WANAHABARI ‘KUVALIA NJUGA’ HABARI ZA VIJIJINI

 


📌NA EDITHA MAJURA

WANAHABARI kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania, wamekutana jijini Dodoma  kuanzisha Chama Cha Waandishi wa Habari za Vijijini (RUJAT).

'Mbeba maono' ya uanzishwa wa chama hicho, Prosper Kwigize ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Radio za Kijamii nchini (TADIO) amesema lengo kuu la kuanzishwa chama hicho ni kuweka mfumo wa kuratibu habari za vijijini ili kuzipa nafasi katika vyombo vya habari nchini.

Akizungumza na blog hii baada ya kikao kazi hicho,Kwigize amesema kupitia RUJAT  waandishi  wataweza timiza majukumu yao ya kuhabarisha kwa weledi habari kutoka vijijini kutokana mfumo wa kujengeana uwezo utakaoanzishwa ndani ya chama hicho.

Tunatambua kuwa waandishi wengi wa vijijini wanachangamoto nyingi hali inayowafanya waandishi hao kuendelea kuwa duni kiuchumi na hata kitaaluma hivyo kupitia umoja huu tutatatua changamoto hizo kwa pamoja

Prosper Kwigize

Kwigize amesema katika ukanda wa Afrika Mashariki nchi za Uganda,Kenya,Burundi,pia Ghana na Ethiopia huku India na Australia wakitajwa kama vinara wa kuandika habari za vijijni,hivyo Tanzania itaingia kwenye kundi la nchi hizo zinatoa kipaumbele kwa habari kutoka kijijini ambazo mara nyingi hazipewi nafasi katika vyombo vya habari.

Mkutano huo umejumuisha  wawakilishi wa kanda sita(6) nchini waliohudhuria mkutano huo maalum, wamepewa hadhi ya kuwa wanachama waanzilishi wa RUJAT.

Naona fahari kwamba wajumbe 14 kutoka mikoa mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wote wamejigharamia kuja Dodoma,hivyo hiyo ni dalili njema kwamba Waandishi wa Habari wana kiu kuwa na chombo kama hiki.

Prosper Kwigize

Pamoja na kupitia vipengele vya Katiba pendekezwa na kuipitisha kwa asilimia 100 ya kura, wanachama hao wamefanya uchaguzi wa viongozi wa muda.

Majina ya viongozi wakuu waliochaguliwa na nyadhifa zao katika mabano ni Prosper Kwigize (Mwenyekiti), Zania Miraj (Makamu Mwenyekiti), Neville Meena (Katibu) na Editha Majura (Muweka hazina).

Wengine waliochaguliwa ni Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji, ambao majina na kanda wanazowakilisha katika mabano ni kama ifuatavyo;

John Kasembe (Kanda ya Pwani), Amina Mrisho (Kanda ya Kati), William Bundala (Kanda ya Ziwa), Meshark Ngumba (Kanda ya Magharibi), Gasper Mushi (Kanda ya Kaskazini) na Sabina Martin (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini).

Uongozi huo umeanza kazi mara moja ikiwamo kufanikisha usajili wa chama hicho, kabla ya kufanyika mkutano mwingine mkuu utakaochagua viongozi rasmi wa RUJAT.

 

 

Post a Comment

0 Comments