MWONGOZO WA UTOAJI WA CHANJO ZA MIFUGO NCHINI WAZINDULIWA JIJINI DODOMA.


📌MWANDISHI WETU.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki amezindua mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini, wenye lengo la kuhakikisha sekta binafsi na umma zinajua haki na wajibu katika zoezi zima la utoaji wa chanjo na kuhakikisha afya ya mnyama inabaki salama.

Mara baada ya kuzindua mwongozo huo jijini Dodoma Januari 22,2021 Mhe.Ndaki aameagiza kusimamishwa kwa muda, utoaji wa chanjo unaofanywa na halmashauri nchini kupitia kampuni walizoingia nazo mikataba, baada ya kubaini chanjo kutolewa kiholela kwa mifugo bila kuwepo utaratibu sahihi na kusababisha madhara kwa mifugo na hasara kwa mfugaji.

Aidha Mhe.Ndaki amesema kuwa  katika kuhakikisha mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini, unakuwa na tija kwa taifa hivyo nataka haki na wajibu kwa kila wadau wa mifugo.

“Hapa tunaangalia  afya ya mifugo, afya ya mifugo ilikuwa hatarini ni kweli utaratibu wanafanya halmashauri lakini hauko wazi sana, ndiyo maana tukasema sasa ni muhimu kuwa na mwongozo huu kutuelekeza nini cha kufanya, chanjo ikifanywa vizuri kwa usahihi bila makosa tuliyokuwa tunayaona tunaweza kuwa na ng’ombe wenye afya bora na njema.” Amesema Mhe.Ndaki

Aidha, amesema kuwa mwongozo huo umeshirikisha wadau zaidi ya thelathini wakati wa kuundaa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo tayari kupokea maoni ya wadau sehemu ambazo mwongozo utaonekana kuwa na mapungufu ili kuurekebisha na kuufanya uwe bora zaidi, lengo likiwa ni kuhakikisha afya ya mifugo nchini inalindwa na mfugaji kutopata hasara ya mifugo yake kufa au kupata madhara mengine yoyote baada ya kuchanjwa.

Hata hivyo Mhe Ndaki amesema kuwa  wizara itahakikisha inaandaa mazingira mazuri ya kuwa pamoja na sekta binafsi ili kufanya kazi pamoja ambayo itakuwa na tija kwa taifa na wafugaji kwa ujumla.

“Sekta binafsi nipende kuwahakikishieni kuwa  sisi tutafanya kazi na sekta binafsi vizuri kabisa tusiwe na mashaka ni vile tuliona kasoro, lakini niwaombeni sekta binafsi hasa wale mlio vizuri katika jambo hili la chanjo msiwe na wasiwasi hata mkiingia mikataba na halmashauri ili mradi muwe na sifa na vigezo ndiyo maana ya sisi tukatoa mwongozo ili tufanye kazi pamoja.” Amefafanua Mhe.Ndaki

Hata hivyo Waziri Ndaki  amewataka viongozi wenzake wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mamlaka za serikali za mitaa, watoa huduma za afya ya mifugo na sekretarieti za mikoa wazingatie maelekezo yaliyopo kwenye mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini na kutoa maoni au kuuliza maswali sehemu ambazo zitakuwa na utata ili kuhakikisha mwongozo huo unatekelezwa kama ambavyo umezingatiwa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini.

Ameitaka pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoa nakala za kutosha za mwongozo huo kwa wadau wa sekta ya mifugo kote nchini na pia kuwataka wadau kupata nakala laini kupitia tovuti ya wizara hiyo, www.mifugouvuvi.go.tz.

Awali akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Mukunda amesema kuwa mkoa huo utahakikisha yale yote ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatamani yatokee katika Sekta ya Mifugo mkoa upo tayari kuyasimamia ili yalete tija kwa taifa na wafugaji.

“Ili pia mwongozo huu uweze kufanya vizuri kama ya wataalamu wa mifugo bado haitoshi hivyo ni vyema wataalamu waliopo katika ngazi za juu waweze kuwafikia pia wafugaji wa chini na tunataka kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kitovu cha kuzalisha nyama na maziwa kwa wingi.” Amesema Mhe.Mukunda

Mhe.Mukunda amesema kuwa  Sekta ya Mifugo kwa sasa imekuwa ikirasimishwa rasmi na kuifanya iheshimishe watu wanaofanya shughuli za mifugo kwa kuwa imekuwa na tija kubwa kwa taifa na mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amesema  kuwa serikali bado inahakikisha inafanya jitihada mbalimbali za kupata masoko zaidi ya mazao ya mifugo yenye ubora ambayo yanachochewa na uwepo wa chanjo bora na mifugo. 

“Wenzangu niwaombe mpokee huu waraka ulipo ukatusaidie ili malalamiko ya mnada umeharibika au wilaya nzima kutokuwa na josho, hayo malalamiko yafike mwisho kupitia mapato mbalimbali ambayo halmashauri wamekuwa wakipata yakiwemo ya minada iliyopo kwenye wilaya hizo, wanapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kuyakarabati.” Amefafanua Mhe. Gekul

Naye  Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini Bw. Jeremiah Wambura amesema kuwa tasnia ya maziwa nchini ikisimamiwa vyema inaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa pato la taifa na kuhamasisha uwepo wa viwanda vingi vya kuchakata maziwa nchini.

Hivyo ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia vyema namna ya kuisimamia tasnia ya maziwa ili iwe na tija zaidi kwa taifa pamoja na kuongeza wingi wa maziwa ambayo yanaweza kutumika majumbani pamoja na kuchakatwa viwandani.

Mara baada ya uzinduzi wa mwongozo huo Mhe. Ndaki amesema kuwa kuanzia sasa mwongozo huo unaweza kutumika na huduma ya chanjo kuendelea kutolewa na sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali.

Post a Comment

0 Comments