📌NA HAMIDA RAMADHANI
BAADA ya uchaguzi mkuu kumalizika, Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) limewaomba viongozi wa dini mbalimbali na Watanzania kwa ujumla kuwa wafariji kwa kuwoambea wote walioshindwa katika uchaguzi huo ili kuondokana na machungu waliyonayo.
Askofu mkuu wa TAG Dk Barnabas Mtokambali amesema hayo jijini hapa wakati akizungumza kwenye mahamali ya 38 ya chuo cha Biblia Kanda ya Kati (CBC) na kusema baada ya matokeo kutangazwa na wao kutofanikiwa kushinda ni dhahiri kuwa wapo kwenye kipindi kigumu.
Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba 28,2020 kwa ajili ya kuwachagua madiwani wangunge na Rais ambapo Rais John Magufuli alichaguliwa kuwa Rais na kuapishwa Novemba 5,2020 ili kuwatumikia Watanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Dk Mtokambali ambaye pia ni Rais wa makanisa ya TAG Barani Afrika, amesema kila mtu anawajibu wa kuwaombea ili Mungu aondoe maumivu na uchungu waliyonayo ambayo yalisababishwa na uwekezaji wa nguvu na mwili waliyokuwa wameufanya katika uchaguzi mkuu.
“Kibinadamu tunajua kuwa wapo kwenye kipindi kigumu ambacho kinaweza kusababisha kukata tamaa, kuwepo kwa mkanganyiko wa mambo yao yanayoweza kuathiri haki zake za msingi. Tuna wajibu wa kuwoambea ili wasikate tamaa ya kugombea awamu nyingine zijazo,” alisema Dk Mtokambali.
Hata hivyo aliwataka viongozi hao wa dini waliohitimu kumpa Mungu nafasi ya kwanza katika utendaji kazi wao, kuweka bidii katika kutimiza uhodari wa kuwatumikia Watanzania kiroho.
Amesema wanatakiwa kuwa na maono makubwa kufikisha huduma hadi vijijini, kutembea katika sheria na kanuni za kanisa ikiwa ni pamoja na kuwatii viongozi wao.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Jonas Mkoba alisema hawatarajii kusikia malalamiko yanayohusu wahitimu hao kuhusu utendaji kazi wao, badala yake wafanye kazi wakiwa na ari waliyotoka nayo chuoni.
Mkoba alisema wahitimu hao 110 wamesomeshwa kwa ufadhili wa kanisa hilo huku akiwaomba wadau wengine kijitokeza ili kusaidia uenezaji wa neno la Mungu kupitia watumishi wanaosomeshwa katika chuo hicho.
Wahitimu hao 110 wa
elimu ya biblia ni wa ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada ya
uzamili.
0 Comments