📌PRISCA ULOMI, WMTH.
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amelitaka Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) kushughulikia malalamiko ya wananchi na changamoto wanazozipata wakati wanatumia huduma na bidhaa za mawasiliano nchini
Dkt.Ndugulile
ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TCRA – CCC akiwa ameambatana
na Naibu Waziri wake, Mhandisi Andrea Kundo Mathew kwa malengo ya kukutana na
bodi, menejimenti na wafanyakazi wa taasisi za Wizara yake ili waweze
kufahamiana, kutambua majukumu yao na kuweka mwelekeo wa utendaji kazi wenye
matokeo ili kufikia matarajio na ndoto za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuunda Wizara hii mpya
Amesema
kuwa wananchi wana malalamiko kuhusu huduma wanazozipata hususani kwenye
mitandao ya simu kuhusiana na mabando yao kuisha, kubadilishiwa gharama za
matumizi ya mabando, kupunjwa mabando yao na fedha wanazotuma kwa njia ya
mtandao na haya yote yanahitaji majibu na kupatiwa matibabu
“Hatutaki
kufanya kazi kwa mazoea, nitawapima kwa matokeo na sio michakato, tutakwenda
kwa mwendo wa takwimu na kila baada ya miezi mitatu tupate taarifa ya
malalamiko mangapi yamepokelewa, mangapi yamefanyiwa kazi, mangapi yameisha na
kwa nini mengine hayajaisha kwa kuwa haya ni mambo ya msingi ambayo tunatakiwa
tuyaangalie na tuwe taasisi ya kutatua changamoto za wananchi,” amesisitiza
Dkt. Ndugulile
Ameongeza
kuwa ni vema tuweke mifumo ya kulinda watumiaji na walaji wa huduma za
mawasiliano na bidhaa za TEHAMA na taarifa na siri zao kwa kuwa sekta hii
inaendelea kukua na watu wanatumia biashara mtandao na hawaendi madukani na
tumieni lugha nyepesi kuelimisha wananchi namna ya kutumia huduma na bidhaa za
TEHAMA na muwe na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa Baraza ili kutekeleza
sheria ya TCRA iliyounda Baraza
Katika
hatua nyingine ameitaka Tume ya Taifa ya TEHAMA kuishauri vizuri Wizara ili
kufahamu mwenendo na mwelekeo wa wapi tunataka tupeleke TEHAMA ndani ya nchi na
tujue tuna wataalamu wangapi wa TEHAMA, tunahitaji wataalamu wa namna gani na
waje watibu changamoto za aina gani.
“Tumejiwekea
malengo ya kuhakikisha kuwa matumizi ya brodibandi yanafikia asilimia 80
ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 45 ya mwaka 2020 ili wananchi wanufaike na
huduma za mawasiliano”, amefafanua Dkt. Ndugulile
Naye
Naibu Waziri, Mhandisi Kundo Andrea Mathwe ameongeza kuwa TCRA na TCRA CCC ni
taasisi zilizo chini ya Wizara na moja inashughulika na watoa huduma na
nyingine watumiaji wa huduma ambapo ni rahisi kufanya nao kazi na kuishauri
Wizara kutatua malalamiko ya wananchi kwa kuwa mwananchi anaweza kulalamika
kuwa ameibiwa bando kumbe akielemishwa atafahamu vizuri kwanini bando limeisha
na hii itawafanya wananchi wavutiwe zaidi kutumia huduma za mawasiliano na
hatimaye tutachangia pato la taifa ili kufikia malengo yaliyowekwa kwenye Ilani
ya CCM ya mwaka 2020 – 2025
Katibu
Mtendaji wa TCRA CCC, Mary Shao Msuya amesema kuwa Baraza limejipanga
kushughulikia maelekezo yaliyotolewa kwa kuwa watumiaji wa huduma na bidhaa za
TEHAMA wameongezeka tofauti na mwaka 2003 wakati Baraza linaanzishwa ambapo
kulikuwa na huduma chache ya kupiga na kupokea simu na za vifurushi tu wakati
hivi sasa kuna huduma za kutuma na kupokea pesa, tutaongeza kasi ya utendaji
kazi ili twende na kasi ya ukuaji wa TEHAMA nchini
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA amesema kuwa watazingatia suala la usajili wa
wataalamu wa TEHAMA pamoja na maeneo yao ya ubobezi ikiwemo usalama wa mtandao;
utengenezaji wa programu; uchakataji na uhifadhi wa taarifa na data; na ubunifu
ili nchi iwe na wataalamu wa kutosha na kuendana na mahitaji kwa kuzingatia
kasi ya ukuaji wa TEHAMA duniani
Dkt.
Ndugulile ataendelea na ziara yake kwenye taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo
ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania
(TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC) ambapo atazungumza na bodi, menejimenti
na wafanyakazi
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
0 Comments