📌MUSSA YUSUPH
MEI
mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Shirika la
Afya Duniani (WHO) na Mtandao wa Kimataifa kuhusu Chakula cha Mtoto (IBFAN),
yalitoa tafiti yakieleza dhana potofu kuhusu maziwa ya mama kwamba yanaweza
kusababisha maambukizi ya virusi vya Corona kwa mtoto.
Katika
utafiti huo, mashirika hayo yamehamaisha wakina mama waendelee kunyonyesha
mtoto, hata kama amethibitishwa kuwa na virusi vya Corona au anashukiwa kuwa
navyo.
Kupitia utafiti huo mashirika hayo yameeleza:
“Wakati watafiti wanaendelea kuchunguza maziwa kutoka kwa mama mwenye virusi
vya Corona au anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona, ushahidi wa sasa
unadokeza kuwa hakuna uwezekano wa virusi hivyo kuambukizwa kupitia unyonyesaji
au kwa kumpatia mtoto maziwa yaliyokamuliwa kutoka kwa mama mwenye virusi au
anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona.”
Hata
hivyo, Umoja wa Mataifa (UN) unaeleza kuwa uchunguzi kutoka mataifa 194,
umebaini kuwa ni nchi sita pekee ambazo zina mikakati ya kisheria kuhusiana na
kanuni ya kimataifa ya kutangaza maziwa mbadala ya mama.
Kanuni
hiyo inapiga marufuku aina zote za matangazo ya maziwa mbadala ya mama, ikiwemo
matangazo, zawadi kwa wahudumu wa afya na mgao wa bure wa sampuli za maziwa
hayo.
Akizungumzia
ripoti hiyo, Dkt. Francesco Branca, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Lishe na
Usalama wa Chakula kutoka WHO, amesema kuwa, “Mikakati mizito ya matangazo ya
maziwa ya unga kwa mtoto, hasa kupitia wataalam wa afya ya kwamba wazazi
waamini ushauri wa lishe na afya, ni pigo kubwa katika kuimarisha afya ya mtoto.”
WHO
na UNICEF wanapendekeza kuwa mtoto anyonye maziwa ya mama pekee kwa miezi 6 ya
mwanzo na baada ya hapo aendelee kunyonya hadi miaka miwili na zaidi huku
akipatiwa vyakula vingine vyenye lishe.
Mkuu
wa masuala ya lishe UNICEF, Dk. Victor Aguayo, amesema kuwa kadri janga la
COVID-19 linavyozidi kuenea, wahudumu wa afya wanaelekezwa maeneo ya kusaidia
kudhibiti janga hilo, huku suala la unyonyeshaji ambalo linaokoa maisha ya
mamilioni ya watoto, linakosa mwongozo wa kutosha.
Tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kila mama na kila familia inapata mwongozo unaotakiwa kutoka kwa wahudumu wa afya waliobobea ili waweze kunyonyesha watoto wao tangu wanapozaliwa.
HATUA ANAZOPASWA KUZINGATIA MAMA WENYE CORONA
Utafiti
huo wa UN, unaeleza kuwa mama aliyethibitishwa kuwa na virusi vya Corona au
anayeshukiwa kuwa na virusi hivyo, anaweza kuendelea kunyonyesha na kwamba anapaswa
kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia maji safi na sabuni au dawa za kutakasa
mikono kabla ya kumbeba au kumshika mtoto.
Pili
anapaswa avae barakoa ya kitabibu wakati akiwa amembeba au anamhudumia mtoto
ikiwemo wakati anamlisha.
Tatu,
apigie chafya au akoholee kwenye kitambaa kisha anawe mikono na nne, asafishe
eneo mara tu anapokuwa ameligusa.
Akizungumzia
kuhusu huduma za lishe kwa mama mjamzito na anayenyonyesha mwenye maambukizi ya
COVID -19, Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe
(TFNC), Fatma Mwasola, anasema kanuni za lishe ya mama
mjamzito na anayenyonyesha zifuatwe ikiwa ni pamoja na kula mlo kamili
unaotokana na vyakula mchanganyiko mara nne mpaka tano na asusa mara mbili kwa
siku.
Ili
kupata unasihi wa kunyonyesha, anasema msaada wa msingi wa kisaikolojia na
kijamii na msaada wa ulishaji unaostahili utolewe kwa akina mama wajawazito na
wenye watoto wachanga na wadogo, bila kujali wao au watoto wao wachanga na
wadogo wanahisiwa au wameambukizwa COVID-19.
