📌RACHEL CHIBWETE
WAKATI dunia ikiwa kwenye maashimisho ya siku 16 za kupinga
ukatili, umeelezwa kuwa wanawake bado wanakwamisha kesi za ukatili kwa
kuwaficha wanaume wanaowafanyia ukatili kwa kuwa ndiyo wanaowategemea kiuchumi.
Hayo yamebainishwa kwenye kikao cha asasi za kiraia
zinazojishughulisha na masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia kilichofanyika
Jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye kikao hicho cha tathmini Mratibu wa mradi
huo kutoka Mtandao wa Kijinsia (TGNP) Zainabu Mmari amesema Kuna kila sababu sasa ya wanawake na
wasichana kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kuwafichua wanaume wanaowafanyia
ukatili huo wa kijinsia.
Hapa inaonekana kuwa changamoto inayowakabili watu wengi ni baadhi ya wanawake kuwaficha wanaume wanaowafanyia ukatili wa kijinsia kwa kuwa hao hao wanaume ndiyo wanaowapa mkate wao wa kila siku na hivyo kushindwa kuwaripoti kwenye vyombo vya sheria.Zainabu Mmari
Ameongeza kuwa, "Ili Sasa wanawake hao waamke na kupaza
sauti zao pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili ni lazima wawe na shughuli zinazowaingizia kipato hiyo
itasaidia kuwaripoti kwenye vyombo vya sheria wanaume wanaowafanyia ukatili wa
kijinsia."
Amesema vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia hufanyika kwa
wanawake na watoto lakini baadhi yao hulazimika kukaa kimya kwa sababu
wanaowafanyia ukatili huo ni waume zao hivyo wakishikiliwa na vyombo vya
sheria watabaki wanateseka na watoto wao.
Kwa upande wake mratibu wa miradi kutoka shirika lisilo la
kiserikali la Peace Relief Organization (PRO) Reuben Charles alisema wanawake
wengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili na waume zao lakini wanaogopa kuwaripoti
kwa kuhofia kuachika kwenye ndoa zao.
Charles amesema siyo kila kesi ya ukatili wa kijinsia huishia kwa
mtuhumiwa kufungwa bali kunaweza kutokea suluhisho la kudumu kupitia vyombo vya
sheria bila mtuhumiwa kuhukumiwa kifungo gerezani.
Amesema ni wakati sasa wa kuwajengea wanawake uwezo wa
kisheria ili wajue haki zao hasa pale wanapokutana na unyanyasaji wa kijinsia
ili wajue mahali pa kupata haki zao kisheria.
Naye Mwanasheria wa TGNP Consolata Chikoti amesema endapo
kesi za ukatili wa kijinsia zitaripotiwa na kutatuliwa kwa wakati zinasaidia
waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kupata haki yao kwa wakati.
Amesema madhara ya kuchelewesha kesi hizo ni pamoja na
kupoteza ushahidi muhimu dhidi ya watuhumiwa na kutoa nafasi kwa watuhumiwa au
ndugu zao kutoa vitisho vya waathirika wa vitendo vya ukatili na hivyo
kusababisha kufuta kesi mahakamani au kutotokea kwenye kesi
0 Comments