📌Na HAMIDA RAMADHANI.
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara kuu ya Afya Prof. Mabula Mchembe amewataka Maafisa Afya ngazi zote kufanya kazi zao kwa weledi na kufuata maadili wakati watimizapo majukumu yao katika jamii.
Prof. Mchembe ameyasema hayo, wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Afya mazingira wenye kauli mbiu ya "Zingatia mahitaji ya Jinsia kwa usafi wa mazingira endelevu " uliofanyika Jijini Dodoma.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, ambae pia ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amewaagiza Waganga wakuu wa mikoa kutoa elimu mara kwa mara kwa watendaji wao juu ya maadili badala ya kusubiri kuchukua hatua baada ya kosa kujitokeza.
"Kutoa elimu mara kwa mara kuhusu maadili, badala ya kusubiri kuchukua hatua kwa Maafisa Afya au wana taaluma wenu, wanapokiuka au kufanya makosa mbali mbali " alisema Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Subi.
Aliendelea kusema kuwa, baadhi ya maeneo hususan mijini bado kuna hali ya usafi wa mazingira usioridhisha, na kuelekeza kuanza kampeni ya usafi wa mazingira ya muda wa miezi miwili, huku akiwataka kuanza oparesheni hiyo kwa kuzingatia Sheria na kanuni za afya ya mwaka 2009.
Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali amewaagiza Maafisa Afya mazingira, kukagua suala la usafi wa mazingira kwenye shule, mabweni, maofisi na maeneo yote yenye mikusanyiko ili kuhakikisha usafi wa mazingira unapewa mkazo ili kuikinga jamii dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.
Wakati huo huo
Mwenyekiti wa Maafisa afya mazingira nchini Bw. Evans Simkoko ameiomba Serikali
kuipa kipaumbele kada ya Maafisa Afya mazingira kwenye ajira mpya, ili kuongeza
ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi, kisha kuikinga Jamii dhidi ya
maambukizi ya ugonjwa ya milipuko.
0 Comments