IMEELEZWA Kuwa Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu
watumishi wa umma wasio waadilifu katika kuwatumikia wananchi.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania
Mizengo Pinda wakati akifungua Kongamano la siku ya Maadili na Haki za
Binadamu kwa watumishi wa Umma.
Amesema licha ya jitihada zinazofanywa na serikali
kuhakikisha watumishi wa Umma wanafanya kazi kwa weledi kufuata maadili
,inatambua kuwa wapo watumishi wachache wenye ubinafsi na hivyo kujihusisha na
vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya kazi zao.
“kila mmoja ameshamsikia Rais John Magufuli akizungumza
kwa ukali na uchungu habari ya watumishi wa umma wazembe na wasio waadilifu
kwamba hawana nafasi katika serikali anayoiongoza,
Amesema serikali imefanya jitihada nyingi katika
kuhakikisha kuwa utumishi wa umma unajengeka na kuwa wa kutegemewa na umma .
“Ni matarajio yangu kuwa kongamano hili litahitimishwa
kwa maazimio yenye lengo la kuboresha maeneo yote ambayo mtakubaliana kuwa yana
upungufu katika uzingatiaji wa maadili mapambano dhidi ya rushwa,
uwajibikaji na uzingatiaji wa haki za binadamu”amesema
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Mkuchika,amesema Serikali
kupitia taasisi na vyombo vilivyopewa majukumu ya kusimamia maadili
itazidi kuongeza ufanisi wake katika kusimamia misingi ya maadili na utawala
bora ili kuwa na Tanzania yenye amani.
Ameongeza kuwa Juhudi za serikali katika
mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora zinatambulika ndani na nje ya nchi
ambapo katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa ikitolewa mfano wa nchi
zilizofanikiwa katika masuala ya uadilifu ,mapambano dhidi ya rushwa na
matumizi mazuri ya rasilimali za nchi kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha kwa kutambua changamoto za rushwa na ukosefu wa maadili
kwa baadhi ya taasisi, serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja
na mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa na Mpango wa utekelezaji awamu ya tatu
ambao ulizinduliwa Desemba 10,2016.
“Mkakati huu unaainisha majukumu ya kila sekta hivyo wadau
wote wanapaswa kuupitia na kuhakikisha wanatoa mchango kwa jamii katika
mapambano dhidi ya rushwa nchini kwani ni jukumu la kila mtanzania,”
amesistiza.
Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuchambua masuala ya
utawala bora,maadili,udhibiti wa rushwa na usimamizi wa haki za binadamu
“Maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu
hufanyika kila mwaka hapa nchini na hii imetokana na siku ya kimataifa ya
kupambana na rushwa na siku ya haki za binadamu ambapo kwa mara ya kwanza
ilianza kufanyika mwaka 2016.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ”Uzingatiaji wa ahadi
ya uadilifu kwa viongozi na watumishi kwa ustawi na utawala bora na haki za
binadamu nchini”
0 Comments