📌Na MWANDISHI WETU.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka Wizara ambazo zina hoja 11 za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kukaa mara moja ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.
Waziri Ummy ameyasema hayo hii leo katika kikao cha pamoja baina yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Dkt. Khalid Mohammed mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.
Amesema tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha tunaimarisha Muungano wetu na kuhakikisha una kuwa imara kwasababu Muungano wetu ndio umoja wetu, usalama wetu na amani yetu.
“Hatutamvumilia mtu yoyote anayeleta chokochoko na kutaka kuvuruga umoja na mshikamano wa watanzania” Ummy alisisitiza.
“Kupitia
vikao vya Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ndani ya kipindi cha miaka mitano
jumla ya changamoto 21 ziliwasilishwa na kati ya hizo changamoto 10 zimepatiwa
ufumbuzi, ni imani yangu kuwa zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi kwa kuwa viongozi
wetu wana dhamira ya dhati” amesisitiza Dkt. Khalid.
Amesema
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar imeanza matayarisho ya ujenzi katika
kiwanja chenye ukubwa wa ekari 33 katika eneo la Mahoma Makulu, Dodoma ili
kurahisha kazi ya uratibu.
“Hakuna
sababu ya sisi kubaki Dar es Salaam, tutahakikisha tunahamia Dodoma mapema iwezekanavyo ili kufanya kazi kwa karibu”
Waziri Ummy amemuhakikishia Waziri Khalid kufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano.
0 Comments