📌DEVOTA SONGORWA
APRILI mwaka huu, Benki ya Dunia
(WB) ilitahadharisha kuhusu uchumi wa Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara,
kuporomoka kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu miaka 25
iliyopita,kutokana na virusi vya Corona, bara hilo pia limeonywa vifo vya
malaria kuongezeka mara mbili zaidi.
Shirika la Afya Duniani (WHO)
linasema idadi ya vifo vinavyosababishwa na Malaria katika nchi za Afrika
zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara inaweza kuongezeka hadi kufikia 769,000
mwaka huu, iwapo nguvu zote zitaelekezwa katika mapambano ya virusi vya corona
(COVID-19).
Inaelezwa kuwa Afrika inaweza
kujikuta njia panda zaidi kupambana na magonjwa mengine kutokana na kuelemewa
na kasi ya maambukizi ya virusi vya corona ambapo hadi sasa imethibitisha kesi
zaidi ya 25,000 za virusi hivyo huku vifo vikipindukia 1200.
Kwa sasa serikali kwa
kushirikiana na WHO, zimejielekeza zaidi kwenye kupambana na janga la corona.
Mkurugenzi Mkazi kanda ya Afrika
Dkt. Matshidiso Moeti mapema wiki hii alitoa wito kwa nchi zote za kiafrika
kuhakikisha kwamba juhudi za kupambana na Malaria zinaendelea.
Uchambuzi wa hivi karibuni ulibaini kwamba vyandarua vilivyowekwa dawa vimeachwa kusambazwa na udhibiti wa kesi umepungua, vifo vya malaria katika nchi za Afrika kusini mwa Sahara vinaweza kuongezeka mara mbili ukilinganisha na mwaka 2018
“Hii itakuwa idadi kubwa ya vifo
kuwahi kushuhudiwa katika ukanda huo tangu mwaka 2000”, ameongeza mkurugenzi
huyo.
Pia aligusia juu ya takwimu za
mripuko wa kirusi cha Ebola barani Afrika, na kuonyesha kwamba watu walikufa
kutokana na maradhi mengine, ikiwemo malaria, kuliko hata Ebola yenyewe,
kutokana na ukosefu wa upatikanaji matibabu.
Mwaka 2018, kulikuwa na visa
milioni 213 vya malaria na vifo 360,000 vinavyohusiana na ugonjwa huo katika
kanda ya Afrika, ikiwa ni asilimia 90 ya kesi zote duniani.
WHO imesema kama lengo la
kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya corona itachangia kupungua kwa
upatikanaji wa dawa za kupambana na malaria, vifo vitaongezeka mara mbili.
“Nchi katika ukanda mzima zina
nafasi ndogo na fursa ya kupunguza uingiliaji katika udhibiti wa malaria,
matibabu na kuokoa maisha katika kipindi hiki cha mripuko wa COVID-19”, ilisema
taarifa ya WHO.
Benin, Jamhuri ya kidemokrasia ya
Congo, Sierra Leone na Chad zote zilianzisha programu za kupambana na malaria
kipindi hiki cha mripuko wa corona.
WHO inasema nchi hizo zinapaswa
kuwa mfano kwa mataifa mengine ya Afrika.
Wakati corona ikitishia mapambano
ya magonjwa mengine pia inatishia hali ya uchumi.
Mripuko wa virusi hivyo unaozidi
kusambaa na utabiri wa benki ya dunia ni kwamba unatarajiwa kuzisukuma nchi
za
Afrika, Kusini mwa Jangwa la
sahara katika mporomoko wa kiuchumi katika mwaka huu wa 2020 kwa mara ya kwanza
katika kipindi cha miaka 25.
Ripoti ya benki ya dunia kuhusu
hali ya kiuchumi barani Afrika imesema kwamba uchumi wa bara hilo utashuka
asilimia 2.1 na kufikia asilimia 5.1 kutoka kiwango cha ukuaji cha mwaka jana
cha asilimia 2.4.
Aidha mripuko huu wa virusi vya
Corona utazigharimu nchi za ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika
dola bilioni 37 hadi dola bilioni 79 ambayo ni hasara itakayoonekana mwaka huu
kufuatia kuvurugwa kwa shughuli nyingi za kibiashara na kiuchumi miongoni mwa
sababu nyinginezo.
Makamu mwenyekiti wa benki ya
dunia kwa upande wa Afrika, Hafez Ghanem amesema janga la ugonjwa wa Covid-19
linapima uwezo wa mwisho wa jamii na nchi zote ulimwenguni na kuna uwezekano
hususani kwa nchi za Afrika kuathirika zaidi.
Benki ya dunia na shirika la
fedha la kimataifa IMF zinakwenda mbio kutoa fedha za dharura kwa nchi za
Afrika na nyinginezo kukabiliana na virusi vya Corona ili kupunguza athari
zitakazosababishwa na hatua za kufungwa kwa shughuli za kimaisha
zinazochukuliwa nchi mbali mbali ulimwenguni kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo
vya Corona.
Ikumbukwe kwamba janga la virusi
vya Corona limesababisha kufutwa kwa safari za kimataifa katika nchi nyingi za
bara hilo la Afrika hali ambayo
imeathiri kwa kiwango
kikubwa sana sekta mbali mbali kama vile sekta ya utalii, uwekezaji na
biashara.
