📌NA MWANDISHI WETU
TUZO za muziki wa dansi nchini Tanzania kwa
wanamuziki waliofanya vizuri mwaka 2020 zitafanyika jijini Dodoma mwezi
Desemba.
Tuzo hizo maarufu kama Cheza Kidansi Music Awards
zilizozinduliwa mwaka 2019 zitahusisha vipengele 11.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni ya
Cheza Kidansi Entertainment ya jijini Mwanza, imebainika kuwa tuzo hizo
zitakuwa na maboresho mengi kwa mwaka huu.
Bernard James amesema vipengele vya mwaka huu ni bendi
bora, wimbo bora, video bora, mtunzi bora, mwandaaji bora, mwimbaji bora, rapa
bora, hall of fame, chipukizi bora, best collabo na mwanamuziki bora.
Hivi vipengele vimeidhinishwa na academy iliyosheheni wataalamu wa muziki nchini waliokaa pamoja mwaka mzima wakivichambua kwa umakini mkubwa
Bernard James
Amesema baadhi ya vipengele mfano msanii bora,
mnenguaji bora, mpigaji bora vyombo, mwanamuziki toka Kongo vimeondolewa ili
kuweka chachu kwa vipengele vilivyopitishwa na kukuza muziki wa dansi nchini.
Mkurugenzi huyo wa Cheza Kidansi pia amebainisha
kuwa mwaka huu ushindani utakuwa mkubwa sana kutokana na tuzo za mwaka jana
kuchochea wanamuziki kutoa kazi nyingi na bora zaidi.
Mfano wa eneo ambalo mwaka huu litakuwa na upinzani mkali ni kwenye rapa bora ambapo marapa wenye majina karibu wote wameshiriki nyimbo nyingi zikiwemo zao na za bendi zingine
Bernard James
Alipoulizwa kwanini tuzo mwaka huu zitatolewa
Dodoma, Bernard amefafanua kuwa lengo ni kusogeza tuzo hizi katika mikoa
mbalimbali na kuamsha mashabiki wa dansi nchi nzima.
Mwanamuziki mkongwe Nyoshi El Sadaat akipokea
tuzo yake katika msimu wa kwanza wa tuzo za muziki wa dansi.
Kwa upande wa zawadi amesema zawadi ni za aina yake,
za kisasa na zitakazowainua zaidi wanamuziki morali na ubunifu.
Kuhusu wadhamini, Mkurugenzi huyo amewaomba
wafanyabiashara, wajasiriamali, wadau wa burudani na wamiliki wa makampuni na
taasisi mbalimbali jijini Dodoma na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi
kudhamini tuzo hizo ili kutangaza pia bidhaa zao, huduma na makampuni kupitia
vyombo mbalimbali vya habari na mitandao itakayotangaza tukio hilo mwanzo hadi
mwisho.
Amezitaka bendi na wanamuziki mbalimbali waliotoa
kazi mwaka huu kutunza taarifa za kazi zao ili kurahisisha zoezi la kuwapata
washindi. Amewaomba pia kutembelea mtandao wa Cheza Kidansi kupata taarifa za
tuzo.
Tuzo za Cheza Kidansi tangu zianzishwe mwaka 2019 zimejizolea umaarufu mkubwa huku zikichochea wanamuziki kutoa kazi nyingi na bora mwaka huu.Burudani mbalimbali za dansi zitatolewa sambamba na utoaji wa tuzo hizo mwishoni mwa mwaka huu.
0 Comments