📌NA DOTTO KWILASA
MENEJIMENTI ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma
imemuagiza Mkandarasi kampuni ya Mohammedi Builders anayejenga mradi wa jengo
la kitegauchumi ‘Government City Complex’ kukamilisha na kukabidhi mradi huo
ifikapo 30 Disemba, 2020.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipoongoza timu yake ya menejimenti kutembelea
na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kitegauchumi wa jiji ‘Government
City Complex’ katika mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini hapa.
Mafuru amesema “nimekuja na timu ya Menejimenti
ninayoiongoza hapa kumsimamia na kumkumbusha mkandarasi anayejenga mradi huu
kuwa kwa mujibu wa mkataba wetu, mradi huu unatakiwa kuisha tarehe 30 Disemba,
2020 na bahati nzuri yeye anasema hana tatizo na kukamilisha mradi huu tarehe
hiyo”.
Mkurugenzi Mafuru amesema kuwa mradi huo umejengwa
katika mji wa Serikali yalipo makao makuu ya Serikali eneo la Mtumba ili
kuwezesha kutoa huduma katika eneo hilo la Mtumba. “Lengo la mradi huu ni
kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati yeye anapambana kujenga ofisi za Serikali hapa Mtumba, sisi kama Jiji
tunapambana kuhakikisha huduma ambazo zitakosekana kwenye maeneo mengine
zinapatikana katika jengo hili. Jengo hili lina awamu nne.
Hii ni awamu ya kwanza ambayo tumekuja kuishuhudia ikiwa inaelekea ukingoni, nimetaarifiwa kuwa awamu hii ujenzi wake umefikia asilimia 60
Joseph Mafuru.
Licha ya hayo Mkurugenzi huyo anawaalika
wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza kutembelea mradi huo na kuweka miradi
ya kupanga katika jengo hilo.
“Mradi huu utakuwa na maeneo ya biashara,
‘apartments’, maduka makubwa ya biashara, sehemu za taasisi za kifedha. Lakini
pembeni tunajenga ukumbi mkubwa wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 500
ili kurahisisha shughuli zote za Serikali kufanyika katika eneo hili.
Eneo hili la
mji wa Serikali litakuwa na wageni wengi ambao watakaokuwa wakihitaji huduma za
Serikali, mabalozi, wawekezaji na watumishi mbalimbali kutoka ndani na nje ya
nchi” anasema Mafuru.
Mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Jiji la
Dodoma ulibuniwa na timu ya menejimenti na kupitishwa katika vikao vyake vya
kisheria ili utekelezwe na kuiwezesha Halmashauri kuongeza wigo wa mapato ya
ndani. Mradi huo, awamu ya kwanza itagharimu shilingi bilioni 18.
Kwa upande wake, Mhandisi Merinyo amemuhakikishia
Mkurugenzi wa Jiji kuwa mradi huo utakabidhiwa ifikapo tarehe 30 Disemba, 2020.
Amesema kuwa katika kufanikisha kukamilika kwa mradi
huo, ujenzi utafanyika usiku na mchana ili kuharakisha mradi huo.
0 Comments