📌FAUSTINE GIMU GALAFONI
WANANCHI katika maeneo
mbalimbali jijini Dodoma wamesema kuwa magonjwa ya Mlipuko mara nyingi
husababishwa na tabia za binadamu zikiwemo utiririshaji wa maji machafu
kutoka chooni na kuyaacha yakitapakaa barabarani.
Wakizungumza na CPC
Blog jijini Dodoma baadhi ya wananchi hao wamesema kuwa mara nyingi tabia
mbalimbali za wananchi zimekuwa ni chanzo ya magonjwa ya mlipuko ikiwepo
kipindupindu na kuhara.
Akizungumza na CPC
Blog mmoja wa wakazi wa Mtaa wa Bonanza jijini hapa Cosmas Mathias amebainisha
kuwa pamekuwepo na tabia ya baadhi ya wananchi kuzibua vyoo vyao
hali ambayo husababisha maji machafu kuzagaa na kutiririka barabarani jambo
ambalo ni hatari kwa afya ya wapita njia wakiwemo watoto na watu wazima.
“Kwa kweli hali kama
hii si nzuri maana unavyoona maji haya yamekosa mwelekeo na kusababisha kuzagaa
ovyo njiani kuna sehemu choo kimezibuliwa, sisi wananchi wakati mwingine
tumekuwa tukisababisha sisi wenyewe mlipuko wa magonjwa na kuilaumu serikali
bure na ukiangalia sasa tunaelekea kwenye mvua za masika na hali itakuwa mbaya zaidi.” Amebainisha Mathias
Mtandao huu umepata fursa ya kuzungumza na
mmiliki wa nyumba ambayo imekuwa kero kwa utiririshaji wa maji machafu mtaani
hapo jina lake limehifadhiwa alibainisha kuwa eneo nyumba ilipo kuna
unyevunyevu ndio maana hutokea hali kama hiyo ya choo kujaaa na inapotokea
hali kama hiyo wakati mwingine huwa hana fedha kukodi gari la kufyonza uchafu
chooni
“Kwa kweli katika eneo
hili kuna changamoto pia ya chemchem[unyevunyevu]sasa inapotokea hali kama hii
wakati mwingine pesa sina lakini huwa najitahidi na kama
unavyoona kuna unafuu, na kitu kingine njia zinatakiwa ziboreshwe pawe na
mifereji ya kupitisha maji taka maana mji huu unazidi
kukua na hakuna mtu anayependa mwenzake apate ugonjwa”amebainisha.
Kwa upande wake mjumbe
wa serikali ya mtaa huo kitengo cha Afya Bi.Kalunde Issa Tumbo
amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo katika mtaa huo ambapo amebainisha
kuwa jambo la utiririshaji maji taka katika mtaa huo imekuwa changamoto .
“Kwa kweli katika
mtaa huu pamekuwa na changamoto hata wakati nakuja ofisini nimekuta kuna
maji taka yaliyochangamana na vinyesi yanazagaa barabarani na mara nyingi
tumekuwa tukisuluhisha migogoro hii kwani wananchi wamekuwa wakileta kero “amesema.
Hata hivyo,Bi.Tumbo amesema usafi ni wajibu wa
kila mtu na usafi ni amri na wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kwa wamiliki
wa nyumba ambapo wamekuwa wakikaa muda mrefu bila kuzibua vyoo vyao.
Pia, amebainisha kuwa
maji taka yaliyoambatana na vinyesi kutapakaa ovyo barabarani kuna sababishwa
na sababu kuu mbili zikiwemo uzembe wa wamiliki wa nyumba kukaa muda mrefu bila
kuzibua vyoo pamoja na miundombinu ya mfumo wa maji taka kuchakaa.
Katika hatua nyingine
Mganga Mkuu wa Serikali,Prof. Abel Makubi amewataka wananchi kuchukua tahadhari
dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwakuzingatia suala la usafi kufuatia mvua
zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo mbalimbali hapa nchini.
Prof.Makubi amebainisha
hayo hivi karibuni Jijini Dodoma wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu wanachi kuchukua tahadhari na njia za kuepuka
magonjwa ya mlipuko katika kipindi cha mvua za Vuli kuelekea Masika
ambazo zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Prof.Makubi amesema
kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ni wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa wa
kuibuka kwa magonjwa kama ya kuhara ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, kuhara
damu na yale yanayoenezwa na Mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue endapo
wanachi hawatazingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema.
