi inaposhindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi.

 Bi.Mwanaid Ally ni Mkazi wa Chinangali jijini Dodoma akifanya mahojiano maalum na mtandao huu alisema kuwa matarajio kwake  ni kuhakikisha kamati zinaenda vyema kusimamia na kuzihoji idara ama halmashauri ambazo zinashindwa kwendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli.

 "Wananchi kwa kweli tunapenda mambo mazuri  katika nyanja mbalimbali mfano miundombinu,barabara,elimu,Afya,Biashara kwa hiyo kwenye kamati hizo pamoja na vikao vya Bunge nina imani wao wakikaa  watafanya mambo makubwa na kufanya maboresho palipolegalega "alisema.

 Kwa upande wake, Robert Kasele Mfanyabiashara mdogo na mkazi wa jiji la Dodoma alisema kamati za kudumu za bunge zitakuwa na tija katika kuleta mabadiliko ya maendeleo  kwa  wananchi .


"Kamati zinaenda kuakisi  mambo mbalimbali kwa mstakabali wa maendeleo ya Taifa letu ,hivyo zitakuwa zenye tija na ari na mwisho wa siku zitaenda kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu"alibainisha.

Nini Ushauri kwa serikali juu ya suala zima la kodi? Kasele alifafanua.

"Kodi zetu ziangaliwe upya ,kodi nyingi zimekuwa zikizuia wafanyabiashara kufanya biashara na kuanza kukwepa na kukimbia biashara wengi sasa wameamua kuanzisha  mifumo mingine ya biashara kukwepa kodi tunajua tuna wataalam wa kiuchumi ambao wataangalia namna zaidi ya kuwavutia watu kufanya biashara badala  ya kukimbia biashara naamini serikali yetu ni sikivu na inalifanyia kazi "alisema.

 Nuru Nuha Hassan Mkazi wa Bonanza  jijini Dodoma alisema  kuwa matarajio yake kwa Kamati za kudumu za Bunge pamoja na vikao vya kawaida vya Bunge  ni kujenga ajenda nzuri katika kuitengeneza Tanzania huku George  Lugodi mkazi wa Chamwino jijini Dodoma akifafanua kuwa serikali ya sasa ni imara hivyo imani yake kwa kamati kupitia viongozi waliochaguliwa kuziongoza kamati hizo wanakuwa imara  kukagua miradi ya maendeleo.

https://blogger.googleusercontent.com/img/proxy/AVvXsEjUWRXL1vKMD-cVsNLhyUaRhma4dASvy5o1fxHkS-IAGfoKwfakQg3q495jqU0RbxlmpzvFwwi2GaP2SHI7NEhsSzJ_UlGM3ztDgYSROIJblo-PD31hU41Q_FUSg7qsNuXP9WhOw5tNJTAjKEATrspsB7N0O_L60XN3q2pL=s0-d-e1-ft

"Mimi cha kuwashauri viongozi wanaochaguliwa kuziongoza kamati hizo za kudumu za bunge ni kuwa imara kama Rais Magufuli alivyo imara"alisema  George Lugodi.

Naye  Abdul Abdallah Omari aliliambia gazeti la Sauti kuu alisema matarajio yake ni kuwa kamati za kudumu za bunge hususan kamati ya miundombinu inafuatilia  na kukagua vyema miundombinu ya barabara ili mamlaka za kisekta ziweze  kuondoa changamoto ya miundombinu katika barabara za mitaa.

 Pia, Omary alisema imani yake kubwa ni kuona kuwa sera ya kuwepo vioski vya kuuzia  maziwa katika kila shule itakelezwa kama ilivyotolewa mwaka jana na Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto  kipindi hicho Ummy Mwalimu ambaye sasa ni Waziri wa Muungano na Mazingira  ili kupunguza udumavu kwa watoto hivyo kamati ya afya pamoja na kamati ya mifugo bungeni zina nafasi kubwa ya kulisimamia suala hilo.

 Sanjari na hayo,baadhi ya wafanyabiashara  jijini Dodoma walisema pindi vikao vya Bunge vinapoanza hali ya biashara huchangamka.

Ikumbukwe kuwa ,katika taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge  mwanzoni mwa Juma hili ilifafanua kuwa shughuli za kamati za Bunge katika Majuma haya mawili  ni pamoja na uchaguzi wa wenyeviti  na makamu wenyeviti,mafunzo kuhusu majukumu na taratibu za uendeshaji wa kila kamati,mafunzo kuhusu bunge mtandao, mafunzo kuhusu Bunge mtandao,na usalama wa mtandao kwa kamati zote huku vikao vya Bunge vikitarajia kuanza  Tarehe 2.Februari,2021.

 Pia ,kamati za kisekta zinapokea maelezo ya wizara kuhusu muundo,majukumu ya taasisi pamoja na sera na sharia zinazosimamiwa na  wizara hizo.

Mafunzo mengine  ni kwa kamati ya Hesabu za Serikali [PAC],Kamati yaHesabu za Serikali za Mitaa[LAAC],Kamati ya Uwekezaji na Mitaji[PIC]na kamati ya Bajeti kuhusu uchambuzi wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali[CAG],Msajili wa Hazina[TR]na namna bora ya kuhoji maafisa Masuuli na mafunzo kwa Kamati ya sheria ndogo kuhusu uchambuzi wa sheria ndogo na uzoefu wa Mabunge mengine ya  nchizinazofuata mfumo wa kibunge wa jumuiya ya Madola.

Kuhusu  shughuli ya kamati ya Bajeti inapokea  na kujadili taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo ya taifa kwamiaka mitano ,2016/17-2020/2021,mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa  wa miaka mitano 2021/22-2025/26.

Aidha,kamati pia inapokea mapendekezo ya mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka mmoja 2021/2022,mwongozo wa kuandaa mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na kupokea taarifa yautekelezaji wa Bajeti ya Serikali pamoja na sharia ya fedha  kwa kipindi cha nusu mwaka ,kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

 

Post a Comment

0 Comments