MASWAHIBU 10 YANAYOWAPATA WAANDISHI WA HABARI DUNIANI WAKATI WA COVID 19

 


📌JOHN BANDA

MLIPUKO wa ugonjwa wa COVID-19 umeathiri mwenendo wa wanahabari katika kutimiza majukumu ya kuuhabarisha umma ambapo nchi nyingi zimetumia ugonjwa huo kama sababu ya kuminya uhuru wa vyombo vya habari.

Hatua zilizochukuliwa kwa sababu ya virusi vya corona zimebadilisha kazi ya uanahabari kwa njia zisizoweza kutabirika kama ambavyo matukio ya kigaidi yalivyochochea kutungwa sheria za kukabiliana na ugaidi, hivyo kusababisha ongezeko la visa vya wanahabari kufungwa.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kutetea Waandishi wa Habari Duniani (CPJ), imeorodhesha mambo 10 ambayo yamegeuka mwiba kwa wanahabari katika kutimiza majukumu yao hususan kuripoti habari kuhusu Covid 19.

 

SHERIA DHIDI YA TAARIFA ZA UONGO

Baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa Corona, nchi nyingi zilikuja na kisingizio kipya cha kupitisha au kutekeleza sheria zinazoharamisha usambazaji wa taarifa za uzushi, kupotosha au uongo.

Ofisa sheria wa ngazi ya juu nchini Uingereza anayefanya kazi na shirika la  Media Legal Defence Initiative, Carlos Gaio, anasema sheria dhidi ya taarifa za uzushi, zitaendelea kuenea duniani kwa sababu serikali zinajaribu kudhibiti uenezaji wa habari kuhusu virusi hivi.

Anasema sheria hizo zitawaathiri wanahabari na ni jambo hatari kwa uhuru wa kukusanya na kutoa taarifa.

Gaio anabainisha kuwa, taarifa za uzushi ni tatizo kubwa, lakini sheria zinazozipa serikali uhuru wa kuamua ni habari gani zitaelezwa kuwa za uongo, jambo hilo ni hatari kwa wanahabari ambao ni wakosoaji wa serikali.

Nchini Marekani, Rais Donald Trump mara kwa mara amekuwa akikosoa ripoti za vyombo vya habari kuhusu COVID-19 kwa kutumia maneno ya kudhalilisha kwa kuziita “taarifa za uzushi.”

Kufuatia matukio hayo, CPJ imebaini kwamba baadhi za serikali zimefanikiwa katika kuvishusha hadhi vyombo ya habari na kupunguza imani kwa umma kwenye vyombo hivyo.

Afrika Kusini, Machi 18 mwaka huu, iliharamisha taarifa za uzushi kuhusu janga hili na adhabu yake ni pamoja na faini kubwa na kifungo jela.

Puerto Rico, Aprili sita mwaka huu ilitangaza kuwa ni hatia kwa vyombo vya habari kueneza au kuruhusu kuenezwa kwa taarifa za uzushi na wanaokiuka sheria hiyo wanaweza kufungwa hadi miezi sita gerezani na kutozwa faini ya hadi $5000.

 

KUFUNGWA JELA KWA WANAHABARI

Jambo la pili ambalo baadhi ya serikali zimekuwa zikichukua hatua dhidi ya wanahabari tangu kuibuka kwa maambukizi ya Corona ni kuwafunga wale wanaonekana kukiuka maagizo ya serikali.

Kwa mujibu wa CPJ, hadi sasa zaidi ya wanahabari 250 wamefungwa katika mataifa mbalimbali duniani.

CPJ na mashirika mengine 190 kwa pamoja wametoa wito kwa watawala kote duniani kuwaachia huru wanahabari wote waliofungwa kwa sababu ya kutekeleza kazi yao.

Nchini India, watawala katika jimbo la Tamil Nadu, Aprili 23 mwaka huu walimkamata mwanzilishi wa tovuti ya habari ya SimpliCity kwa kumtuhumu kuwa alikuwa amevunja sheria ya zamani ya magonjwa ya mlipuko na sheria nyingine.

Tovuti hiyo ilikuwa imechapisha ripoti zilizodai kulikuwepo na ufisadi serikalini wakati wa kusambaza chakula cha msaada wakati wa ugonjwa wa Corona.

