📌NA DOTTO KWILASA.
KILA ifikapo
Disemba tisa ,Tanzania huadhimisha uhuru wa Tanzania Bara ambapo zamani ilikuwa
ikijulikana kama Tanganyika kabla ya kuungana na visiwa vya Zanzibar na kuunda
neno huru Tanzania.
Ikiwa imebaki miezi miwili kuingia katika
kipindi cha historia ya uhuru wa Tanzania Bara uliopatikana tangu mwaka
1961 na kuifanya Tanzania kuwa huru kwa miaka 56 sasa,ni wazi kuwa jamii
inapaswa kuwakumbuka na kuwaenzi wanawake waliopigana kufa na kupona
kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za kuikomboa Tanganyika.
Wapo wanawake wengi waliojitoa kuipigania nchi
hii ya kizalendo ambao majina yao yamo katika historia.
Hata hivyo michango mingi ya
wazalendo wanawake imefichwa na kuwafanya wasijulikane kabisa
katika historia japo tunapaswa kuwashukuru na kuzidi kuwaombea kwa Mwenyezi
Mungu.
Hivyo basi,hatuwezi kuuzungumzia uhuru wa
Tanzania bila kuwahusisha wanawake waliochochea maendeleo ya kuwa na Taifa
huru.
Hapa namaanisha hatuwezi kuiadhimisha siku hii
bila kumkumbuka mwanaharakati mmoja wa wanawake wa kwanza
wazalendo kujiunga na harakati za kuikomboa Tanganyika na
huyu si mwingine ni Bibi Titi Mohamed .
Bibi Titi
Mohammed ni jina linalojulikana kwa wakongwe huku vijana wa kizazi cha
sasa wengi wao hawamjui wala kufahamu harakati zake katika ukombozi wa
Tanganyika.
Titi Mohamed
Salim Mandwanga alizaliwa jijini Dar es Salaam mwaka 1926 ,na tarehe 5 Novemba
mwaka 2000 alihitimisha safari yake ya kuishi duniani kama ilivyoandikwa katika
vitabu vyote vya dini.
Katika maisha
yake Mama huyu alipenda uhuru na haki na kuamua kuvisimamia vitu hivi kwa
vitendo na kuamua kujiingiza kwenye masuala ya siasa.
Siasa ilimweka
akawa rafiki wa karibu wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere
aliyetambulishwa kwake mwaka wa 1954, na dereva wa familia ya Rais
huyo kutokana na imani ya usawa aliyokuwa nayo Baba wa Taifa.
Kwa wakati
ule wanawake kujulikana ilikuwa ni mtazamo mbaya kwa jamii kwani
jamii ilijiwekea imani kuwa kazi kubwa ya mwanamke ni kushughulikia familia
pekee.
Titi Mohamed
alikuwa mmoja wa wanachama waanzilishi wa TANU(Tanganyika African National
Union), ambacho kilikuwa chama kikuu cha kisiasa ndani ya Tanzania , na
alifanya jukumu kubwa katika kupambana na uhuru wa Tanzania.
Kutokana na kipaumbele kikubwa cha sera ya Nyerere, aliwahimiza wanawake ikiwa
ni pamoja na kuihimiza jamii kutambua kuwa binadamu wote ni sawa hivyo kumtoa
Bibi Titi kwenye jukwaa alilohitaji ambapo alikuwa kiongozi wa
mlengo wa wanawake wa TANU, yaani Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).
UWT ilikuwa chanzo
kikubwa cha uwezeshaji kwa wanawake nchini Tanzania ambapo
kilileta mafanikio ya ajabu na kutoa historia iliyokuwa imezoeleka
ya kuwadhoofisha wanawake na kuwaona hawafai.
Hata hivyo
,mnamo Oktoba 1969, Bibi Titi, na Waziri wa zamani wa Kazi Michael Kamaliza
walikamatwa, pamoja na maafisa wa jeshi wanne, wakishtakiwa kwa kupanga mpango
wa kupindua serikali kutokana na kutokubaliana kwa baadhi ya mambo ndani ya
chama hali iliyomfanya kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Taarifa zinaeleza zaidi kuwa
,miaka miwili baadaye yaani mwezi wa Aprili 1972, Bibi Titi alipokea
msamaha wa Rais.
Baada ya
kutolewa kwake, machungu na mateso yalianza kwa mwanamke huyu
mzalendo (Bibi Titi) ambapo alianza kuishi maisha ya kutengwa na
jamii yake iliyokuwa ikimpenda mwanzo.
Unajua nini
kilitokea? washirika wake wa kisiasa walimpinga, rafiki zake wengi walimkataa
na kumwona kuwa hafai kuambatana nao lakini kubwa zaidi ni hili la mume wake
aliyempenda na kumuamini sana kumtaliki kutokana na mfumo dume
uliokuwapo wakati ule hali iliyozidi kuamsha ari ya mwanamke huyu katika
kupambana kwa nguvu zote kusimamia kile alichokiamini kuwa kitamfanya kuwa
huru.
Hayo ni baadhi tu
ya mambo yaliyomtokea mwanaharakati huyu mwanamke anayetazamwa na wegi kama
mzalendo wa kweli na hatimaye kufanikiwa kufikia malengo ambapo mnamo mwaka
1991, wakati Tanzania ilipokuwa ikisherehekea miaka 30 ya uhuru, Bibi Titi
kinara wa ushindi na kuwahamasisha wanawake wengine kuiga mfano wake.
Hata hivyo kila
lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho,mnamo Novemba 5, 2000 mama huyu alifariki
kwenye hospitali ya huduma ya afya huko
Johannesburg nchini Afrika ya Kusini ambako alikuwa akipatiwa
matibabu.
Kutokana na umuhimu wake katika Taifa hili ambalo kwa sasa ni huru ,Serikali
iliona ni vema kumuenzi kwa namna ya pekee ili kumhifadhi katika kumbukumbu kwa
vizazi vijavyo.
Moja ya
barabara kuu za jiji la Dar es Salaam inaitwa jina la Bibi Titi
Mohamed kwa heshima ya mafanikio makubwa yaliyotolewa na yeye
kuelekea uhuru wa Tanganyika.
Kubwa zaidi
ni matumizi ya lugha ya kiswahili katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambapo inasemekana akiwa waziri alishauri lugha hii kutumika na
kuwaweka watu pamoja badala ya kiingereza .
Huyo ndiye shujaa
wa kike aliyepigania uhuru wa Tanganyika,nakukumbusha msomaji wa makala haya ya
Sauti
ya Mwanamke kuwa vielelezi vingi katika makala haya ni kwa hisani ya
mtandao.
Kwa
maboresho ya ukurasa huu usisahau kuwasiliana nasi kupitia barua pepe habaricentral4@gmail.com au
kupitia dottokwilasa@gmail.com.
0 Comments