LISHE BORA INAVYOSAIDIA KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA CORONA



📌RASULI KIDINDI

UGONJWA wa Corona kama ulivyo kwa magonjwa mengine ya kuambukiza una uhusiano mkubwa na lishe, kwani mtu anapopata maambukizi ya Corona huweza kupata dalili mbalimbali ikiwemo homa inayosababisha mwili kuwa na ongezeko la mahitaji ya virutubisho mbalimbali ikiwemo vitamini na madini mwilini.

Kwa kuwa maambukizi ya Corona husababisha homa inayoathiri hali ya lishe ya mgonjwa, umeng’enyaji dhaifu wa chakula na ufyonzwaji duni wa virutubisho katika tumbo la mgonjwa huongeza tatizo la mwili kushindwa kukidhi mahitaji yake ya virutubisho.

Dalili za ugonjwa wa corona ni joto mwilini, kikohozi kikavu na baada ya wiki moja kikohozi hicho, kinaweza kusababisha tatizo la kushindwa kupumua.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya duniani (WHO) kwa wagonjwa 56,000, ulibaini kuwa asilimia 80 ya wale walioambukizwa, hupata dalili zisizo kali kama vile za kukohoa, joto mwilini na mara nyingine homa ya mapafu, asilimia 14 hupatwa na dalili kali, kama vile tatizo la kupumua.

Utafiti huo unaeleza kuwa, asilimia sita ya wagonjwa hukumbwa na tatizo la mapafu kushindwa kufanya kazi na viungo vingine mwilini na hata kusababisha kifo.

Miongoni mwa dalili nyingi zilizoripotiwa na wagonjwa, asilimia 88 walidai kuwa na joto mwilini, asilimia 68 kikohozi kikavu na asilimia 38 waliripoti uchovu. Tatizo la kupumua liliwapata asilimia 19 ya wagonjwa, asilimia 13 waliripoti kuumwa na kichwa na asilimia nne waliripoti kuharisha.

Hivyo basi, kupambana dhidi ya maambukizi ya Corona hatua muhimu ni kuhakikisha mwenye maambukizi anapata nguvu (nishati lishe) ya kutosha kwa kuongeza ulaji, kuimarisha kingamwili kwa kula vyakula vyenye kuupatia mwili virutubisho muhimu ikiwemo protini, vitamini na madini kwa wingi.

Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Fatma Mwasola, anaeleza kwamba uwezo wa mwili kupambana dhidi ya maambukizi ya Corona unategemea hali ya afya na lishe ya mtu husika.

Mtu mwenye afya na lishe bora mwili wake unakuwa na uwezo mkubwa wa kupambana dhidi ya maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona. Hali nzuri ya lishe huimarisha kinga ya mwili na hivyo kumsaidia muathirika kupambana na virusi vya Corona, hivyo kupata athari kwa kiasi kidogo

Fatma Mwasola

Anasema mtu mwenye lishe duni huwa na kinga mwili dhaifu, hivyo apatapo maambukizi ya virusi vya Corona mwili huwa na uwezo mdogo wa kupambana, hivyo kupata madhara makubwa, kuchelewa kupona na kwa baadhi ya watu kupoteza maisha.

 

VIRUTUBISHO KAMA KINGA DHIDI YA CORONA

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo anasema kinga mwili huuwezesha mwili kukabiliana dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Coroba.

Fatma anabainisha kuwa mwili unapokuwa kinga ya kutosha, huweza kuzuia athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza kutokana na aina ya maambukizi husika.

“Uimarishaji wa kinga mwili unahitaji uwepo wa virutubisho mbalimbali ili mfumo wa kinga uweze kufanyakazi sawa. Virutubisho hivyo vinapatikana kutoka katika vyakula, hivyo ili tuweze kuimarisha kinga mwili tunapaswa kufuata taratibu sahihi za ulaji,” anasema.

Anavitaja vyakula muhimu vya kuzingatia kama sehemu ya kuupa mwili virutubisho kukabiliana dhidi ya magonjwa ya kuambukiza hususanI Corona ni ulaji wa vyakula vya asili ya nafaka, mizizi, na ndizi mbichi, nyama, jamii ya mikunde, mbogamboga na matunda.

