SERIKALI YAWATOA HOFU WAMILIKI WA MABASI NCHINI

 


📌DEVOTA SONGORWA.

SERIKALI imewatoa hofu wamiliki wa mabasi nchini kutokana na kutangaza mabadiliko ya mfumo wa kawaida wa kukata tiketi kuwa wa kielektroniki.


Hayo yalisemwa  jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri ardhini (LATRA), Gilliard Ngewe ambapo alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato ya Serikali.

Alisema uamuzi huyo utawezesha kukuza sekta ya uchukuzi na kuondoa usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza kwa abiria wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali kwani baadhi yao wamekuwa wakikatiwa tiketi isiyo halali.

"Tiketi ya kawaida ukikata pesa inapita katika mikono ya watu wengi kwa hiyo kiasi inachomfikia msafarishaji ni kidogo Sana unakutwa mwisho wa mwaka wanashindwa kulipa Kodi wanadiclare hasara,"alisema Mkurugenzi huyo.

Pia alieleza kwamba Serikali iko tayari kukaa pamoja na wamiliki kujadili  changamoto za ili kuhakikisha wanaboresha sekta hiyo muhimu akiwasisitiza kutotuma wawakilishi pindi wanapohitajika.

" Tujafanya uamuzi huu kuumiza yeyote tunalenga kusaidia kila upande kwa nafafsi yake tuone tija ya sekta hii Sasa unakuta tukiwaita wamiliki wanatuma wawakilishi Sasa kwa namna hii hatuwezi kufika tuanendelea kuwaeilimisha tumeshafanya mikoa mingi ikiwemo Arusha,Tanga,Dar es salaam tukagundua tatizo ni uelewa na uoga hawataki kuwa wazi,"alieleza Ngewe.

Kwa upande wake Mabkhet Omary kutoka kampuni ya Shabiby aliipongeza Serikali akisema mfumo huo utakuwa msaada mkubwa kwao Kama wamiliki kwani utadhibiti wapiga debe hali iliyokuwa ikisababisha kutopata mapato waliyokusudia.

"Kuna vitu sisi wamiliki tulikuwa tukikosa hasa ikisababisha na hawa wapiga debe wanapunguza Sana faida maana na yeye anategemea hapo kwahiyo katika huu mfumo tutapata kiasi Cha fedha kikichopangwa na niombe tu elimu itolewe,"alipongeza Omary.

Issa Swalehe Mrwata ambaye ni Mkurugenzi wa basi la Shukrani alieleza kwamba mfumo huo kwao ni changamoto kwani zipo baadhi ya huduma ambazo wamekuwa wakilipa kwa fedha taslimu na bado hawana elimu ya kutosha kuhusu mfumo wa tiketi mtandao.

"Sikatai huu mfumo ni mzuri lakini kwa baadhi yetu ni shida kama mimi sijui kusoma nikamua kuingia katika biashara hii unaweza kuondoka na abiria wachache tunapakia njiani Sasa wanasema tunaweza kutumia simu kukata tiketi na sikwenda shule kwakweli watuelimishe zaidi," alieleza Mrwata.

Akitoa maoni yake  Moses Julio ambaye ni mkazi wa Mpunguzi   akasema mfumo huo utapunguza usumbufu ambao wamekuwa wakiupata kituoni ikiwemo kudanganywa, kupewa tiketi feki na kung'ang'aniwa na mawakala wa mabasi ambapo wengine hupoteza mizigo yao .

Aidha Husna Juma mkazi wa Veyula  alisema hatua hiyo itawasaidia kuepuka gharama za kwenda kukata tiketi Kituo Cha mabasi kwani wengine hutoka mbali  akiomba Mamlaka kuona namna watakavyo wasaidia vijijini kufikiwa na elimu hiyo.

" Kwa mjini wenye elimu zao itawasaidia lakini siyo vijijini wawape elimu tutapunguza gharama za usafiri maana tunatofautiana uwezo nimefurahi sana  Sasa naweza kupata tiketi yangu nikiwa nyumbani,"aliomba Husna.

Ikumbukwe kuwa mfumo wa tiketi mtandao ulizinduliwa mwezi Mei mwaka jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kwa lengo la kuleta tija kwa Serikali,abiria,na wamiliki wa mabasi.

 

Post a Comment

0 Comments