CWT,UDOM WAPENDEKEZA MBINU YA KUMALIZA TATIZO LA AJIRA KWA WALIMU

N
📌NA DOTTO KWILASA

CHAMA   cha Walimu Tanzania (CWT) kimesema kinaangalia namna ya  kuishawishi Serikali ili  walimu wanaomaliza masomo yao waweze kwenda kujitolea katika maeneo wanayotoka hasa wale wa vijijini .

Hatua hiyo itasaida  kuondoa tatizo la uhaba wa walimu kwa baadhi ya maeneo ikiwa ni pamona na kuwasaidia walimu hao kuongeza ujuzi na uelewa .

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki Jijini hapa na Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif wakati akizungumza katika kongamano la Mwalimu Baba lao liloambatana na na kuwaaga wahitimu wa mwaka wa tatu wa masomo ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma,(UDOM).

Kongamano hilo liliandaliwa na Chama cha Walimu,Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSTA)

Katibu Mkuu huyo amesema suala la wanafunzi wanaomaliza masomo yao kwenda kufundisha maeneo wanayotoka linachukuliwa kama chachu kwa maendeleo ya elimu hivyo CWT watalifikisha katika sehemu husika .

Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Ndaki ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Profesa Julius Nyahongo kutoa ushauri kwa Serikali kwamba wanafunzi wanaomaliza masomo yao kurudi vijijini na kwenda kufundisha katika shule za Kata.

Tunaambiwa Serikali ina fedha hawa walimu wanapohitimu warudi kwenye vijiji vyao kila mmoja kwenye shule ya Kata afundishe kwa kujitolea lakini awe anapewa fedha kidogo.
 Profesa Nyahongo.


Vilevile Prof. Nyahongo  ameshauri kuwe na Mfuko  maalum kwa ajili ya kushughulikia walimu ambao wanamaliza masomo yao ili yule mwenye nidhamu ndio awe wa kwanza kuajiriwa.

“CWT msiwaache walimu suala hili lichukueni nyinyi mna nguvu nawaambia shule hazitakosa walimu lakini lazima wapatiwe fedha za kujikimu,”amesema Profesa Nyahongo.

Aidha,amesema kuna baadhi ya watu walikuwa  wakibeza shule za Kata ambapo kwa sasa zimekuwa msaada mkubwa ambapo wanafunzi wengi wamesoma na kufaulu.

“Wakati shule hizi zinaanza watu walibeza sana,hakuna walimu hebu niambie sasa hivi unasikia kuna tatizo la walimu? Hawa walipo hapa wakimaliza hakuna tena tatizo la walimu na Udom ndio ilimaliza tatizo lile kwa miaka 10  wamezalishwa walimu 8000,”alisema.

Wakati huo huo Katibu huyo wa CWT amesema Chama hicho kinajuwa kwamba wakati wa upandishaji wa vyeo mwaka 2019-2020 kulikuwa na changamoto ya waraka kuwaacha walimu waliokuwa masomoni ambapo alidai jambo hilo wameliona na wameishaliwasilisha kwa Mamlaka husika.

“Mwaka 2020 kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kwa wanachama kukijua chama chao,Takwimu zinaonesha kwamba walimu waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali walikuwa zaidi ya 91,000 sawa na asilimia 45.Hii  haijawahi kutokea.

“Tunaendelea na utetezi wa kesi mbalimbali na kwa taarifa ya mwisho  iliyowasilishwa kwenye mkutano CWT kupitia wanasheria wake tumeshinda kesi kwa zaidi ya asilimia 98,”alisema Seif.

Aidha,Komredi Deus Seif amewapongeza Chama cha Walimu,Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSTA) kwa malengo waliyojiwekea ya  kuwaunganisha walimu tarajali na walimu waliopo kazini ili kushirikiana  na kubadilishana uzoefu kuhusu taaluma ya ualimu.

Kuhusu la kuanzisha matawi mengine,katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu tayari tumelifanyia kazi na tumeanzisha kitengo Makao Makuu kinachohusika na usimamizi wa Taasisi na Vyuo.
Deus Seif



Awali akisoma risala,Katibu wa Walimu  Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSTA),Emmanuel Elias amesema wanakabiliwa na changamoto za chama chao hakijaweza kusambaa katika vyuo vingine vinavyoandaa walimu kwa ajili ya kupata wanachama.

Pia,wanakabiliwa na changamoto ya vyanzo vya mapato hivyo kujiendesha kwa michango ya wanachama na wadau mbalimbali hasa CWT.

“Wanachama walimu tarajali wamekuwa wakikosa haki zao kama watumishi hasa katika suala la kuzuiwa kupanda madaraja suala hili limekuwa likiwaumiza sana walimu hivyo kuonekana kuwa kujiendeleza kitaaluma ni adhabu,”alisema.

Post a Comment

0 Comments