AFYA ZA MAJERUHI WA AJALI YA TRENI ILIYOTOKEA KIGWE-DODOMA ZAENDELEA KUIMARIKA.



📌DEVOTA SONGORWA.

MAJERUHI 63 kati ya 66 wa ajali ya treni iliyotokea usiku wa kuamkia juzi, wilayani Bahi mkoani hapa ambao walikuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, wameruhusiwa baada ya hali zao kutengemaa.

Akitoa taarifa hiyo Jana Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Stanley Mahundo, alisema kati ya majeruhi 66 waliowapokea siku ya kwanza hospitali hapo  wamebaki majeruhi watatu ambao hali zao sio mbaya sana na wanaweza kutoka wakati wowote.

“Hadi kufikia leo (jana) tumebakiwa na majeruhi watatu ambao wawili ni wanaume na mmoja mwanamke kati ya majeruhi 66 tuliowapokea siku ya kwanza, kati ya hao 32 walikuwa katika hali isiyoridhisha na sita walifanyiwa upasuaji mkubwa huku wengine 34 waliruhusiwa baada ya hali zao kutengamaa,”alieleza

Dk. Mahundo alisema kati ya majeruhi hao watatu waliobakia hali zao sio mbaya sana na wanaweza kuwaruhusu muda wowote.

Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuboresha huduma za afya hapa nchini, hivyo imesaidia majeruhi kupona kwa haraka kutokana na kupatikana kwa vifaa na dawa kwa wakati.

“Naipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu ya afya, hivi sasa imekua tofauti na zamani tulipokea majeruhi wengi lakini hakuna hata mmoja aliyeandikiwa rufani kwenda kutibiwa kwenye hospitali kubwa, hiyo inadhiirisha kuwa sasa tumepiga hatua kwenye sekta ya afya,”alisema.

Kwa upande wake mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Niko Bihole, aliwapongeza wauguzi kwa juhudi na mchango walioonyesha katika kuhakikisha wanaokoa maisha ya majeruhi.

Alisema kazi waliyoifanya ni kubwa kutoka siku ya kwanza wamekuwa wakipambana kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma licha ya uwingi wa majeruhi uliokuwepo.

“Tunawapongeza wauguzi wa hospitali ya mkoa wa Dodoma na serikali kwa ujuml;a kwa jitihada walizozifanya katika kipindi hiki najua wamefanya kazi usiku na mchana licha ya kuwa ni wajibu wao lakini wametusaidia sana naomba wasdikate tamaa na ikibidi waongeze juhudi wafanye zaidi ya hapa,”alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma Dk. Damas Mukasa, alisema baada ya kutembelea majeruhi wa ajali ameridhishwa na huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo

Alisema wanampongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuiboresha sekta ya afya kwa kuboresha vifaa na madaktari bingwa ambapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya vifo ambavyo vilikuwa vinatokea kwa kukosa huduma bora za afya.

“Tumewatembelea majeruhi wa ajali treni tumeridhishwa na huduma zinazotolewa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma sio kwa majeruhi bali ni kwa wogonjwa wote ambao wapo hapa hospitali kongole za dhati ziende kwa Rais Dk. Magufuli haya ni matunda ya uongozi wake mzuri uliotukuka,” alieleza.

Post a Comment

0 Comments