📌NA DOTTO KWILASA
Akizungumza na
Waandishi wa Habari jana Jijini hapa,Mganga Mkuu wa Serikali,Profesa Abel
Makubi alisema kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha kuna uwezekano mkubwa
kuibuka kwa magonjwa ya milipuko kama kuhara damu,Kipindupindu na
yale yanayoenezwa na Mbu ambayo ni Malaria na Dengue.
Kutokana na
hayo,amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuendelea kushirikiana
kwa karibu na viongozi wengine wa Serikali za Mitaa, wananchi na wadau
mbalimbali ili kuhakikisha kila eneo haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa
ya milipuko.
Tumeshuhudia kuanza kujitokeza kwa uharibifu wa miundombinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka ambapo hali hii itahatarisha afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko
Licha ya hayo Mganga
Mkuu huyo alizitaja kanuni na taratibu za kiafya zinazotakiwa kufuatwa na
wananchi ni pamoja na kuchemsha maji ya kunywa,kuepuka kula chakula
kilichopoa,au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama.
Prof.Makubi alizitaja
kanuni zingine ni kutumia ipasavyo vyoo na kunawa mikono kwa maji safi na maji
tiririka na sabuni kabla ya kula,baada ya kutoka chooni,baada ya kumnawisha
mtoto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia mgonjwa.
Kanuni nyingine
ni kuosha matunda na maji safi kabla ya kula,kuongeza usimamizi wa usafi
wa jumla na mikono katika maeneo ya mikusanyiko kama shuleni,vyuoni na
masokoni.
Pamoja na mambo
mengine Mganga Mkuu huyo wa Serikali alizitaja sababu zingine ni kutotapisha
vyoo,kujikinga kuumwa na mbu pamoja na kutumia vyandarua,kusimamia hali ya
usafi katika mifumo ya maji safi,maji taka na mitaro.
“Kwa hiyo nawaomba
sana waganga wetu wa wilaya wachukue tahadhari katika hili mtafute namna
ya kuweza kushirikiana na mamlaka ndani ya kila eneo ili kuzuia
maambukizi,amesema na kupongeza;
Wizara tutaendelea kuwakumbusha tiba ni bora kuliko kinga.
Katika hatua nyingine
Prof.Makubi aliitaka jamii kuendelea kumuenzi baba wa Taifa Julius Nyerere kwa
kuendeleza juhudi na mafanikio katika kudhibiti magonjwa kwa kuwa alikuwa
mstari wa mbele kusimamia kupingana na maadui watatu ikiwemo maradhi.
0 Comments