📌Na DEVOTHA SONGORWA.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo amewataka wahitimu kutoka chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kuwa kielelezo cha kutunza na kuenzi amani ya Taifa la Tanzania.
Waziri Jafo ameyabainisha hayo Katika mahafali ya 34 katika chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini Kampus kuu ya Dodoma ambapo ameeleza kuwa amani ni tunu ya taifa, hivyo ni wajibu kwa kila mtanzania kutunza na kuenzi amani ya Tanzania.
“ Ni siku ya furaha sana kwetu wahitimu 4072 wa fani mbalimbali 24 kuhitimu lazima tujiulize Sisi wanazuoni wa chuo cha Mipango tuna nini cha kufanya,tuna input gani ya kufanya ili nchi yetu iweze kusonga mbele kwa mwendo tulionao na niwatake wote tulinde, tukaitangaze Amani yetu isingekuwa hivyo tusingekutana hapa leo hii iwe ajenda yetu kuu”,amesema Waziri Jafo.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo amewaasa wahitimu hao kuwa wabunifu zaidi Katika mipango ya maendeleo kwani elimu waliyoipata ikawe chachu ya mabadiliko huku akiahidi kushirikiana Katika kutatua changamoto za chuo hicho.
“Chuo cha Mipango kinawatengeneza wahitimu wake wanapo kwenda katika soko la ajira iwe kwa kuajirwa serikalini,sekta binafsi,au kujiajiri nendeni mkafanye kazi, msijikweze kuna mtu akipata tu Astashahada,Stashahada au Shahada anajikweza nendeni mkawe msaada kwa jamii na zile changamoto zenu za upungufu wa watumishi na miundombinu nimezisikia naahidi kufanya linalowezekaa tuzitatue”,ameeleza Waziri huyo.
Naye Mkuu wa chuo cha Mipango ya maendeleo vijijini Prof. Prof. Hozen Mayaya amesema Katika mwaka wa masomo 2018/2019 kumekuwa na ongezeko la udahili wa wanafunzi wapya kutoka wanafunzi 4,317 mwaka 2019/2020 hadi wanafunzi 5,856 ikiwa ni ongezeko asilimia 26.
Aidha, Prof. Mayaya ameendelea kufafanua kuwa chuo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kimeendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha hali maisha ya wananchi hasa vijijini ikiwa ni pamoja mradi wa kuboresha ustahimilivu wa jamii za wafugaji na wakulima wa Serengeti kwa ajili ya kupunguza migogoro ya Rasilimali za kiikolojia na nyingine zinazofanana na hizo(2019-2023).
“Miradi mingine ni mradi wa kuwajengea uwezo watumishi wa mamlaka za serikali za Mitaa za serikali ya mapinduzi Zanzibar(Agosti 2018-Julai 2021),mradi Wa kuwajengea uwezo watumishi wa wizara ya mamlaka za serikali za Mitaa Katika uandaaji mipango na bajeti inayozingatia mahitaji ya watoto (Agosti 2018-Julai 2021).
Ameendelea kutaja miradi ni pamoja na mradi wa kuandaa mipango mikakati Tanzania Bara (Julai 2020-2021)na mradi wa tathmini ya mbinu za upangaji wa mipango ya maendeleo na uhusishaji wa programu ya O&OD Katika mitaala ya vyuo vya elimu ya juu (2020-2021)”,ameeleza Prof.Mayaya.
Akisoma hotuba ya shukrani kwa niaba ya wahitimu wote Emedian Musa ametumia fursa hiyo kutoa kupongeza uongozi wa Chuo na Serikali kwa kusimamia vyema mpaka kuhitimu kwao akiwaomba kuendelea kuunga mkono wanafunzi wanaoendelea na masomo yao.
“Tunaishukuru sana Serikali na Chuo chetu kwa tusaidia kufika hapa kama wanafunzi tumepitia misuko suko mingi lakini tulijipa moyo na leo tunafurahia ushindi tunaahidi kuendeleza mema mliyotufundisha ili kukitangaza vyema Chuo chetu wakati wote tutakapokuwa katika shughuli zetu”,ameshukuru Mhitimu huyo.
0 Comments