NA FARAJA
MPINA, WUUM, DODOMA
Katibu
Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt.
Zainabu Chaula ametunuku vyeti kwa wahitimu 24 waliopatiwa mafunzo ya
teknolojia mpya ya 5G yaliyotolewa na Kampuni ya simu ya Huawei Tanzania katika
hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano uliopo Mji wa Serikali, Mtumba mkoani Dodoma.
Wahitimu
wa mafunzo hayo ni wataalamu watano 5 kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), wataalamu 8 kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wataalamu
10 kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na mtaalamu mmoja kutoka Tume
ya Taifa ya TEHAMA.
Dkt.
Zainabu Chaula amewapongeza wahitimu kwa kumaliza mafunzo hayo ambayo yamefanyika
nje ya muda wa kazi na kuwashukuru Huawei Tanzania kwa ushirikiano wao endelevu
na kuwawezesha watumishi wa Sekta ya
Mawasiliano pamoja na taasisi zake kuifahamu teknolojia mpya ya 5G.
Dkt. Chaula
amesema kuwa kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA yenye kasi zaidi, itawezesha
Serikali kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza makusanyo ya mapato ambayo yataliwezesha
Taifa la Tanzania kutoka uchumi wa kati na kwenda katika uchumi wa juu.
Naye Afisa
TEHAMA kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano),
Mhandisi Aweso Aweso ambaye ni mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo amesema kuwa,
teknolojia mpya inapotambulishwa ni jukumu la wataalamu wa Serikali kujifunza
na kuielewa ili kuwawezesha katika kutunga Sera, ambazo zitasaidia kusimamia
mwenendo mzima wa miundombinu ya TEHAMA na matumizi ya huduma za mawasiliano.
Aliongeza
kuwa teknolojia ya 5G ni teknolojia yenye sifa za ziada kwa sababu ina akisi
akili za binadamu, hivyo itasaidia Serikali kutoa huduma bora na za uhakika kwa
wananchi wake kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye kasi.
Naye
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Huawei Tanzania, Damon Zhang amesema Tanzania
imeboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya TEHAMA kwa kuhakikisha kila kona
ya nchi imefikiwa na miundombinu hiyo, hivyo nchi kuweza kuleta mabadiliko ya
kweli na kuipeleka Tanzania katika
uchumi wa viwanda.
Akizungumza
katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya TEHAMA amesema
kuwa Sekta ya Mawasiliano ina jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata huduma
zenye viwango bora zaidi, na mafunzo yaliyotolewa na kampuni ya Huawei Tanzania
ni hatua nzuri ya kuwajengea uwezo wataalamu ili kuleta ushindani na mataifa
mengine.
Mkurugenzi
wa TEHAMA wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano)
Mulembwa Munaku amesema kuwa mafunzo hayo ya teknolojia ya 5G ambayo yametolewa na Kampuni ya Huawei
Tanzania kwa wataalamu wazalendo watanzania ambapo yamejikita katika masuala
yanayohusu teknolojia mpya ya 5G katika usimikaji wa miundombinu, usambazaji wa huduma za mtandao, mahitaji ya mpangilio
na mgawanyo wa masafa, mpango wa
biashara na usimamizi wa teknolojia mpya ya 5G.
Munaku ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya teknolojia
mpya ya 5G kwa wataalamu wengine wa Serikali ili kuhakikisha kuwa wananchi
wananufaika na teknolojia mpya.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 Comments