📌NA HAMIDA RAMADHANI
WATUMISHI wa Shirika la posta Tanzania wametakiwa
kuwajibika katika utendaji kazi wao ili kuleta chachu ya mabadiliko katika
shirika hilo na serikali kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya
Mawasiliano, Dk.Zainabu Chaula, wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa
Shirika la Posta Tanzania .jijini hapa .
Amesema ni wajibu kwa kila meneja wa Shirika la Posta
kuweka malengo ya makusanyo na kuongeza wigo ili kujitangaza zaidi kwa huduma
zinazotolewa na shirika hilo.
Aidha amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa bidii ili kupata
matokeo mazuri katika kuhudumia jamii na kupata fursa kiuchumi.
Posta mnajukumu la usafirishaji vitu mbalimbali vya taasisi za umma kwa mfano Wizara ya Afya inawatumia kusafirisha sampuli za damu, sampuli za vitu vingi hadi maabara ya Taifa.Dk.Zainabu Chaula
“Lazima katika kipindi cha miaka mitano ijayo tufike
uchumi wa juu, lakini tutafikaje kama hatuna uwajibikaji wa pamoja wa matokeo,
tupo Tanzania ya kidigitali, tunatumia mifumo, anuani za makazi, posta
kiganjani hakuna haja ya kukimbizana na daladala, tuma mzigo kwa njia ya posta
na utafikishiwa hadi nyumbani wakati unafanya kazi nyingine,”amesema.
Dk.Chaula amelitaka shirika hilo kujiimarisha zaidi kwenye
utoaji huduma na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya kwanza barani Afrika na
ulimwenguni kwa utoaji huduma.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mang’ombe alisema
mafunzo hayo yamewakusanya mameneja wa shirika hilo wa mikoa yote nchini ili
kuweka mikakati juu ya kuongoza shirika kwa pamoja.
“Tunatengeneza kitu cha maelewano ya pamoja, kwanini sisi ni
viongozi, kitu gani tufanye ili twende mbele, tumekusanyika hapa ili kuangalia
majukumu yetu ya kila siku, kila mtu apate kupangiwa majukumu na kuyasimamia
ili kupata matokeo chanya,”amesema.
Amesema shirika hilo lina majukumu mbalimbali ya kuwahudumia
wananchi, ikiwemo barua, usafirishaji wa nyaraka muhimu(EMS), kaunta na Wakala
na kuna taasisi zaidi ya 350 ambazo zinatumia huduma ya posta huku watanzania
asilimia 50 wanatumia huduma hizo.
Posta imejiandaa kiutendaji kazi, Posta ndio tulikuwa wasafirishaji wakubwa wa sampuli za Corona na tumefanya kwa asilimia 100, tulipeleka Dar es salaam ndani ya saa 24Hassan Mang’ombe
Ameeleza kuwa tayari wamejipanga kwa kuwa na wafanyakazi na
pikipiki za kutosha ili kusafirisha sampuli ambapo ilianza kazi hiyo
tangu mwaka 2012.
“Tunafanya kazi kila siku, kadri soko linavyopanuka na sisi tupo
tayari kuwahudumia watanzania,tunataka Tanzania iwe kama kijiji, ukienda kwenye
mifumo ya posta, unafungua maduka mbalimbali na kununua bidhaa yeyote,”amesema.
0 Comments