Jeshi nchini Jordan, liliwakamata wanahabari wawili wa runinga ya Roya TV mnamo Aprili 10 mwaka huu kuhusiana na ripoti iliyoangazia malalamiko ya wafanyakazi kuhusu athari za kiuchumi za amri ya kutotoka nje.

Kadhalika, watawala nchini Somalia walimkamata mhariri wa shirika la habari la Goobjoog Media Group, mnamo April 14 mwaka huu na kumtuhumu kwamba alieneza habari za uongo na kumvunjia heshima rais baada ya mwanahabari huyo kuchapisha ujumbe kwenye Facebook uliokosoa jinsi serikali ilivyokuwa inalishughulikia janga la Corona.

KUZUIA UHURU WA KUJIELEZA

Baadhi ya hatua za dharura za serikali duniani zimehusisha kubatilisha au kusimamisha haki ya uhusu wa kujieleza kipindi cha hali ya dharura wakati huu wa ugonjwa wa Corona.

Nchini Honduras, Machi 16 mwaka huu ilitangaza hali ya dharura ya muda ambayo ilisimamisha utekelezaji wa baadhi ya vifungu vya katiba, kikiwemo kifungu kinacholinda haki ya uhuru wa kujieleza (ingawa serikali ilibadilisha hatua hiyo siku chache baadae).

UDHIBITI WA HABARI

Mamlaka katika mataifa kadhaa zimesitisha uchapishaji na usambazaji wa magazeti katika kile ambacho walisema ni juhudi za kudhibiti kusambaza kwa COVID-19 huku mataifa mengine, mamlaka zinazosimamia vyombo vya habari zimefungia mitandao ya habari au kuondoa makala za mtandaoni zinazokosoa serikali.

Nchi za Jordan, Oman, Morocco, Yemen, na Iran zote zilisimamisha usambazaji wa magazeti Machi, mwaka huu.

Tajikistan nayo iliifungia tovuti huru ya habari ya Akhbor, Aprili 9 mwaka huu, baada ya kuchapishwa taarifa zilizoikosoa serikali.

Mamlaka inayosimamia vyombo vya habari nchini Urusi (Roskomnadzor), iliamuru kituo cha redio cha Ekho Moskvy, kutopeperusha mahojiano na mtaalamu wa magonjwa, na mtandao wa habari wa Govorit Magadan ulishurutishwa kuondoa mtandaoni makala kuhusu kifo kilichotokana na nimonia.

VITISHO

Kiongozi wa Chechnya, Ramzan Kadyrov, alimtishia mwandishi wa gazeti la Novaya Gazeta baada chapisho la Aprili 12 mwaka huu, lililoeleza kwamba Wachechen walikuwa wameacha kutoa ripoti wanapokuwa na dalili za virusi vya Corona kwa hofu ya kubandikwa kuwa magaidi.

Wanahabari nchini Haiti walishambuliwa na wanaume wasiojulikana katika Ofisi ya Taifa ya Vitambulisho, Aprili 2 mwaka huu, walipokuwa wanachunguza madai kwamba ofisi hiyo ilikuwa inakiuka mwongozo wa COVID-19 kwa watu kukaa mbali na wengine.

Aidha, wanajeshi wa Ghana waliokuwa wakitekeleza masharti kuhusiana na janga hili waliwapiga wanahabari wawili katika matukio mawili tofauti, Aprili mwaka huu.

KUPUNGUZWA KWA UHURU WA KUSAFIRI

Tangu kuibuka kwa maambukizi ya ugonjwa huu, baadhi ya mataifa yamepunguza uwezo wa wanahabari kusafiri na kutembea kwa uhuru, wanapotaka kuripoti wakati wa amri ya kutotoka nje au kuingia hospitalini kupata taarifa za moja kwa moja kuhusu huduma.

Wakati mwingine wanahabari wanapewa vibali maalumu, lakini takwa kwa wanahabari kuwa na vitambulisho vinavyotolewa na serikali kunawaruhusu viongozi kuamua ni nani ataruhusiwa kuhudumu kama mwanahabari.

Polisi nchini India, waliwashambulia wanahabari wanne katika visa vitatu tofauti kwenye maeneo ya Hyderabad na Delhi, mnamo Machi 23 mwaka huu, walipokuwa wanasafiri wakati wa zuio la kutosafiri.