Fatma
anaeleza pia, wakina mama hao muhimu wapatiwe huduma za kujikinga na athari za
COVID ili wasiambukizwe au wasiwaambukize wengine kwa kujitenga na mwingiliano
na kuchukua hatua nyingine zinazoweza kusambaza maambukizi.
Washauriwe kupata huduma za kliniki na kusaidiwa pale wanapokutwa na matatizo mbalimbali.
UMUHIMU WA UNYONYESHAJI WATOTO WAKATI WA CORONA
Ofisa
Mtafiti huyo wa masuala ya lishe anaeleza kuwa kunyonyesha mtoto huzuia vifo
pamoja na magonjwa mara baada ya mtoto kuzaliwa na wakati mtoto akiwa mchanga
na mdogo.
Anasema
matokeo ya kumkinga mtoto ni makubwa kupitia uimarishaji wa kingamwili moja kwa
moja toka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Hivyo,
anaeleza kuwa kanuni zinazoshauriwa katika ulishaji wa watoto wachanga
unaokubalika ni muhimu kuzingatiwa pamoja na kuchukua tahadhali za kuzuia
maambukizi ya COVID 19.
“Watoto
waliozaliwa na wanawake wenye maambukizi ya Corona walishwe kwa kuzingatia
mwongozo wa kitaifa wa ulishaji watoto wachanga na wadogo, na mama zao
wazingatie taratibu zinazopendekezwa za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
“Anza
kunyonyesha mtoto mapema katika kipindi cha ndani ya saa moja baada ya
kujifungua. Mnyonyeshe mtoto maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita
ya mwanzo na mtoto akitimiza umri wa miezi sita anza kumpa vyakula vya nyongeza
na endelea kumnyonyesha maziwa ya mama hadi atimize umri wa miaka miwili au
zaidi,” anabainisha.
Mtaalamu
huyo anaeleza kama inavyofanyika kwa watu walioambukizwa virusi vya Corona,
wanawake wanaonyonyesha wanaotekeleza taratibu ya kugusana na watoto wao
kimwili au ubebaji watoto kwa mtindo wa kangaroo, wanapaswa pia kuzingatia
taratibu za usafi wa mwili na kuzuia majimaji yanayotoka puani na kwenye mfumo
wa kupumua wakati wote wanapowanyonyesha watoto wao.
“Kwa
mfano wanapaswa kutumia vifaa vya kufunika pua na mdomo unapokuwa karibu na
mtoto, kunawa mikono mara kwa mara kabla na baada ya kumhudumia mtoto,
kusafisha na kutakasa maeneo yote ambayo mama mwenye maambukizi ameyagusa.
Anaongeza kuwa: “Wanawake wajawazito na wanawake wenye watoto wachanga na wadogo wapate ushauri nasaha kuhusu unyonyeshaji, ulishaji watoto na huduma za msaada wa kisaikolojia iwapo wao wenyewe au watoto wao wanahisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona.
Mtaalamu
huyo anaeleza: “Inapotokea kuwa mama mwenye maambukizi makali ya virusi vya
Corona au matatizo mengine ya kiafya yanayosababisha ashindwe kuendelea
kumnyonyesha mtoto wake, ashauriwe na asaidiwe kukamua maziwa yake, na kumlisha
mtoto maziwa hayo yaliyokamuliwa. Hayo yafanyike sanjari na kuzingatia taratibu
zinazoshauriwa za kudhibiti maambukizi.”
Fatma
anaeleza kuwa mama na mtoto wasaidiwe kugusana mwili, kubeba mtoto kwa mtindo
wa kangaroo, kukaa pamoja bila kutenganishwa mchana na usiku, hasa mara baada
ya mama kujifungua na siku za mwanzo wakati mama anapoanzisha unyonyeshaji,
bila kujali iwapo mama au mtoto anahisiwa au amethibitiishwa kuwa na maambukizi
ya virusi vya Corona.
Anaeleza kuwa wazazi na walezi wanaohitaji kujitenga au kutenganishwa na watoto wao, na watoto wanaohitaji kujitenga au kutenganishwa na wazazi au walezi wao, wanapashwa kupata huduma saidizi za kitaalamu kutoka kwa watoa huduma za afya, au watoa huduma wengine wa afya ya akili na msaada wa kisaikolojia
0 Comments