“Wote tumeshuhudia
kuanza kujitokeza kwa uharibifu wa mioundombinu ikiwemo ile ya kusafirisha na
kuhifadhia maji safi na taka ambapo hali hii inaweza kuhatarisha afya ya jamii
na kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya
kuambukiza na yale ya mlipuko,”amesema.
Aidha amesema
kwa sababu hiyo Wizara imeona bora kutoa taarifa na tahadhari
kwa umma ili kuweza kuchukua tahadhari na kuelekeza njia za kujikinga dhidi ya
magonjwa hayo.
“Ili kuweza
kuandika historia ya kutokomeza kabisa kipindupindu na magonjwa mengine hatuna
budi kukumbushana na kuchukua tahadhari kwa kila mwanachi, Taasisi na viongozi wa
ngazi zote ili kujikinga na kuzingatia kanuni za afya kwa kuchemsha maji ya
kunywa au kutibu kwa dawa maalum kama waterguard kabla ya kuyatumia na
kuhakikisha maji ya kunywa na yale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika
vyombo safi,” amesisitiza.
Prof.Makubi ameendelea
kufafanua ni vyema kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika
mazingira yasiyo safi na salama, kutumia vyoo ipasavyo na kunawa mikono
kwa maji safi yanayotiririka na sabuni mara kwa mara kabla ya kula baada
ya kutoka chooni,baada ya kumuhudumia mgonjwa pamoja na kuosha matunda kwa maji
safi kabla ya kula.
Pia amewataka
wananchi kuongeza usimamizi wa usafi wa ujumla na mikono katika maeneo ya
mikusanyiko kama mashuleni, Vyuo na Masoko, kutotapisha vyoo au kutiririsha
maji taka, kujikinga dhidi ya kuumwa na mbu muda wote na kutumia ipasavyo
vyandarua
Aidha, amewataka
waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa
Serikali za Mitaa,wananchi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila eneo lililo
chini yao haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko.
Hata hivyo. Prof.Makubi
amesema kutokana na jitihada zinazofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii Jinsia,Wazee na Watoto hakujaripotiwa mlipuko wa ugonjwa wa
kipindupindu kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu hadi sasa.
“Tanzania imepiga
hatua kubwa katika kudhibiti magonjwa haya ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu
ambao ulikoma Julai 2019 na hii inatokana na jitihada kubwa za maboresho ya
miundombinu ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi na
salama pamoja na ushirikiano mzuri wa wanachi,” amesema.
Wakati huohuo, katika
kuadhimisha miaka 21 ya Kumbukizi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarange Nyerere Octoba 14, Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa
kushirikiana na kampuni ya Green Waste walifanya shughuli mbalimbali za usafi
wa Mazingira katika kata ya madukani jijini hapa.
Akizungumza na Mtandao
huu mara baada ya kufanyika kwa usafi huo Afisa Mazingira wa Jiji la Dodoma
Bwana Ally Mfinanga amesema walisafisha mitaro ya maji ya mvua kwani wakati
mwingine huwa kuna changamoto ya taka ngumu hivyo kusababisha kuziba ndio maana
wamefanya usafi huo kwaajili ya kuzibua mifereji ili maji yaweza kupita
kiurahisi bila kuleta athari hususani kwa wafanyabiashara na wakazi ambao wako
kata hiyo.
Alisema mifereji hiyo
imejengwa mahususi kwaajili ya kupitisha maji ya mvua na si kwaajili ya kutupa
takataka.
Kwa upande wake
Sebastian Mkomagi ambaye ni Mwakilishi wa Kampuni ya Green waste
inayojishughulisha na ufanyaji usafi katika jiji la Dodoma alisema wao wakiwa
kama wadau wa mazingira wameamua kuadhimisha siku hiyo kwaajili ya kufanya
usafika lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba wanaweka mazingira katika hali ya
usafi.
Katika
hatua nyingine ,mratibu wa shughuli za vijana kutoka Raleigh Tanzania
Society Jonathan Ngonyani alisema ni vyema jamii pia ikawa na
tabia ya kusoma sheria mbalimbali ikiwemo hizo za mazingira kuendelea kuyatunza
mazingira kikamilifu na kushiriki kuwachukulia hatua wanaokwenda kinyume na
vifungu vya sheria.
0 Comments