KUELEKEA siku kuu ya mwaka mpya viongozi wa umma na watanzania wametakiwa kujitathimni kuhusu utendaji wao kwa mwaka mzima na kwa namna gani wanajipanga kutekeleza majukumu kwa uadilifu kwa maslahi ya Taifa.
Akizungumza jana na gazeti hili Sheikh Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajabu Shaban alisema kufanya tathimini huwezesha
kutambua ikiwa malengo yaliyokusudiwa yalifikiwa na kufanyia kazi changamoto
zilizojitokeza.
“Kwanza tumshukuru Mungu kwa kutujalia uzima
mwisho mwaka huu ni wa kujitathimini kuanzia Kaya, Wilaya, Mkoa hadi
Taifa kwamba je, katika mwaka uliopita wamefanya nini,yapi
hayajatekelezwa wajue ni kwanini na wanajipanga vipi mwaka ujao wa
2021”,alisema Sheikh Shaban.
Akizungumzia suala la kulinda amani alihimiza
watanzania kuheshimu,kulinda amani na utulivu katika nchi badala ya kutumika
kuharibu tunu hiyo muhimu akisistiza kusameheana kutokana na
mapungufu ya kibinadamu na kuanza mwaka upya kwa upendo na mshikamano.
“Sisi hatuna cha kumlipa Mungu zaidi ya
kufanya toba,majuto na kujiongeza zaidi kumjua Mungu na uwe mwaka wa kudumisha
amani siyo kupanga kuvuruga kama tumeishi vyema mwaka uliopita tujiulize tulitumia
vigezo gani kuwa salama hadi sasa?”,alieleza Sheikh huyo.
Naye Mchungaji wa Kanisa la International
Evengelism Church,Askofu Sylvester Thadey alisema ipo sababu ya kila mmoja
kumshukuru Mungu kwa kulipigania Taifa mwaka 2020 dhidi ya ugonjwa
wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona(COVID-19) na
kusheherekea kwa amani mwaka mpya.
“Nitoe salamu za kheri ya mwaka mpya na
tunapoanza mwaka mpya waumini wa imani zote tufanye kazi kwa bidii kuunga
juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuinua uchumi wetu,wazazi na walezi nao
niwasihi kuwalea watoto wao katika maadili mema kwani ndiyo nguvu kazi ya Taifa
kwa siku zijazo”,alifafanua Askofu Thadey.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi
MKoa wa Dodoma,Gilles Muroto alitoa onyo kwa baadhi ya watu watakaofanya fujo
au vitendo vya uhalifu wakati wote hasa kipindi cha siku kuu akisema jeshi
halitomfumbia macho mtu huyo.
“Sisi Jeshi tuko imara kuhakikisha watu
wanasherehekea salama na tumeshirikisha wenye nyumba za wageni, vikundi vya
ulinzi shirikishi kutoa taarifa za watu ambao wanawatilia shaka, tuna
doria za magari,miguu na tuwatake wazazi kuwa makini na watoto wao”,alisisitiza
Kamanda Muroto.
Akitoa salamu za mwaka mpya Neema Chitete
mkazi wa Chamwino aliishauri jamii kupendana na kushirikiana katika shughuli za
uzalishaji kwa kupeana fursa za kiuchumi kujiletea maendeleo kwa mwaka ujao.
Aidha Rehema Suleiman Idd alieleza mwaka huu
umekuwa wenye historia kubwa kwa nchi kutokana na ugonjwa wa COVID-19
ulioyakumba mataifa mengi Duniani akiwaomba watanzania kumtegemea Mungu katika
maisha yao na kuishi kwa malengo.
0 Comments