📌NA JASMINE SHAMWEPU
WAMILIKI wa leseni za
madini wametakiwa kufika katika ofisi za kanda zao kwa ajili ya kuhakiki leseni
bila kufanya hivyo watanyang’anywa leseni hizo.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari jijini Dodoma,Katibu Mtendaji Tume ya Madini Profesa Shukrani
Manya amesema zoezi la uhakiki wa leseni za madini nchini limeanza rasmi wiki
hii na linatarajiwa kuhitimishwa Novemba
2 mwaka huu.
Amesema,Tume hiyo imapanga
kuendesha zoezi la uhakiki wa leseni zote za madini kwa kipindi hicho kirefu
ili kutoa mwanya kwa kila mmiliki wa leseni kupata muda wa kuhakiki leseni yake
huku akisema wamiliki wote wanatakiwa kufika kwenye ofisi za madini za hizo za
madini wakiwa na leseni zao halali na taarifa muhimu zinazohusiana na leseni
zao.
Amesema mambo muhimu
ya kuhakiki ni pamoja na uhalali wa leseni husika,ili kujua leseni ambazo
hazijaendelezwa na leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango la mwaka .
Aidha amewataka
wamiliki wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini wenye mapungufu
kuyarekebisha ndani ya siku 30 kuanzia jana.
Prof.Manya amesema
miongoni mwa mapungufu hayo ni pamoja na maombi yaliyokosa viambatanisho
muhimu,maombi ambayo hayajalipiwa ada na waombaji ambao walikidhi vigezo vya
kupewa leseni lakini kwa namna moja ama nyingine hawajalipa ada za maandalizi
pamoja na wamiliki ambao leseni zao zimeshatolewa na lakini hajachukua.
Leseni za walioomba uchimbaji wa kati zipo 15 na leseni za utafutaji madini zipo 96, mmiliki au mwombaji atakayeshindwa kuwasilisha mapungufu yaliyoainishwa baada ya uhakiki zitafutwa kwa mujibu wa sheria.Profesa Manya
Kwa mujibu wa Profesa
huyo maombi yote ya leseni za utafutaji na uchimbaji yenye mapungufu
yataondolewa kwenye mfumo wa uombaji leseni ili wenye sifa waweze kuomba maeneo
hayo.
Pia ametumia fursa
hiyo kuwaagiza maafisa madini wakazi wote waweke dawati la uhakiki katika ofisi
zao kwa kipindi chote cha zoezi la uhakiki huo.
Awali Kamishina
wa Tume ya Madini Profesa Abdulkareem Mruma ameoneshwa kushangazwa na
kitendo cha wamiliki wa leseni mbalimbali kupewa leseni hizo baada ya kukidhi
vigezo lakini hawajachukua leseni zao.
Profesa Mruma pia
amesema Wizara ya Madini tayari imeshatunga na kukamilisha kanuni za uongezaji
thamani madini za mwaka 2020 kanuni ambazo amesema ndio zitatumika katika
kusafirisha madini ambayo yameongezwa thamani.
Amewataka wateja
watumie kanuni hizo ili waweze kupeleka nje ya nchi madini ambayo yameongezwa
thamani huku akiwaomba ambao hawakusafirisha madini siku nyuma watumie kanuni
hizo katika kuongeza thamani na ubora kwa viwango vilivyoainishwa.
Ikumbukwe kuwa mwaka
2017 Serikali ilifanya marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo pamoja
na mambo mengine ilizuia usafirishaji makinikia na madini ghafi kwenda nje ya
nchi baada ya kubaini udanganyifu na upotevu mkubwa wa mapato ya serikali
wakati wa usafiorishaji wake.
0 Comments