Nigeria nayo iliwahitaji wanahabari kuwa na kitambulisho kuwawezesha kusafiri katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa na zuio la usafiri, ikiwemo mji mkuu Abuja na ilitangaza kwamba ni wanahabari 16 pekee walioruhusiwa kuingia makao ya rais.

KUZUIA KUFIKIWA KWA HABARI

Sheria kuhusu uhuru wa kupata habari zinazoruhusu wanahabari kuomba taarifa na stakabadhi za serikali zimesimamishwa kwenye baadhi ya nchi.

Mikutano na hafla ya kiserikali ambazo wanahabari huhudhuria imehamishiwa mtandaoni ambapo kuna viwango mbalimbali vya kuruhusiwa kwa wanahabari kushuhudia au kupata habari.

Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro mnamo Machi 23 mwaka huu, aliidhinisha hatua ya kisheria inayosimamisha marufuku kwa maofisa wa umma na taasisi kujibu maombi ya habari na pia hatua hiyo inaondoa fursa ya kukata rufaa iwapo ombi litakataliwa. (Mahakama ya Juu ya Brazil ilibatilisha hatua Aprili 30 mwaka huu).

Magavana na mameya nchini Marekani wameweka pia masharti mbalimbali ya kuhudhuria vikao na wanahabari.

Gavana wa jimbo la Florida, Machi 28 mwaka huu, alimzuia mwanahabari kuhudhuria kikao cha wanahabari alipouliza swali kuhusu hitaji la watu kutokaribiana.

KUNYIMWA VIZA

China na Marekani zimekuwa kwenye hali ya vuta nikuvute kuhusu uhuru wa wanahabari tangu kuibuka kwa ugonjwa wa Corona.

Mvutano huo ulisababisha Februari mwaka huu China kuwafukuza wanahabari watatu wa Wall Street Journal, kama hatua ya kulipiza kisasi kuhusu kichwa cha habari kwenye makala ya maoni kuhusu COVID-19.

Machi mwaka huu, Marekani nayo iliweka kikomo cha wanahabari wa vyombo vya serikali ya China ambao wangepewa, China nayo ilijibu kwa kufutilia mbali viza za  wanahabari 13 wa Marekani kutoka The New York Times, The Washington Post na The Wall Street Journal.

Misri ilimfukuza mwandishi wa habari wa gazeti la Guardian, Ruth Michaelson, kulipiza kisasi taarifa yake ya Machi 15 mwaka huu iliyotilia shaka takwimu zilizokuwa zikitolewa na serikali kuhusu janga hilo.

UPELELEZI NA KUWAFUATILIA WATU

Serikali katika nchi mbalimbali duniani zinatumia data za simu kuchunguza walipo na wanakoenda baadhi ya watu na pia zinafanyia majaribio au kuanza kutumia program mpya za kuwafuatilia watu.

Upelelezi na ufuatiliaji huu unaweza kuwa tishio kwa usiri wa wanaotoa habari kwa wanahabari.

Carrie DeCell, Mwanasheria katika taasisi ya kutetea uhuru wa kujieleza Knight First Amendment Institute jijini New York, anasema vitendo hivyo vinaweza kukubalika katika hali Fulani, lakini havifai kukubalika baada ya serikali kudhibiti janga hili.

David Maass, Mtafiti mchunguzi wa ngazi ya juu katika wakfu wa Electronic Frontier Foundation wenye makao yake San Francisco, anakubali kwamba kila vyombo vya utekelezaji wa sheria vinapokabidhiwa teknolojia mpya, huwa vigumu kuvipokonya.

Kampuni za mawasiliano ya simu Italia, Ujerumani, na Austria zimekuwa zikikabidhi data kuhusu mienendo ya watu kwa maafisa wa afya.

HALI YA DHARURA

Bunge nchini Hungary, Machi 30 mwaka huu liliidhinisha sheria kadhaa za hali ya dharura zinazomwezesha Waziri Mkuu, Viktor Orbán, kutawala kwa amri yake mwenyewe.

Thailand, Machi 26 mwaka huu ilianza kutekeleza hali ya dharura inayoiruhusu serikali kusahihisha ripoti au taarifa ambazo inaamini si sahihi na inaruhusu wanahabari kufunguliwa mashtaka chini ya Sheria ya Uhalifu wa Kompyuta, ambayo adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano jela.

Post a Comment

0 Comments