SERIKALI KUANZA MCHAKATO BIMA YA AFYA KWA WOTE

 


📌HAMIDA RAMADHANI

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jimii Jinsia Wazee na Watoto inatarajia kuanza mchakato wa kutafuta namna ya kutoa Bima ya Afya kwa Wananchi wote jambo ambalo litasaidi kupata huduma kwa haraka.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Prof. Mabula Nchemba alipokuwa akifungua Mkutano wa mwaka wa kutathmini utekelezaji katika sekta ya Afya uliofanyika jana Jijini hapa.

Suala la bima la Afya kwa Wananchi wote inawezekana lakini lazima jamii ishirikishwe kuanzia ngazi ya chini kwa kukusanywa maoni ya Wananchi kuhusiana na suala hilo’’, amesema Katibu Mkuu huyo.

Aidha Prof. Nchemba amesema wakati wanaendelea na mchakato huo lazima ijulikane wananchi  watachangia kiasi gani ili kufanikisha mpango huo ambao utawahusu wananchi wote.

‘’Hakuna huduma ya Afya ya bure ni lazima kila mmoja achangie hata kama ni kidogokidogo, hivyo machakato huo utakapomalizika  watu watafahamishwa'', amesema Prof. Nchemba.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (Tamisemi) Dkt. Doroth Gwajima amesema suala la Bima ya Afya kwa wote ni suala la kisera hivyo ili liweze kufanikiwa inatakiwa utungaji wa sera mpya.

‘’Mchakato huo ukianza utaanza katika utungaji wa sera kwanza alafu utaratibu mwingine utafanyika ili kukamilisha huduma hiyo ambayo Watanzania wengi wanasubiria kwa hamu’’, amesema Dkt. Gwajima.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo alisema katika Serikali ya awamu ya Tano katika kipindi cha kwanza walifanya mambo mengi mazuri katika sekta ya Afya ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Wilaya na kuwepo vifaa tiba  vya kisasa lakini kipindi hiki cha pili wanatarajia kufanya makubwa zaidi.

‘’Serikali imejenga miundombinu ya kisasa katika sekta ya Afya pamoja na uboreshwaji wa vituo vya Afya, lakini katika kipindi hiki cha pili tutaenda kwa kasi kubwa’’ amesema Dkt. Gwajima amesema.

Dkt. Gwajima amesema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli imeweza kufanya maboresho makubwa katika  sekta ya Afya, hivyo kikao hicho kitaangalia mafaniko yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizopo ili ziweze kutatuliwa.

Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa wa Dodoma Alphonce Chandika alisema kuwa kikao  hicho kitatumika kutoa mawazo chanya yatakayo nufaisha Wananchi wote kwa kuwashirikisha moja kwa moja ili kuleta matokeo makubwa katika jamii.

‘’Sisi lengo letu ni kumuhudumia mwananchi siyo kwa kuangalia ugonjwa mmoja tu, bali tutachunguza kwa undani  zaidi ili tuweze kujua magonjwa mengine kwani ili tufikie uchumi wa juu tunatakiwa tuwe ma Afya njema’’, amesema Chandika.

 

Post a Comment

0 Comments