PINDA ASEMA KUNA HAJA YA MITAALA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA KWENYE KILIMO.

 


📌FAUSTINE  GIMU GALAFONI

WAZIRI mkuu mstaafu wa Tanzania  Mizengo Peter Pinda amesema sasa kuna haja kubwa Kwa serikali kuandaa mitaala ya shuleni itakayowajengea uwezo vijana kujikita zaidi kujiajiri kwenye sekta ya kilimo pindi wanapohitimu masomo ili kupunguza tatizo la ajira nchini. 

Pinda amebainisha hayo leo Disemba 3,2020 jijini Dodoma wakati akifungua Mafunzo ya wadau wa kilimo nchini yaliyoandaliwa na jukwaa la wadau wa kilimo wasio  wa kiserikali, Agricultural Non state Actors Forum(ANSAF)ambapo amesema hali hiyo itaondoa utegemezi kwa vijana. 

Aidha, Waziri mkuu huyo mstaafu amesema sekta ya kilimo inayo ufanisi Mara 11 zaidi katika kuo,ndoa umasikini ambapo amebainisha kuwa ili kukuza uchumi wezeshi lazima kuongeza nguvu kwenye sekta ya kilimo hasa kwa kutumia viwanda. 

Hali kadhalika Pinda amesema dola bilioni 100 zilikuwa zikipotea kwa mwaka hapa nchini kutokana na uuzaji wa bidhaa ghafi za korosho nje ya nchi kwa mujibu wa utafiti wa ANSAF. 

Pia amesema kwa mujibu wa shirika la kazi duniani, tatizo ajira bado lipo  zaidi ya asilimia 11 kwa vijana huku akibainisha kuwa changamoto ya kilimo ni kutokana na baadhi ya wasomi kudharau kilimo ambapo amesema unakuta kuna Profesa wa kilimo na mifugo lakini hana hata robo moja tu ya shamba.

Katibu Mkuu wizara ya kilimo Gerald  Kusaya amesema changamoto zinazowakabili vijana kwenye sekta ya kilimo ni changamoto ya masoko pamoja na upatikanaji wa ardhi ambapo halmashauri zimeagizwa kutenga maeneo ya kilimo kwa vijana. 

Pia Kusaya amesema Wizara ya Kilimo imeandaa mazingira mazuri ya utafiti wa wa aina ya udongo kwa kilimo cha mazao husika ambapo kuna sampuli za udongo  elfu 30 na 40 zimekusanywa kwa ajili ya utafiti wa kilimo. 

Mwakilishi wa katibu mkuu wizara ya mifugo na uvuvi Prof. Ole Sante Gabriel, Bw.Amos Zefania amesema asilimia 30 ya pato la taifa inatokana na mifugo huku wastani wa unywaji wa maziwa ni Lita 49 kwa mwaka ikilinganishwa na Lita 200 Kwa mtu mmoja hapa nchini. 

Pia,amebainisha kuwa wizara imeanzisha dawati la sekta binafsi katika kuwezesha vijana. 

Mwakilishi kutoka taasisi ya Maendeleo ya Mwalimu Nyerere amesema Siku hizi vijana wameacha msingi bora wa kilimo vijijini na kwenda mjini kuuza vitumbua, pipi na mihogo hivyo kunahitaji mabadiliko. 

Mkurugenzi mtendaji wa ANSAF Audax Rukonge amesema kuna haja ya kuwa na sera ya kuwajengea vijana Katika kupata ajira ambapo takwimu zinaonesha kuwa vijana wa vijijini wana fursa zaidi ya kujiajiri kuliko wa mjini. 

Naye mwenyekiti wa ANSAF Edmond Joseph Ringo amesema lengo kuu la jukwaa La ANSAF ni kufanya ushawishi wa kisera na kufanya tafiti kuchambua maeneo yenye changamoto kwenye sekta ya Kilimo.

Post a Comment

0 Comments