📌BARNABA KISENGI.MKUU wa Mkoa wa Dodoma
Dokta Binilith Mahenge amemuelekeza Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda kutomlipa mkandarasi Musons
Engineering fedha hadi arekebishe ukuta alioujenga wa daraja la Chimaligo katika
mto chinyasungu ambao ukuta huo wa daraja hilo umepinda.
Dokta Mahenge ametoa
maelekezo hayo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma akiwa katika ziara yake ya kikazi
ya kukagua maeneo ya barabara yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha
wilayani hapo ambapo serikali imezitengea fedha na kuanza ukarabati ikiwemo
ujenzi wa madaraja.
Maeneo hayo ni
barabara ya Pandambili-Mlali-Mpwapwa hadi Nghambi ambapo ujenzi wa daraja la
Chimaligo ulipo pita mto Chinyasungwi na eneo la Iyoma ambapo zaidi ya Sh Bilioni
2.5 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo za ujenzi na ukarabati.
"Mkandarasi huyu
anatakiwa alipwe Sh Bilioni 1.109 lakini nikiangalia hapa naona kabisa ukuta
mmoja wa ukingo wa daraja umepinda lakini pia upana wa ukuta huo naona ni
mwembamba wakati eneo hili linapita maji mengi,nikuelekeze kaimu Meneja
usimlipe mkandarasi fedha hadi arekebishe hali hii tuliyoiona wote
hapa,"aliagiza Dkt Mahenge
Sambamba na hilo
amesisitiza uwepo wa usimamizi katika maeneo yote ambayo ujenzi unaendelea ili
makosa kama hayo na mengine yasiweze kujirudia tena katika ujenzi na ukarabati
wa maeneo yote
"Kama ukuta
unatakiwa kujengwa kwa centimeter 30 ukipunguza hata centimeter 2
unaongelea kupunguza saruji,mchanga na ukipiga hesabu unaona kabisa fedha
nyingi zinakuwa zimepotea,hivyo ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na usimamizi wa
karibu wakati wote wa ujenzi huo"alisisitiza Dkt Mahenge.
Mbali na maagizo hayo
amemuagiza mkurugenzi wa Bahati Investment anayejenga barabara kipande Cha
Iyoma kuongeza vitendea kazi na kufanya kazi usiku na mchana Ili mvua ikitokea
isiweze kuathiri kazi inayoendelea na hivyo kupelekea barabara hiyo
kutokupitika.
Awali Mkuu wa Wilaya
hiyo Jabir Shekimweri ameishukuru serikali kwa kupeleka fedha na kuwezesha
ujenzi katika maeneo hayo kuendelea kufanyika na hivyo kuboresha miundombinu
iliyopo wilayani hapo.
"Eneo hili la
daraja la Chimaligo ambapo umepitiwa na mto Chinyasungwi yanapita Maji mengi
mengine kutoka Mkoani Manyara na katika mvua iliyonyesha mwaka jana kuna
kitongoji kilikuwa kisiwa,familia 22 zilikwama huko ikabidi tutafute boti kwa
ajili ya kuwatoa,hivyo uwepo wa daraja hili utasaidia Sana kupunguza changamoto
hiyo,"alisema Shekimweri.
Amesisitiza suala la
kuimarishwa kwa usimamizi katika maeneo yote yanayoendelea na ujenzi ili kazi
inayofanyika iendane na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali ya awamu ya
tano
"Kila mmoja wetu
awe mzalendo,aumie kuona kazi inayotarajiwa inakamilika na kuwa katika kiwango
bora, tuimarishe usimamizi,tutunze mazingira Ili kuzuia wingi wa maji yanayokuja
hapa na katika hili niombe tu kwenye vikao vyetu vile vya kata ajenda ya
utunzaji wa mazingira iwe miongoni mwa mambo yanayojadiliwa katika vikao
hivyo,"alisisitiza Shekimweri
Kwa upande wake kaimu
Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma mhandisi Salome Kabunda amesema mipango
ya muda mfupi ni kuhakikisha wanakarabati barabara hiyo Ili iweze kupitika
katika kipindi hiki ambacho wanasubiri mipango ya muda mrefu ya kujenga
barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
"Hapa tunaendelea
na ukarabati ili barabara hizi ziweze kupitika,lakini kama Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi CCM ilivyoahidi kujenga kwa kiwango cha lami kazi hiyo
tutaitekeleza,"alisema Mhandisi kabunda
Wananchi wanasema
changamoto wanayoipata kwenye usafiri wakati wa mvua ni kubwa sana kukwama kwa
muda mrefu pia kupanda kwa nauli wakati huu wa mvua jambo ambalo huwakwamisha
kujichumi hivyo wameiomba serikali kuendelea kuwasaidia.
Mwisho.
0 Comments