📌FAUSTINE GIMU.
Waziri wa
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Faustine Ndugulile amesema kuwa
serikali ipo katika Mchakato wa kuweka sera ya kuhakikisha makampuni ya
simu yanakuwa na mfumo wa uuzaji wa vocha kama ilivyo kwenye mfumo
wa uuzaji wa LUKU kwenye Umeme ili kuondoa malalamiko ya wananchi kuibiwa
vifurushi vyao na makampuni hayo
Dkt.Ndugulile
amebainisha hayo jijini Dodoma wakati akifanya mahojiano maalum
na mtandao huu kufuatia wananchi kutoka maeneo mbalimbali
nchini kutoa malalamiko kwa kampuni za simu juu ya vifurushi ama bando
walizojiunga kuisha mapema ikilinganishwa na kiasi cha fedha walizotumia
kujiunga.
“Malalamiko
yamekuwa mengi sana kwa wananchi kutokana na vifurushi kuisha kabla ya
wakati ikilinganishwa na fedha walizotumia kujiunga hivyo sisi kama
serikali tumeamua kuchukua hatua ili wananchi wanufaike na mawasiliano ya
simu ambapo kuna haja sasa kuwa na mfumo wa vifurushi kama ilivyo kwenye
LUKU za Umeme “alisema.
Aidha,Dkt.Ndugulile
amesema tayari ameshatoa maagizo kwa mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
[TCRA]kulifanyia Uchunguzi kwa Muda wa miezi mitatu pamoja na kuwa na mpango wa
kupeleka malalamiko Wizarani kila mwezi.
“Tumeagiza TCRA kwenda
kulifanyia uchunguzi suala hili kubainisha nini changamoto lakini pili
waje na mapendekezo kwa serikali na tuone namna ya kuyafanyia uchunguzi na
maagizo hayo tumetoa ndani ya miezi mitatu”alisema.
Hata
hivyo,Dkt.Ndugulile amebainisha kuwa hadi sasa zaidi ya simu kadi milioni 50
zimesajiliwa ,huku watanzania milioni 27 wanatumia internet na Watanzania
milioni 29 wakitumia miamala ya fedha kwa njia ya Simu.
“Mhe.Rais
alivyoanzisha hii wizara mpya alikuwa na makusudi yake ,moja ni kuongeza wigo
wa Matumizi ya TEHAMA kwa manufaa ya Watanzania,hivi tunavyoongea hadi
sasa zaidi ya simu kadi milioni 50 zimesajiliwa ,huku watanzania milioni 27
wanatumia internet na Watanzania milioni 29 wakitumia miamala ya fedha kwa njia
ya Simu”amesema.
Wakizungumza na
mtandao huu jijini Dodoma baadhi ya wananchi jijini Dodoma
wamesema kuishiwa virufurushi kabla ya matumizi limekuwa changamoto kubwa
katika maisha yao huku wakiipongeza serikali kupitia Wizara ya
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuanza kufuatilia malalamiko hayo
ya muda Mrefu.
Danson Mwaluko
ni miongoni mwa Wananchi waliopata fursa ya kuzungumza na Gazeti hili ambapo
alisema jambo hilo limekuwa ni kero kubwa kwani hurudisha nyuma uchumi.
"Kwa kweli siku
hizi changamoto mno ukijiunga bando la Tsh.1000 ndani ya Dk 15 au 7 linakata
tunashindwa tufanyaje"alisema Danson.
Tatizo la Wananchi
kulalamika vifurushi kukata mapema katika simu zao limekuwa la nchi nzima
ambapo serikali ya awamu ya tano imejipanga kutatua malalamiko hayo.
MWISHO.
0 Comments