📌Na Augusta Njoji.
Kangara, Choya, komoni na wanzuki ni pombe maarufu
za kienyeji zinazotengenezwa mkoani wa
Dodoma.
Baadhi ya pombe hizi hutengenezwa kwa kutumia nafaka
ya mtama, uwele na mahindi na huuzwa kwa bei rahisi ikilinganishwa na bia au
kinywaji kingine cha kiwandani.
Tabia kuu ya wanywaji wa pombe hizi ni kuchangia chombo kimoja zaidi ya watano hadi kumi jambo ambalo ni hatari kwa afya zao hasa maambukizo ya magonjwa ya mlipuko.
Kutokana na hali hiyo, uwepo wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya Corona(COVID-19), umebadili maisha yao kwa kuwa lazimisha kunywa kila mtu na kikombe chake.
Mbali na kunywa kwenye vyombo vyao, pia wauzaji wa pombe hizo wamebuni utaratibu wa kuwa na vidumu vya kuanzia lita moja hadi tano ambavyo hutumika kujaza na kuuza kulingana na uhitaji wa mteja ambapo lita moja ya pombe hiyo ni Sh. 500.
WATUMIAJI WANENA.
Fabiana Mazengo anasema ugonjwa huo umesaidia pombe
hizo kunyweka kwa ustaarabu ili kuepuka kupata maambukizi ya corona na magonjwa
mengine.
“Pombe hizi za kienyeji raha yake ni kupokezana chombo kimoja tukiwa kundi, ili iishe haraka na kuwekewa tena, sasa baada ya huu ugonjwa kuwepo tumebadili muundo wa maisha kwa kiasi kikubwa kwanza unanunua lita mbili ambazo ukinywa peke yako unatosheka na kuendelea na majukumu mengine,”anasema.
Anasema wakati wa Corona wanywaji wa pombe hizo
walikuwa wachache kwa hofu ya kuambukizana.
“Hii hofu ilipunguza idadi ya watu kunywa maana
tulibandikiwa masharti ya wataalam wa afya ambayo yalitulazimu wengine kununua
kwenda kunywa nyumbani jambo ambalo mtu anaona hapati raha kwa kuwa amezoea
kunywa kwa pamoja na wenzake,”anasema.
Naye, Mkazi wa Mpalanga, Job Mdolosi, anasema
wauzaji huwa na vikombe ambavyo huhifadhiwa kwenye ndoo ya maji safi kwa ajili
ya kuosha na kuhudumia watu.
“Wakati wa kunywa ni kila mtu na kikombe chake,
hatuchangii tena chombo maisha yetu yameendelea kuwa hivyo wakati wa Corona na
baada ya Corona,”anasema.
Maria Mcheela, anabainisha kuwa utaratibu unaotumika
ni kupewa pombe kidogo kwenye kikombe kwa ajili ya kuonja na baada ya kuipenda
ndipo muuzaji anaweka kwenye chombo kulingana na uhitaji wa mteja.
Kefa Jeremia, anasema wamezingatia maelekezo ya
wataalam kwa kutumia kila mtu kikombe chake na kunawa na maji safi na sabuni.
“Kwetu hatujawahi kupata matukio mengi ya ukatili
kwasababu ya pombe,”anasema.
WAUZAJI POMBE.
Muuzaji wa pombe Bihawana, Mariam Sijila, anasema wameongeza kwa kiasi kikubwa usafi ili kudhibiti maambukizi ya Corona kwa wanaotumia pombe hizo.
Anasema wakati wa Corona hakuna mlevi wa pombe ya kienyeji ambaye alikuwa hautambui ugonjwa huo, kutokana na kila moja kuchukua tahadhari zilizokuwa zimetolewa na Wizara ya Afya.“Mimi kwenye kilabu changu kila mlevi aliyekuwa
akiingia humu ndani sharti la kwanza lazima anawe maji ambayo nilikuwa nimeweka
hapo mlangoni,pia akiingia humu ndani alikuwa akikutana na tangazo lililokuwa
limeandikwa tahadhari zinazotakiwa kuchukuliwa kwa ajili ya kujilinda na
ugonjwa huo”anasema.
Naye, Mandeje Samsoni Muuzaji wa pombe hizo kijiji
cha Chidilo, anasema vyombo vinavyotumika vinachemshiwa maji ya moto ili kuua
vijidudu ambavyo vinaweza kusababisha ugonjwa wa Corona au magonjwa mengine ya
mlipuko.
MTAALAM WA AFYA AFUNGUKA.
Mratibu wa matibabu na njia za kuzuia maambukizo
magonjwa ya mlipuko kutoka Kitengo cha Dharura na Maafa, Wizara ya Afya,
Dk.Alex Sanga, anasema ugonjwa wa Corona unaambukizwa kwa njia ya maji maji,
hivyo kutochangia pombe itasaidia kuepuka baadhi ya magonjwa ya mlipuko.
“Maji maji haya aidha ni kutoka njia ya hewa ikiwemo
mdomoni, ndio maana tunashauri aidha kama ni chombo cha chakula au cha kunywa,
atumie chombo chake inasaidia kuepusha na magonjwa mengine,”anasema.
Dk. Sanga anaongeza kuwa “Afya zinaweza kutofautiana
mwingine akawa na midomo imepasuka au vidonda anatokwa damu, inaweza
kusababisha maambukizo pia ya magonjwa mengine.
Anafafanua kuwa ni vizuri kila mtu kutumia chombo
chake na si kwa wanaokunywa bali hata kwenye jamii kwenye masuala ya vyakula.
“Hii ni njia moja wapo ya kupunguza maambukizo
kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine, magonjwa ya mlipuko kwa mfano
Corona lakini pia kuna magonjwa mengine yanaambukizwa kwa maji maji,”anasema na
kuongesha:
“Utafiti unaonesha uwezekano ni mdogo lakini upo na
umetokea, kwa mfano kama mtu amepasuka mdomo unatoa damu akatumia chombo hicho
hicho kunywa pombe na kumpa mwenzake anaweza kupata magonjwa kama vile Ukimwi.”
Aidha, anasema Wizara ilitoa elimu na miongozo
mbalimbali ya kuzuia maambukizo ya Corona kwa watanzania ikiwemo watumiaji wa
pombe hizo.
MIONGOZO ILIVYOTOLEWA.
Afisa Afya Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya,
Innocent Swai, alisema Wizara hiyo ilitoa miongozo kwenye Halmashauri namna ya
kukabiliana na ugonjwa huo kwenye maeneo yao ikiwemo vilabu vya pombe na
minada.
“Tulitoa mwongozo wa namna ya kuzingatia kukaa kwa
umbali kwenye maeneo yote yenye mikusanyiko, kama ukienda hospitali utakuta
kuna alama hapa kaa hapa usikae,”anasema.
Anaeleza pia kuna miongozo ya watu kutofanya
mikusanyiko isiyo ya lazima na kutotumia vifaa jumuishi ikiwemo vyombo vya
kunywea pombe ambayo imesaidia kuondokana na magonjwa ya mlipuko.
“Pia mahali kwenye mikusanyiko kuwe na vifaa vya
kunawia mikono, tulitoa matangazo ya namna Corona inavyoambukizwa na namna ya
kujikinga, ufanye nini ukiwa na dalili,”anasema.
Mwisho.
0 Comments