📌NA BEN BAGO
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la
Dodoma mjini kimezindua kampeni zake za Ubunge katika jimbo hilo huku mgombea
wake Aisha Madoga akibanisha vipaumbele vyake ikiwemo kukuza uchumi kwa wananchi
wa jimbo hilo.
Akizindua kampeni hizo katika viwanja vya shule ya
msingi Chang’ombe Aisha Madoga amewaambia wakazi wa jimbo hilo iwapo atapewa
ridhaa ya kuwa mbunge atahakikisha anakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja katika jimbo
hilo la Dodoma mjini na hatokubali kuona wafanyabiasha wadogo wadogo wakilipishwa kodi na ushuru mbalimbali kutoka kwenye mitaji yao midogo.
Madoga amesema anazijua shida za watu wa Dodoma
hivyo akiingia bungeni jambo la kwanza ni kuhakikisha anafanyia kazi changamoto
zinazowasumbua wakazi wa jimbo hilo kwa muda mrefu.
Pia ameahidi kupambana kuhakikisha wakazi wa Dodoma wanamiliki ardhi yao kwa mujibu wa sheria bila usumbufu kutoka kwenye mamlaka husika.
Uchaguzi wa 2015 tuliwahidi kuwa tukipewa mamlaka tutaivunja CDA ili isiendelee kula ardhi ya Dodoma,lakini wakaivunja wakawapa mamlaka halmashauri ambako pia ardhi ya watu inaendelea kuliwa
Aisha Madoga
Akizungumzia miundombinu katika jimbo la
Dodoma,mgombea huyo amesema bado kuna maeneo ya jimbo hilo barabara ni tatizo kubwa hivyo akipata ridhaa ya kuwa
mbunge atahakikisha maeneo hayo yanafikika muda wote.
Madoga amesema kiupambele chake kingine ni kuboresha
huduma za afya katika jimbo hilo
ikiwemo ujenzi na uboreshwaji wa vituo vya afya.
Kata kibao zipo mjini Dodoma lakini hakuna huduma za afya,hakuna huduma za haraka.Watu wanapoteza maisha kwa kuwa kuna huduma za afya duni
Aisha Madoga
Awali akimkaribisha mgombea huyo,mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya kati ambaye pia ni mgombea wa Ubunge wa jimbo Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu amewataka wapiga kura wa Dodoma Mjini kumuamini na kumpa kura mgombea huyo pamoja na madiwani wa chama hicho kwa maendeleo ya jimbo hilo.
Pamoja na hilo Nyalandu amewataka wale wote
waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze siku hiyo ili kutumia haki yao ya kikatiba
ya kuchagua kiongozi wanayempenda.
Najua wapo wanaotusikilizia wakiwa majumbani wanaogopa kuja hapa uwanjani,Umsijali!CHADEMA inahitaji kura yako,msiogope nendeni mkapige kura Oktoba 28.
Nyalandu
0 Comments