Serikali mbali mbali za bara la
Afrika zimetangaza hatua ya kufunga miji au nchi kwa maana ya kwamba hakuna
shughuli za kawaida za kimaisha haziruhusiwi tena kufanyika au baadhi ya nchi
zimetangaza kuzuia watu kutoka nje, na zile ambazo zimeruhusu raia wake
wamekuwa waoga na hata wengine kulazimika kufunga biashara zao.
Kwa mujibu wa WHO licha ya virusi
hivyo kuchelewa kuingia barani Afrika sasa inaonekana kuanza kusambaa kwa kasi.
Kutokana na hali hiyo benki ya
dunia inasema ukuaji wa pato la ndani utapungua kwa kiwango kikubwa na hasa
katika nchi tatu zenye uchumi mkubwa katika bara la Afrika ambazo ni
Nigeria,Angola na Afrika Kusini.
Kadhalika nchi zinazouza mafuta
pia zitaathirika sana.
Wakati Afrika ikisubiri ahueni na
misaada, Marekani taifa tajiri imechukua hatua ya kupunguza makali
yaliyosababishwa na virusi vya corona.
Ikiwa inaongoza kwa maambukizi ya
virusi vya corona duniani huku raia wake wakipoteza ajira kwa kiwango kikubwa
imeamua kuidhinisha karibu dola nusu bilioni katika mpango mpya wa kuuokoa
uchumi.
Wakati ulimwengu ukipambana na
kutafuta mbinu za kuuokoa uchumi unaoathirika kwa janga la virusi vya corona
Baraza la Wawakilishi Marekani lilipitisha mswada mpya wa kichocheo cha uchumi
wa dola bilioni 483.
Hatua hiyo imekuja wakati kiwango
cha ukosefu wa ajira kutokana virusi vya corona kikipanda na kampuni zikihitaji
msaada zaidi.
Mpango huo unaongeza kwa ule wa
dola trilioni 2.2 ulioidhinishwa mwishoni mwa Machi mwaka huu.
Karibu watu 50,000 wamefariki
dunia Marekani kutokana na virusi vya corona, huku idadi ya walioambukizwa
ikifikia zaidi ya 866,646.
Spika wa bunge Nancy Pelosi
amesema mpango huo ni muhimu kwa kuzilinda familia za Marekani na kuhakikisha
kuwa kampuni ndogo ndogo zina rasilimali zinazohitaji.
“Dola bilioni 60 zitatengwa kwa
ajili ya wanawake na jamii za walio wachache, maveterani, wamarekani asili,
wanaoishi vijijini na watu ambao hawakuwa na fedha kwenye benki lakini wana
mahitaji makubwa ya mikopo.
Bilioni 60 nyingine ni mikopo na ruzuku kwa biashara ndogondogo. Na kisha dola bilioni 100 kwa mahospitali na upimaji.
Bara la Ulaya, ambalo ndilo
lililoathirika zaidi na vifo 110,000, viongozi wa Umoja wa Ulaya waliipa
Halmashauri Kuu ya umoja huo jukumu la kutayarisha mpango wa kuufufua uchumi
kwa ajili ya mporomoko unaotarajiwa, baada ya mazungumzo yaliyosifiwa kupiga
hatua moja mbele, japokuwa wengine wameonya kuwa mazungumzo magumu bado
yanakuja.
Aidha wameidhinisha mpango wa
awali wa kipindi kifupi wa euro bilioni 540 na wakautaka mpango huo kuanza
kufanya kazi mwanzoni mwa Juni.
Ugonjwa huo unaonekana kuongezeka
barani Ulaya na Marekani, mataifa mengine yangali katika hatua za mapema za
vita hivyo ambavyo mpaka sasa vimewauwa zaidi ya watu 190,000 na kuwaambukiza watu
zaidi ya milioni 2.7 kote duniani.
WHO limeonya kuwa hatua kali
zinapaswa kuendelea kutekelezwa hadi pale tiba mwafaka au chanjo
vitakapopatikana.
Juhudi zinaendelea kote duniani,
huku Chuo Kikuu cha Oxford kikizindua majaribio ya chanjo kwa binaadamu.
Ujerumani imetangaza kuwa
majaribio ya aina hiyo yataanza wiki ijayo.
Katika Ikulu ya Marekani,
wanasayansi wamesema wamegundua kuwa kirusi hicho kinaharibiwa haraka na miale
ya jua, na kutoa matumaini kuwa janga hilo litapungua wakati msimu wa joto
ukianza.
Baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza
kuondoa taratibu vizuizi vya kupambana na virusi vya corona, lakini marufuku
dhidi ya mikusanyiko mikubwa imeongezwa.
Migahawa, mabaa na matukio ya
michezo bado vimefungwa.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril
Ramaphosa ametangaza kuwa serikali itaanza kuondoa vizuizi vilivyowekwa kuanzia
Mei mosi. Ramaphosa
amesema utaratibu huo
utafanywa kwa umakini na tahadhari kubwa.
Watu milioni 58 nchini Afrika Kusini wamefungiwa majumbani mwao kwa wiki tano, isipokuwa tu kama unataka kununua chakula au dawa. Nchi hiyo imerekodi visa zaidi ya 3,953 vya maambukizi na vifo zaidi ya 75
0 Comments