Anasema vyakula vingine ni sukari, mafuta na asali, lakini vyakula hivyo vitumike kwa kiasi kidogo.

Mtaalamu huyo wa lishe anasema ulaji wa vyakula mchanganyiko utasaidia kupata virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika mwilini ikiwemo protini, madini na vitamini.

Fatma anabainisha kuwa protoni husaidia mwili kutengeneza chembe chembe au seli mpya na kukarabati seli za mwili zilizoharibika, kuimarisha mfumo wa kinga.

“Vitamini na madini husaidia katika kuongeza kinga ya mwili. Ili kupata vitamini na madini kwa wingi mgonjwa atahitajika kula kwa wingi vyakula mbalimbali hususani mbogamboga, matunda na vyakula vya asili ya wanyama.

“Mfano wa mbogamboga ni pamoja na kisamvu, mnavu, majani ya maboga, majani ya kunde, matembele, pilipili hoho, mchicha, maembe, papai, boga, na karoti,” anaeleza.

 

Mfano wa matunda ni pamoja na pera, chungwa, limau, chenza, ndimu, ubuyu, ukwaju, nanasi, stafeli, parachichi, machungwa, pasheni, rozella, zabibu, nyanya, , na mbilimbi, mabungo, na aina nyingine za matunda ya porini. Mfano wa vyakula vya asili ya wanyama ni pamoja na nyama, kuku, samaki, jibini, maziwa, maini, samaki. Vyakula vingine vyenye vitamin kwa wingi ni mafuta ya mawese, mahindi lishe na viazi lishe.

TIBA LISHE NIMRCAF

Wakati maambukizi ya Corona yalivyobisha hodi nchini, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadamu (NIMR), ilifanya utafiti kisha kuja na dawa yenye mchanganyiko wa vyakula lishe iliyopewa jina la NIMRCAF ambayo uitafiti wa awali ilionyesha kuleta mafanikio katika kubaliana dhidi ya maambukizi ya Corona.

Akielezea mchanganyiko huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Tiba Asili cha NIMR, Dk. Justine Omolo, anasema dawa hiyo ni fomula ya tiba lishe ambayo ina mchanganyiko wa pilipili kichaa, tangawizi, limao, kitunguu saumu, asali na maji.

Anasema dawa hiyo inasaidia kumpa nafuu mgonjwa wa corona, kwa kutibu dalili zinazotokana na ugonjwa huo.

Tayari imeshaonyesha matokeo chanya. Mchanganyiko wa tiba lishe hiyo sio dawa ya corona, lakini inasaidia kumpa nafuu mgonjwa wa corona kwa kuwa inatibu dalili zinazoambatana na ugonjwa huo

Dkt. Justine Omolo.

Anasema mpaka sasa tiba lishe hiyo, imeshaleta matokeo chanya kwa kuwa imesaidia wagonjwa wengi wa corona. Alisema kwa sasa mahitaji yamekuwa ni mengi, tofauti na awali.

“Mwanzo tulikuwa tukitengeneza chupa 1,000 na tumekuwa tukisambaza hospitali kwa wagonjwa kwa siku chupa 120 hadi 200, lakini sasa mahitaji yamekuwa makubwa na imeonyesha matokeo mazuri kwa wagonjwa,” anabainisha.          

Omolo anaeleza kwa mtu ambaye hana dalili, anapaswa kutumia dawa hiyo mara moja kwa siku na hiyo itamsaidia kujikinga na ugonjwa huo wa Corona.

NIMR iliibuka na dawa lishe hiyo, ikiwa tayari WHO imekwisha kutoa taarifa ikieleza kuwa inatambua na kuthamini mchango wa tiba asili kutoka Afrika na kusisitiza dawa hizo, zinapaswa kupewa nafasi sawa katika kufanyiwa majaribio, kama dawa kutoka maeneo mengine duniani.

 

 

Post a Comment

0 Comments