📌NA.FAUSTINE GALAFONI
WAHANDISI nchini
watakiwa kufanya kazi kwa ueledi,uzalendo na kwa kufuata maadili ya taaluma
yao.
Rai hiyo imetolewa leo
jijini Dodoma na Katibu Mkuu kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi katika
mkutano mkuu wa 17 wa bodi ya usajili wa wahandisi nchini ambapo
amebainisha kuwa fani ya uhandisi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa hivyo ni
wanapaswa kufanya kazi kwa ueledi kwa kuzingatia maadili na matakwa ya taaluma
yao .
Nitoe pongezi kwa wahandisi kwani mna mchango mkubwa ,muendelee kufanya kazi kwa uzalendo,na bodi ya usajili wa wakandarasi (ERB)iendelee kuwachukulia hatua wakandarasi wasiokuwa waaminifu,bodi bado mna jukumu kubwa kuhakikisha wakandarasi wasiokuwa waaminifu na wanaoenda kinyume na taaluma zao wanachukuliwa hatua. Balozi Mhandisi John Kijazi
Aidha,Balozi Kijazi
amebainisha kuwa ni muhimu kwa wahandisi kuwa wabunifu ,wadadisi katika
kusukuma mbele gurudumu la maendeleo hususan katika kipindi hiki cha mapinduzi
ya nne ya viwanda.
“Tupo katika Mapinduzi ya 4 ya viwanda toka karne ya 18 hadi leo karne
ya 21 ni lazima wahandisi wawe wabunifu ,mitaala ya vyuo lazima izingatie
mapinduzi ya viwanda ,wahandisi ni vyema kushirikiana na taasisi zingine katika
kufanikisha masuala ya teknolojia”amebainisha.
Katika hatua nyingine
Balozi Mhandisi Kijazi ameainisha baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na
serikali ambapo mchango mkubwa unatokana na wahandisi ikiwa ni pamoja na Bwawa
la Ufuaji wa umeme la Rufiji ,Mradi wa wa Reli ya Kisasa(SGR),upanuzi wa
miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami huku pia akigusia ongezeko la
ajira .
Katibu mkuu Wizara ya
Ujenzi,Uchukuzi na mawasiliano Elius Mwakalinga amesema kuwa kwa kuwa maendeleo
yanasimamiwa moja kwa moja na wahandisi ni vyema kulipa kipaumbele suala la
wahandisi ambapo pia amebainisha kuwa Wizara inatumia gharama kubwa kuwasomesha
wahandisi hivyo itahakikisha wahandisi wanabaki hapa nchini kulitumikia
taifa.
Pa Mwakalinga
amebainisha kuwa wahitimu 351 wa fani ya uhandisi wameshikizwa katika taasisi
zilizo chini ya wizara na ametoa rai kwa taasisi zingine kuwaendeleza
wahandisi.
Kwa upande
wake,Mwenyekiti wa bodi ya usajili wa Wahandisi Tanzania(ERB)Mhandisi Prof.Ninatubu
Lema amesema lengo la mkutano huo wa mwaka ni kubadilishana uzoefu na
kujengeana uwezo pamoja na kuwatambua wahandisi wapya waliohitimu ambapo
pia amebainisha kuwa hadi sasa Tanzania ina jumla ya wahandisi 29,000
waliosajiliwa na bodi hiyo.
Aidha,Mhandisi
Prof.Lema amesema Tanzania ina lengo la kufikisha wahandisi 80,000 ifikapo
mwaka 2025 ambapo pia zaidi ya wahandisi 452 wameapishwa katika mkutano mkuu wa
17 wa wahandisi nchini.
Naye Msajili wa bodi
ya Wahandisi Mhandisi Patrick Balozi amesema bodi hiyo imeanzisha chombo cha
kuendeleza wahandisi huku akibainisha miongoni mwa majukumu ya bodi hiyo kuwa
ni pamoja na kusajili wahandisi,kuwaendeleza pamoja na kusimamia miiko ya
wahandisi.
Kwa upande wake,Mkuu
wa mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge ametoa wito kwa vijana kuacha kuogopa
kujaza fomu kwa ajili ya kusomea uhandisi kwani mahitaji yake ni makubwa huku
akitoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwamo wahandisi kuwekeza viwanda ikiwemo
uongezaji thamani katika zao la zabibu .
Akitoa salam kutoka
ubalozi wa Norway,Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ms. Elisabeth
Jacobsen akizungumza kwa njia
ya video kupitia Mtandao wa ZOOM kwenye mkutano huo amesema serikali ya
Norway itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha sekta ya uhandisi
inaendelea kukua huku akiipongeza serikali ya Tanzania kwa kuendeleza
mashirikiano hayo.
Jumla ya Mada 8
zinajadiliwa katika mkutano huo wa Wahandisi nchini ambapo pia washiriki kutoka
nchini Norway,Botswana ,Uganda,Rwanda,na Kenya wamefuatilia mkutano wa 17 wa
Wahandisi nchini Kwa video kupitia Mtandao wa Zoom na kutoa maoni yao
ambapo mkutano huo unafanyika ukumbi wa mikutano wa Dodoma Convention
Centre ukitarajiwa kuhitimishwa Septemba 4,2020.
0 Comments