Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wameagizwa kuhakikisha wanasimamia ipasavyo upimaji wa maeneo ya viwanja vya shule zote nchini na yapatiwe hati miliki.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo ambaye amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia Idara ya Elimu, kusimamia.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo leo alipozungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 15 wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) unaofanyika jijini hapa.
Amesisitiza kwamba atafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa agizo hilo na Wakurugenzi watapimwa utendaji kazi wao kwa utekelezaji watakaofanya.
“Wataalamu wapo kwako, wapimaji wapo kwako, lakini unakuta shule haina hati miliki, hili ni jambo la aibu, mwaka 2021 ni wa upimaji wa maeneo yote ya taasisi za shule zetu zote ndani.
“Ni agizo kwa wakurugenzi wote wa halmashauri na eneo la upimaji utendaji kazi wenu, ni jinsi gani mkurugenzi amesimamia maeneo ya serikali yaweze kupimwa na kupata hati miliki,hili jambo tuseme limefika mwisho na halina mzaha,” amesisitiza.
Awali, Waziri Jafo ametumia jukwaa hilo kueleza mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya elimu katika utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.
Amesema ndani ya kipindi hicho sekta ya elimu imepiga hatua kubwa ikiwamo utoaji wa fedha za elimu bila malipo kutoka Sh. bilioni 20.8 hadi kufikia Sh. bilioni 24.
“Tumeweza kukarabati jumla ya shule kongwe 86 za Serikali hadi sasa, ufaulu wa wanafunzi kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 67.91 mwaka 2015 hadi asilimia 79.41 mwaka 2019,” amebainisha.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2020/21 Serikali imekusudia kuhakikisha shule zake zote zinajengewa maabara ili kuwezesha wanafunzi kufanya majaribio ya kisayansi na hilo linakwenda sambamba na kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya sayansi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel na mratibu wa mkutano huo, amesema kimekuwa kikao chenye mafanikio.
“Tumeweza kuwakutanisha wakuu wote wa shule za sekondari nchini ambao kwa pamoja wametoa maoni, wanashauri yatakayosaidia kuboresha sekta ya elimu.
“Tuliona kuna malalamiko mbalimbali, wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita, wanapotaka kujiunga na elimu ya juu, au wa kidato cha nne wanapotaka kujiunga na program za nacte huwa wanashindwa kuelewa baadhi ya taratibu.
“Katika kikao hiki wapo Nacte, Bodi ya Mikopo na taasisi nyingine za elimu ambapo wanawaelewesha walimu wakuu nao wakirudi kule watakwenda kusaidia wanafunzi wao,” amesema.
Amesema Taasisi ya Elimu Tanzania nao ni miongoni mwa wadau waliohudhuria kikao hicho, vile vile wamepata huduma ya uchunguzi wa afya dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Katibu Mtendaji wa Nacte Dk, Adolf Rutayuga amesema wameshirika katika mkutano huo kutokana wateja wao wakuu kutoka katika shule za sekondari hivyo watakuwa na fursa ya kukutana na wakuu wa shule pamoja na wadau wengine wa elimu.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Global Education Link Abdulmalik Mollel, ambao ndiyo waratibu wa mkutano huo, alisema kuwa umekuwa na mabadiliko makubwa tofauti na miaka iliyopita.
Amesema, katika mkutano wa mwaka huu wamezialika Taasisi mbalimbali za elimu ili wakuu wa shule za sokondari wapate elimu ambayo wataifikisha kwa wanafunzi wao ikiwemo namna ya kufanya udahili kujiunga na vyuo vikuu.
0 Comments