📌DOTTO KWILASA.WALIMU wakuu wa shule
za msingi nchini wametakiwa kubainisha aina za ulemavu wa wanafunzi ili
kuirahisishia Serikali kuwasaidia watoto hao kulingana na aina ya ulemavu
walionao.
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi wa elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia
Dk.Magret Matonya wakati wa kufunga Mkutano wa Pili wa walimu wakuu wa shule za
msingi Tanzania Bara (TAPSHA).
Aidha mkutano huo wa
siku mbili uliowakutanisha walimu 314 ulikua na lengo la kuwaunganisha
walimu na kubadilishana uzoefu ikiwa ni pamoja na kujadili changamoto
mbalimbali za kielimu ili kuendelea kuinua kiwango Cha elimu Tanzania.
Akieleza zaidi
Dk.Matonya amesema,watoto wengi wenye mahitaji ya elimu Maalum hawapatiwi
huduma zao za msingi Kutokana na taarifa zao kutowekwa wazi kutokana na sababu
mbalimbali huku baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi wakiwa chanzo kikuu.
"Serikali yetu
haina ubaguzi,inahitaji kuwahudumia watoto wote lakini kwa bahati mbaya ninyi
walimu mnashindwa kuwasilisha taarifa zao,kuna wanafunzi wengine wana ulemavu
zaidi ya aina moja ya ulemavu hivyo taarifa zao pia zinapaswa
kuzingatiwa,"anasema.
Mkurugenzi huyo wa
elimu Maalum ameeleza kuwa ,jamii ya watanzania imezungukwa na watoto Wenye
aina nyingi za ulemavu ambazo Wakati mwingine sio rahisi kuzibaini hivyo
kuwataka walimu wakuu nchini kuwa makini wakati wa usajili.
"Tafadhali
niwaombe muwapokee watoto wote kisha wapelekwe kwenye hospitali za
Halmashauri ili kubainisha aina za ulemavu wa watoto na kuwapangia shule husika
kwa kuzingatia aina ya mtu na ulemavu alionao,"anasisitiza.
Mbali na hayo
,Dk.Matonya amebainisha Kuwa licha ya Serikali kuwapa kipaumbele watoto Wenye
mahitaji Maalum bado kuna walimu wakuuu wanakataa kuwasajili .
"Hatutamvumilia
mwalimu yeyote ambaye atakataa kumsajili mtoto mwenye ulemavu,nawakumbusha kuwa
kila mtoto anahitaji elimu bila kubaguliwa kwani sisi tunaamini watoto wte ni
sawa,”anasema na kuongeza;
“Kila mtoto anahitaji
mwalimu ambaye anaendeleza kwa vitendo ujumuishi katika elimu na ndio maana
Serikali inapanua uelewa wa Walimu kuhusu Ujumuishi ili kuwasaidia kikamilifu
wanafunzi waliotengwa kama vile walemavu wa kutosikia au wenye vilema
vingine,”alisema.
Kutokana na hayo,Naibu
waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga amesema kuwa Serikali ya
Jamhuri ya muungano wa Tanzania itaendelea kusimamia maboresho ya upatikanaji
wa elimu ya msingi kwa kuzingatia maadili ya haki za binadamu bila ubaguzi
ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu rafiki ya kufundishia.
Katika kufanikisha
hilo ,alieleza kuwa imefanya maboresho kwa shule za msingi kwa kusambaza vitabu
vya kiada na ziada kwa nchi nzima kwa kuzingatia uwiano wa kitabu kimoja kwa
wanafunzi wawili huku lengo likiwa ni kitabu kimoja kwa kila mwanafunzi.
Mbali na hilo,
Serikali katika kuhakikisha elimu inakua bora zaidi kwa kuzingatia usawa kwa
watoto wote ,imeongeza uchapaji na usambazaji wa vitabu kwa wanafunzi
wenye mahitaji ya elimu maalum kwa uwiano wa moja kwa moja nchi nzima.
Aidha ameeleza
kuwa ili kurahisisha upatikanaji na kupunguza gharama za uchapaji wa
vitabu vya kiada , zida na machapisho ya kielimu, tayari Wizara imepokea
mashine ya kubwa ya kisasa yenye thamani ya shilingi bilioni 6.9.
Hatua hiyo itaimarisha
upatikanaji wa vitabu kupitia huduma ya maktaba mtandao ambapo wanafunzi
wanapata vitabu hivyo moja kwa moja kwa njia ya mtandao lengo ni kumwezesha
mwanafunzi kujisomea na kuimarisha utamaduni wa kujisomea bila kusukumwa.
“Pamoja na jitihada
zote hizi ifahamike kuwa mafanikio katika elimu yanategemea sana mwalimu kwani
ana mchango mkubwa wa kuchangia katika ufaulu au kufeli kwa
mwananfunzi,”anasema
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Elimu,Sekondari kutoka OR-TAMISEMI ambao ndio waandaaji na
wasimamizi wakuu wa Mkutano huo wa TAPSHA Benjamini Oganga alieleza umuhimu wa
walimu kwa shule za msingi kuwa ndio nguzo ya mafanikio ya wanafunzi wa
Sekondari.
“Kila mwaka kwa miaka
mitano mfululizo darasa la saba wamekuwa na takwimu nzuri za ufaulu wa mitihani
yao ya mwisho ambapo kwa mwaka huu wanafunzi laki nane wanaingia kidato cha
kwanza kwa nchi nzima,”anasema.
Naye Mwenyekiti wa
TAPSHA Mwl.Rehema Ramole ameishukuru serikali kwa kuwajali walimu kwa kuwapatia
stahiki zao na kusema kuwa wana deni kubwa la kuhakikisha wanatekeleza misingi
ya elimu kwa watoto .
“Tukitoka hapa kazi
yetu ni moja kuwafikishia wenzetu tuliyojifunza kuleta mabadiliko chanya kwenye
elimu ya msingi,”anasema.
0 Comments