(COSTECH) YATOA ZAIDI YA BILIONI 50 KUFADHILI MIRADI YA MAENDELEO.

 


📌Na Ramadhan Hassan.

TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imesema katika kipindi cha miaka 10 imeweza kutoa zaidi ya shilingi bilioni 50 kufadhili miradi ya utafiti na ubunifu mbalimbali  ambapo  zaidi ya miradi  100 imeishakamilika kwa asilimia 70 ambayo  imezidi kuwaongezea kipato watanzania.

Hayo yameelezwa Jijini hapa na Mratibu wa Mafunzo kutoka COSTECH,Merchades Rutechura  alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari.

COSTECH iliandaa mafunzo ya siku mbili   kwa  Waandishi wa Habari wa Mikoa ya Dodoma pamoja na watafiti     na kisha kwa siku mbili  waandishi wa habari walipata fursa ya  kutembelea   miradi mbambali pamoja na watafiti  katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo (Tari Makutupora),Taasisi ya Mifugo (Taliri Kongwa) na (Taliri Mpwapwa).

Merchades amesema kuanzia mwaka 2010 Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imetumia zaidi ya shilingi bilioni 50 kufadhili miradi ya utafiti na ubunifu.

“Katika kipindi hicho miradi zaidi 100 imeishafadhiliwa na katika hiyo asilimia 70 imeishakamilika na matokeo  yake yamepatikana.Pia tumefadhili ubunifu mbalimbali  pamoja na watafiti wachanga na tunafadhili tafiti kutoka katika Taasisi na Vyuo vikuu kwa sasa hivi tuna mashindano ya Kitaifa  yanayoitwa  Makisatu.

Akizungumzia ziara amesema  sehemu nyingi walizotembelea wamegundua kuna mbegu nyingi za wanyama ambazo zinatakiwa kuwafikia wananchi ambapo amedai kwamba hiyo ni kazi ya waandishi wa habari kuhakikisha zinafika katika jamii ili iweze kutambua.

“Matokeo ya utafiti yanatija kubwa sana kwa jamii kwa mfano baadhi ya sehemu tulizotembelea tumegundua kwamba kuna mbegu nyingi  za wanyama kama vile mbuzi na ng’ombe ambazo zipo katika Vyuo vya utafiti na zinatakiwa kuwafikia wananchi.

“Lakini pia tumegundua kuna teknolojia ya malisho ya ngombe na wanyama wengine ambayo ikisambaza kwa wananchi lile tatizo la uhaba wa malisho katika kipindi cha ukame linaweza kumalizwa.

“Lakini tumeona baadhi ya matokeo kama ufugaji wa kuku na namna ya kumpima kuku kama unataka kumuuza muuzaji asiweze kudhulumiwa,”amesema.

Amesema lengo la COSTECH ni   matokeo hayo yaweze  kusaidia katika uchumi wa Taifa na kila kinachofanyika katika Taasisi na Vyuo vikuu kiweze  kuwafikia wananchi.

“Lengo kuu la matokeo haya tunataka yasaidie katika uchumi wa Taifa kwa sababu kila tunachofanya katika chuo cha utafiti tungependa kiwafikie wananchi na tunatumia fedha nyingi za Serikali ili zisaidie hizi teknolojia na kurahisisha maisha ya mtanzania,” 
amesema.

Pia,amewataka watafiti kuweka wazi kazi zao ili waandishi waweze kuwafikia na kuzipeleka katika jamii.

“Wajitahidi kuweka mazingira rafiki  hata mwandishi wa habari akikufikia aweze kukipata kile ambacho anakihitaji,”amesema.

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mafunzo kwa waandishi wa habari na watafiti ambayo yanafanyika nchi nzima ili kusaidia kufikia malengo kufanyika kwa tafiti mbalimbali zinazofanyika nchi nzima kwenye vituo na Taasisi mbalimbali.

Amesema kuwa toka mafunzo hayo yaanze kwenye kanda mbalimbali kumekuwa na ongezeko kubwa la Makala,vipindi na habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu na hivyo kusaidia jamii kujua ni wapi wanaweza kuzipata ili kuzitumia kwenye shughuli zao mbalimbali za uzalishaji na kuongeza tija.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments