UDUMAVU UNAUA NDOTO ZA WATOTO.

 


📌DEVOTHA SONGORWA.

MKURUGENZI wa Idara ya Usalama wa Chakula Wizara ya Kilimo Dk. Honest Kessy amesema Serikali imefanya juhudi kubwa ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo mazao inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la utapiamlo.

Amesema  taarifa ya matokeo ya mapitio ya nusu mwaka ya Mpango wa Kitaifa wa Lishe (Mid Term Review – MTR) imeonyesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula hasa mahindi umekuwa ukiongezeka akisema eneo linaloonekana kutofanya vizuri ni  uzalishaji wa mazao mchanganyiko na ulaji unaofaa kukidhi mahitaji ya virutubishi katika mwili.

Ameyasema hayo jana jijini Dodoma katika kikao kazi cha kuandaa mpango kazi wa kutekeleza afua za lishe katika kilichoshirikisha  wadau wa kilimo ikiwemo Shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa (FAO),WFP unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa FIRST ambao umeanza 2020 unaotarajiwa kukamilika 2025.

“Ukiangalia ile mikoa inayozalisha chakula kwa wingi kama Rukwa,Songwe, Ruvuma,Njombe,Iringa na Kigoma wapo zaidi asilimia 40% ya udumavu kwa sababu ya uelewa,utamaduni na njia za maisha ya wale watu na tunaweza kupunguza hili kwa kuendelea kutoa elimu.

Wizara tumejipanga kupitia mpango huu jumuishi unaoonyesha kila mdau ana sehemu ya kufanya kuanzia ngazia za mikoa hadi vijiji kukabili udumavu",alisema Mkurugenzi huyo.

Ameeleza kwamba Wizara ya Kilimo ni miongoni mwa Wizara zinatotekeleza Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe (National Multi- sectoral Nutrition Action Plan) na kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili yaani ASDP II ambapo mikakati hii yote imetambua   umuhimu wa kilimo katika kuboresha lishe.

Kwa upande wake Afisa Lishe kutoka FAO, Stella Kimambo alisema licha ya kuwepo ukuaji chanya wa kiuchumi nchini Tanzania, udumavu bado unawaathiri theluthi moja ya watoto wenye umri wa chini ya miezi 60 wakati  viwango vya udumavu vimepungua katika kipindi cha miongo miwili iliyopita kutoka asilimia 48.3 mwaka 1999 hadi asilimia 31.8 mwaka 2020.

"Tunahitaji kutatua vyanzo vyenye mzizi ya kina vya lishe duni ,nyaraka za programu za ASDP II na NMNAP hazina budi kutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili ili kuwafikia watu wengi zaidi ,wakulima wengini nchini  hawapati taarifa za kutosha kuhusiana na tabianchi na   Kuongoza sera na programu ili kuunganisha matokeo ya kilimo na lishe”,alieleza Stella.

 

Aidha Afisa kilimo mkuu Wizara ya kilimo Magreth Natai alifafanua kwamba serikali,wizara wanashirikiana na wadau wa maendeleo kwa kuweka mpango jumuishi unaohusisha wizara tisa kupitia mpango wa kitaifa wa lishe na mpango wa maendeleo wa kilimo ASDP II.

“Huu ni mpango wa kwanza wa kutekeleza lishe katika kilimo sasa tutaweza kujiratibu,kufanya ufuatailiaji kuanzia kwa wadau hadi wakulima na ni maika mitano tunalenga kukabili utapia mlo katika jamii zetu”,alifafanua Magreth.

Washiriki wa mkutano wa kupitia Mpango Kazi wa Kutekeleza Kazi zinazohusu Lishe katika Sekta ya Kilimo  wakimsikiliza Dkt. Honest Kessy (Hayupo pichani) jana katika hoteli ya Nashera, Jijini Dodoma. 
Mkurugenzi Idara ya Usalama wa Chakula Wizara ya Kilimo Dkt. Honest Kessy akihutubia baadhi ya washiriki wa mkutano wa kupitia Mpango Kazi wa Kutekeleza Kazi zinazohusu Lishe  katika Sekta ya Kilimo Jana katika hoteli ya Nashera, Jijini Dodoma.


Post a Comment

0 Comments