WAZIRI Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ameomba Serikali kuboresha posho na maslahi ya walimu hasa wanaofundisha shule za awali akisema kazi yao ni ngumu na wanastahili kupongezwa.
Pinda ambaye ni
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ametoa kauli hiyo wakati wa kugawa
vyeti kwa walimu 436 wa shule za msingi kutoka wilaya za Chemba na Mpwapwa.
Walimu hao
walikuwa kwenye mafunzo maalumu ya Stashahada kwa walimu wanaofundisha shule za
msingi katika masomo ya awali ambao mafunzo yao kwa miaka miwili yaligharamiwa
na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Mstaafu huyo
aliahidi kuwa atawasiliana na Waziri wa Elimu (Profesa Joyce Ndalichako) ili
kufikisha kilio cha walimu kuhusu maslahi na posho zao lakini kwake anaamini
wanaofundisha madarasa ya chini ndiyo wanastahili kupewa kipaumbele licha ya
kuwa kazi ya kufundisha ni ngumu.
“Kwa kweli
tukubaliane, posho za walimu hasa wa masomo ya awali ni muhimu zikatazamwa
upya, na mimi nitazungumza na Waziri angalau nifikishe kilio chenu kwake ili
waone namna ya kulifanya jambo hili ambalo naamini likitekelezwa litaleta
tija,” amesema Pinda.
Akizungumzia
walimu hao, aliwataka kuwa na mabadiriko chanya katika shule wanazokwenda
kufundisha ili wasio na elimu kama yao wakajifunze umuhimu na faida ya Mwalimu
kusoma zaidi.
Amesisitiza kwa
Serikali na CWT kuwasiliana na wadau wengine kwa pamoja wafufue vituo vya
walimu (Teacher Center) ambavyo vilikuwa ni msaada katika kuwafanya walimu
waende na wakati.
Amekiagiza OUT
kuanzisha mjadala kuhusu ubora wa elimu nchini ambao unalalamikiwa na wengi
kuwa umeshuka ili waone kama kuna ukweli wowote kuhusu kauli hiyo na nini cha
kufanya.
Rais wa CWT Leah
Ulaya,amesema pamoja na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, lakini walimu bado
wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo suala la maslahi yao kutoboreshwa.
Ulaya alimwomba
Pinda kufikisha kilio chao kwa Rais John Magufuli ili aweze kuwatazama kwa
jicho la Huruma huku wao wakiahidi kufanya kazi katika mazingira yoyote
watakayopangiwa.
Awali Katibu wa
CWT Deus Seif amesema waliwadhamini walimu hao kusoma Stashahada kwa
ushirikiano Shirikisho la vyama vya walimu duniani (EI).
Seif alisema CWT
imeachana na mpango wa malalamiko badala yake kimeamua kujikitza zaidi kwenye kuwasomeha
walimu ili wawe na manufaa na uelewa wa pamoja ambao utazaidia kulijenga Taifa.
0 Comments