📌NA HAMIDA RAMADHANI.
KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na
Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, amekiri kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa
udahili wa fani za ufundi hali inayosababisha kushindwa kukidhi mahitaji katika
soko la ajira.
Aidha, ameliagiza Baraza la Taifa la elimu
ya ufundi (NACTE), kuendelea kuweka usimamizi mahiri ili kuhakikisha wanapata
watumishi wenye sifa stahiki na wanaokidhi mahitaji katika soko la ajira ndani
na nje ya nchi.
Dk. Akwilapo ametoa kauli hiyo jijini hapa
wakati akifungua kongamano la kitaifa la elimu ya ufundi lililoandaliwa na
NACTE
Amesema katika kukabiliana na changamoto
hiyo lengo la serikali ni kuhakikisha wanaongeza udahili na Mafunzo mengi yenye
ubora ili kutekeleza kikamilifu miongozo mbalimbali na fani zinazotolewa katika
vyuo vya kati.
Pia, amesisitiza kuwa serikali
itaendelea kutoa ushirikiano kwa Nacte kwenye vyuo vya serikali na taasisi
binafsi ili kuhakikisha utendaji wa kazi unakuwa imara.
Amewataka washiriki kutumia kongamano hilo
kama jukwaa la kutafakari wajibu wao katika utoaji wa elimu ya mafunzo ya
ufundi nchini kwa maendeleo endelevu.
"Nawataka mjadili na kufikia maamuzi
yanayotekelezeka, tulikubaliana kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo ya kufikia
katika ajenda ya nchi ya kujenga uchumi wa viwanda,"amesema
Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk
Adolf Rutayunga, amesema lengo la kongamano hilo ni kutoa fursa kwa wadau wa
elimu ya ufundi kujadili na kubaini njia bora za kuimarisha ushirikiano kati ya
vyuo vya mafunzo ya ufundi na wadau wengine.
Amesema mpaka sasa Baraza limesajili jumla
ya vyuo 418 ambapo kati ya hivyo vyuo 182 ni vya serikali na vyuo 236 ni vya
binafsi.
Dk. Rutayunga amefafanua kuwa vyuo hivyo
vinatoa fani mbalimbali ikiwemo fani ya afya na Sayansi shirikishi ambapo ni
vyuo 174, fani ya Biashara Mipango na Utalii vyuo 155 na fani ya Sayansi na
Teknolojia shirikishi vyuo 89.
Mwisho
0 Comments